Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Ridhiwani Kikwete amewataka Watanzania kuutumia mwezi Mtukufu wa Ramadhani kuendelea kuiombea na kudumisha amani ya Taifa.
Amesema maendeleo ya kiuchumi hayawezi kufikiwa pasipo kuwepo amani na Tanzania imefanikiwa kuwa na mazingira ya amani na kuwa moja ya mataifa yanayovutia uwekezaji.
Waziri Ridhiwani ametoa rai hiyo jana Jumatano Machi 4, 2026 wakati wa hafla ya futari iliyoandaliwa na Shirika la Bima la Zanzibar (ZIC), iliyohusisha wadau mbalimbali zikiwemo taasisi zinazofanya kazi kwa ukaribu na shirika hilo.
“Ni wajibu wetu sote kuhakikisha tunalinda na kudumisha amani hiyo na tutumie kipindi hiki cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani, kuliombea Taifa letu amani na mshikamano vizidi kutawala,” amesema Ridhiwani.
Mbali na hilo, amesema mwezi wa Ramadhani una umuhimu mkubwa kwa Waislamu na jamii, ni kipindi kinachokumbusha kujenga maadili mema katika maisha ya binadamu ya kila siku.
Waziri huyo amefafanua kuwa Ramadhani ni mwezi uliojaa subira, unawakumbusha pia Watanzania kujenga uhusiano mwema sambamba na kusaidiana kwa watu wote wakiwemo wanaoishi katika mazingira magumu.
Kuhusu bima, amesema ni muhimu katika maendeleo ya nchi na zina nafasi katika mwendelezo wa uchumi wa Taifa.
“Bima ni muhimu inatusaidia kulinda mali, biashara na maisha ya wananchi kwa ujumla dhidi ya hatari mbalimbali. Katika mazingira ya kisasa ya uwekezaji na biashara hakuna uchumi unaoweza kukua pasipo kuwepo kwa bima imara.”
“Wawekezaji wanahitaji mazingira salama ya biashara, lakini pia Serikali inahitaji taasisi imara zitakazoweza kusimamia hatari na kuhakikisha ustawi wa uchumi wa nchi. Nitumie fursa hii kuipongeza ZIC kwa kuwa mstari wa mbele kulinda mali za wananchi, biashara na miradi,” amesema Ridhiwani.
Kaimu Mkurugenzi wa ZIC, Sabri Omar Ali amesema mwezi wa Ramadhani unasaidia kuimarisha maadili ya taasisi na jamii kwa ujumla.
“Tunapofunga tunajifunza kutawala na kuwa na nidhamu katika maisha yetu. Tunajifunza kuthamini neema tulizopewa na Mungu, lakini pia kuwajaili wengine wasiojiweza,” amesema Ali.
Ali amesema katika ulimwengu wa biashara na taasisi, maadili yana nafasi kubwa kwa sababu ndio msingi wa uaminifu unaojenga uhusiano imara kati ya taasisi na wateja wake.
“Katika sekta ya bima uaminifu ndio jambo la msingi sana, wateja wanakata bima wanaweka matumaini kwetu kwamba pale wanapopata changamoto tunasimama nao. Mwezi huu unatukumbusha uaminifu na kuwajibika katika taasisi zetu,” amesema.
Ali amesema bima ni nguzo muhimu katika inayosaidia kulinda mali za watu, biashara na uwekezaji, lakini bila uwepo wa mfumo imara shughuli za kiuchumi zisingeweza kufanyika kwa ujasiri kwa sababu wafanyabiashara wanahitaji uhakika wa mitaji.