USHINDI wa bao 1-0, ilioupata Fountain Gate dhidi ya Mbeya City katika mechi ya Ligi Kuu Bara, iliyopigwa Machi 3, 2026, kwenye Uwanja wa Sokoine jijini, Mbeya, umemfanya kocha wa timu hiyo, Mohamed Ismail ‘Laizer’ kuandika rekodi mbili mpya, baada ya mwenendo usioridhisha wa matokeo.
Rekodi ya kwanza ambayo Laizer ameiweka sambamba na timu hiyo, ni ya kushinda mechi ya kwanza kwa mwaka 2026 katika Ligi Kuu, huku ya pili pia ni kupata ushindi wa kwanza ugenini msimu huu.
Ushindi huo wa bao 1-0, ulikuwa wa kwanza kwa Lazier mwaka 2026 katika Ligi Kuu Bara, kwani kabla ya hapo, mara ya mwisho kuonja ushindi iliichapa Tanzania Prisons 1-0, kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Manyara, Novemba 26, 2025.
Timu hiyo iliyohamishia makazi yake kwa sasa jijini Arusha ikiutumia Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, tangu ilipoifunga Prisons bao 1-0, Novemba 26, 2025, ilicheza mechi sita na kati ya hizo ilichapwa nne na kutoka sare mbili.
Msimu huu katika mechi 15 ilizocheza Fountain Gate kwenye ligi, ushindi huo wa Mbeya City ni wa kwanza kushinda ugenini, kwani hadi sasa timu hiyo imecheza nane, imeshinda moja tu, sare mbili na kupoteza tano, huku saba ikiwa ya nyumbani.
Ikumbukwe kikosi hicho kilianza msimu huu chini ya Denis Kitambi aliyeongoza mechi mbili ambazo zote alipoteza dhidi ya Mbeya City (1-0 nyumban) na Simba (3-0 ugenini). Baada ya hapo, Laizer akaanza na kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Mtibwa Sugar, ugenini, akaja kuifunga Dodoma Jiji (1-0) nyumbani.
Msimu uliopita wa 2024-2025, Fountain ilimaliza nafasi ya 14 na pointi 29, katika Ligi Kuu Bara na kukutana na Tanzania Prisons iliyomaliza nafasi ya 13 na pointi 31 na kwenye mechi ya mtoano kikosi hicho kilichapwa jumla ya mabao 4-2.
Baada ya hapo, Fountain ikacheza tena ‘Play-Off’, ya kubakia Ligi Kuu, na iliitoa Stand United mabao 5-1, baada ya kikosi hicho cha ‘Chama la Wana’, kinachoshiriki Championship, kuifunga Geita Gold mabao 4-2.
Msimu huu wa 2025-2026, Fountain Gate inashika nafasi ya 13 na pointi 15, baada ya kucheza mechi 15 na imeshinda nne, sare tatu na kupoteza nane, huku ikifunga mabao saba na kuruhusu 18.