RC TANGA AIPONGEZA NHC KWA UJENZI WA JENGO LA KITEGA UCHUMI MKWAKWANI PLAZA


Na Oscar Assenga, Tanga

MKUU wa Mkoa wa Tanga Balozi Batilda Burian amefanya ziara ya kutembelea Jengo la Kitega Uchumi la Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) “Mkwakwani Plaza” ambalo litagharimu kiasi cha Bilioni 8.6 huku akiwapongeza kwa usimamizi imara na ubora mkubwa.

Akizungumza akiwa katika eneo la mradi huo RC Batilda alisema kwamba ubunifu ambao wameutumia shirika hilo kuanzia hatua ya ujenzi mpaka usimamizi wanafanya wenyewe kupitia wataalamu wao jambo ambalo litawezesha kuwepo kwa ubora.
Alisema kwamba kutokana na uwepo wa fursa hiyo watu wa Tanga wanapaswa kuichangamkia sasa na wasisubiri bali waanze sasa kujiitokeza kuchukua nyumba katika Jengo hilo la kitega Uchumi la NHC

“Nitumie fursa hii kuwahimiza wananchi kuchangamkia fursa zilizopo katika Jengo hili wale ambao wana fedha za mitaji waweze kuzungumza na Meneja wa NHC na leo tumekuja kwenye ziara hapa na kamati ya usalama ya mkoa kukagua ujenzi wa jengo hilo niendelee kuwapongeza NHC kazi inaendelea vizuri na ya viwango vya hali ya juu hongereni sana”Alisema
Aidha alimpongeza Rais Dkt Samia Suluhu kwa kuendelea kusukuma mbela maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo miundombinu na makazi

Awali akizungumza Menej awa Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) Mhandisi Mussa Kamendu alisema kwamba Jengo hilo litakuwa na maeneo ya maduka ,ofisi za kupangisha katika sehemu ya Biashara huku likiwa na Gorofa nne za makazi.

Alisema kwamba katika Jengo hilo eneo la makazi nyumba ya vyuma viwili itakuwa inauzwa kwa kiasi cha Milioni 178 na za vyumba vitatu zitauzwa kwa shilingi Milioni 240 bei zote zikijumuisha VAT.

Aidha alisema kwamba wanawakaribisha wananchi kuchangia fursa ya kuweza kununua vyumba hizo huku akiwashukuru ambao wamekwisha kujitokeza na wapangaji wamepata wengi.

Naye kwa upande wake Mhandisi wa Ujenzi huo Mhandisi Ephahim Fanuel Msigwa alisema kwamva jengo hilo lilianza mwaka 2025 na kwa mujibu wa mkataba wanatakiwa kumaliza mwezi Juni 2027.

Mhandisi Ephahim aliongeza kwamba kupitia mradi huo wametengeneza ajira za kazi 189 na wanawashukuru watu wa Tanga wamejitokeza kwa asilimia kubwa .

Mradi wa jengo hilo la Mkwakwani Plaza ni mradi wa Kisasa ambalo linajumisha sehemu za biashara na makazi na kwamba utajkapokamilika utaongeza thamani ya mji wa Tanga na kutoa fursa zaidi ya ajira na uwekezaji kwa wananchi.