Programu ya AI yawasaidia wanafunzi wa sayansi Dodoma

Dodoma. Katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuimarisha sekta ya elimu nchini, hususan katika masomo ya sayansi na teknolojia, kituo cha Tanzania School of CommunityNetworkskimeanzisha programu maalumu ya kuwasaidia wanafunzi wa masomo ya sayansi kujifunza kwa kutumia teknolojia ya akili unde (AI).

Programu hiyo inatekelezwa katika kituo kilichopo Nzuguni, jijini Dodoma ikiwa na lengo la kuwajengea vijana uwezo wa kukabiliana na ushindani wa kiteknolojia katika dunia ya sasa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa programu hiyo leo Alhamisi, Machi 5, 2026, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Idara ya Biolojia, Dk Rehema Ulimboka amesema maendeleo ya sayansi na teknolojia yanaendelea kwa kasi kubwa, hivyo kuna umuhimu wa kuwafundisha watoto teknolojia hizo wakiwa katika umri mdogo.

Amesema katika kujadili Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050, sayansi, ubunifu na teknolojia ni mambo yasiyoweza kutenganishwa, hivyo vijana wanapaswa kuandaliwa mapema ili waweze kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali.

“Tunapozungumzia Dira ya Maendeleo ya Taifa kwa upande wa Kiuchumi ya mwaka 2050, hatuwezi kuitenganisha na sayansi, ubunifu na teknolojia. Ni lazima tuwaandae vijana wetu mapema ili waweze kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali,” amesema Dk Rehema.

Amesema programu hiyo inaunganisha teknolojia ya akili unde, sayansi ya jamii, ubunifu pamoja na uchumi, hatua itakayowasaidia vijana kupata ujuzi wa vitendo utakaowawezesha kujiajiri au kupata ajira katika sekta mbalimbali.

Kwa mujibu wa uongozi wa kituo hicho, ni miongoni mwa viwili pekee nchini vinavyotoa mafunzo ya aina hiyo kwa wanafunzi wa sayansi, jambo linaloifanya kuwa fursa muhimu kwa vijana wa Kitanzania.

Dk Rehema amewahimiza vijana kujitokeza kwa wingi kujifunza katika kituo hicho, akisisitiza kuwa mafunzo yanayotolewa ni bure kabisa na hayahusishi gharama yoyote kwa wanafunzi kuanzia ngazi ya shule za msingi hadi vyuo vikuu.

Amesema kuanzishwa kwa programu hiyo ni hatua muhimu katika juhudi za kujenga Tanzania yenye vijana wabunifu, wenye ujuzi wa kisasa na waliopo tayari kushindana katika uchumi wa kidijitali ifikapo mwaka 2050.

Mmoja wa walimu wa masomo ya sayansi kutoka Shule ya Msingi Nzuguni B, Anna Mlimi amesema kuanzishwa kwa programu hiyo kutarahisisha ufundishaji wa masomo ya sayansi kwa kutumia mbinu za vitendo.

Amesema kwa muda mrefu walimu wamekuwa wakifundisha zaidi kwa nadharia, lakini kupitia teknolojia ya akili unde, wanafunzi wataweza kuona na kufanya majaribio kwa njia ya kidijitali, jambo linaloongeza uelewa wao.

Baadhi ya wanafunzi waliopata fursa ya kushiriki mafunzo ya awali pia wameeleza kufurahishwa na mbinu mpya ya ufundishaji inayotumia teknolojia hiyo.

Mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Nzuguni, Mwanahamisi Abdallah amesema awali alikuwa akiona teknolojia ya akili unde kuwa jambo la mbali, lakini sasa ameanza kujifunza namna inavyoweza kutumika hata katika masomo ya sayansi.

Naye mwanafunzi wa kidato cha tano wa Shule ya Sekondari Nzuguni B, Abdukarim Saidi amesema mafunzo hayo yamempa hamasa ya kutaka kuwa mtaalamu wa teknolojia siku zijazo.

Amesema amegundua kuwa teknolojia ya akili unde inaweza kutumika kutatua changamoto mbalimbali za jamii, jambo ambalo limempa ndoto mpya ya kuingia katika taaluma hiyo.