Arusha. Zaidi ya wajumbe 700 kutoka nchi nane wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wanatarajiwa kuwasili Arusha Jumamosi hii kwa ajili ya mkutano wa 25 wa kawaida wa wakuu wa nchi, unaopangwa kufanyika Machi 7, 2026 katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC).
Katika mkutano huo muhimu, viongozi wa EAC ambao wana dhamana ya kufanya uamuzi muhimu kwa jumuiya, watajadili masuala makuu ya kanda, ikiwa ni pamoja na maendeleo katika utekelezaji wa programu za kikanda, ripoti za taasisi na mipango mikakati inayolenga kuzidisha ujumuisho na kuboresha maisha ya wananchi wa Afrika Mashariki.
Miongoni mwa ajenda kuu ya mkutano huu ni uchaguzi wa mwenyekiti mpya wa EAC, ambaye atashika wadhifa kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Marais watakaopiga kura ni pamoja na Mwenyekiti wa sasa, Rais William Ruto wa Kenya, pamoja na marais Dk Samia Suluhu Hassan wa Tanzania, Yoweri Museveni wa Uganda, Paul Kagame wa Rwanda, Evariste Ndayishimiye wa Burundi, Salva Kiir Mayardit wa Sudan Kusini, Félix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, Katibu Mkuu wa EAC, Veronica Nduva amesema nafasi ya uenyekiti inategemea makubaliano kati ya viongozi hao wanane.
“Wadhifa huu unazunguka miongoni mwa nchi wanachama kuhakikisha usawa, hivyo yoyote kutoka nchi wanachama anaweza kuchaguliwa,” amesema.
Tangu mwaka 2012, uwenyekiti wa EAC umezungushwa miongoni mwa nchi wanachama.
Rais Yoweri Museveni wa Uganda ameiongoza EAC kutoka 2012 hadi 2013 na tena kati ya mwaka 2017 hadi 2019, pia, kati ya mwaka 2013 hadi mwaka 2015, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alishika wadhifa huo, akifuatiwa na Rais John Magufuli wa Tanzania kutoka mwaka 2015 hadi 2017.
Kutoka mwaka 2019 hadi 2021, uwenyekiti ulikwenda kwa Rais Paul Kagame wa Rwanda na Rais Kenyatta alirudi tena kati ya mwaka 2021 hadi 2022.
Rais Évariste Ndayishimiye wa Burundi alishika wadhifa kutoka mwaka 2022 hadi 2023, akifuatiwa na Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini kutoka mwaka 2023 hadi 2024.
Rais Ruto akiwakilisha Kenya, kwa mara ya tatu, akashika nafasi hiyo tena mwaka 2024 ambapo ndio anatarajiwa kukamilisha kipindi chake mwaka huu.
Nchi ambazo hadi sasa zinatajwa kushika uwenyekiti ni Tanzania, iliyoongoza mara moja mwaka 2017, pamoja na Somalia na DRC ambazo ni wanachama wapya na bado hazijawahi kushika wadhifa huo.
Wataalamu wa maswala ya kisiasa wanaitaja Tanzania, inayoongozwa na Rais Samia, kama kinara wa kete hiyo kutokana na kuwa moja ya nchi tatu waanzilishi, hivyo kuwa na uzoefu, pia, ni mlipaji mzuri wa michango kwa jumuiya na zaidi ameshika nafasi hiyo mara moja tofauti na nchi zingine.
Mwandishi mwandamizi wa masuala ya kisiasa, Marc Nkwame amesema: “Tanzania, Somalia na DRC zote zina nafasi, ingawa sifa zao zinatofautiana.”
“DRC na Somalia ni wanachama wapya wenye uzoefu mdogo wa uongozi wa EAC na mabadiliko ya sera za michango yanaweza kuongeza ugumu kwao kwani ni nchi ambazo hazijakuwa mstari wa mbele katika michango, hali inayowaweka Tanzania katika nafasi nzuri.”
Mchambuzi mwingine wa masuala ya kisiasa, Abel Mtupwa, amesema: “Tangu kuanzishwa kwa EAC, uenyekiti umezungushwa kati ya Uganda (2012), Kenya (2015) na Tanzania (2017).”
“Nchi hizo zimewahi kushika uwenyekiti mara kadhaa isipokuwa Tanzania, miaka tisa imepita tangu Tanzania kushika nafasi hii, hivyo ni wakati mwafaka wa kurudi.”
Mkutano huo, wenye kaulimbiu: “Kuzidisha Ujumuisho kwa Maendeleo Bora ya Maisha ya Raia wa EAC”, pia, utahudhuriwa na makatibu wakuu na mabalozi wa nchi wanachama.
Miongoni mwa majukumu yatakayotekelezwa ni uzinduzi wa Dhamana ya Forodha ya EAC, itakayobadilisha haja ya dhamana nyingi za kitaifa na kuweka mfumo mmoja wa kikanda.
Nduva amesema mfumo huu mpya utawezesha wafanyabiashara na wakaguzi wa bidhaa kutumia dhamana moja inayotambulika katika nchi zote za EAC, kupunguza gharama, kucheleweshwa mipakani, kulinda mapato ya serikali, na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa haraka na salama ndani ya jumuiya.
Wajumbe wa mkutano, pia, watazindua rasmi Mkakati wa Saba wa Maendeleo ya EAC (2026/27–2030/31), unaoeleza mwelekeo wa miaka mitano wa kuharakisha ujumuisho wa kikanda na mabadiliko ya kijamii na kiuchumi.
“Mkakati huu unajengwa juu ya mafanikio na masomo yaliyopatikana katika kipindi cha maendeleo kilichopita, na unalingana na Maono ya EAC 2050, Ajenda ya Umoja wa Afrika 2063, na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs),” amesema Nduva.
Ajenda zingine ni pamoja na kupitia ripoti ya baraza kwa kipindi cha Novemba 30, 2024 hadi Desemba 31, 2025, utekelezaji wa maelekezo ya Mkutano wa 24 wa Wakuu wa Nchi juu ya ufadhili endelevu wa bajeti ya EAC.
Pia, wakuu wa nchi watafanya uteuzi wa Katibu Mkuu mpya wa EAC, wateuzi wa majaji wa Mahakama ya Afrika Mashariki, uteuzi wa Naibu Katibu Wakuu, uteuzi wa Wakuu wa Tume ya Ushindani ya EAC, na idhini ya sheria zilizopitishwa na Bunge la Afrika Mashariki.
“Matokeo ya mkutano yanatarajiwa kuimarisha usawa wa sera miongoni mwa nchi wanachama na kuharakisha utekelezaji wa programu muhimu za kikanda zinazolenga ukuaji jumuishi na ujumuisho wa kiuchumi,” amesema Nduva.
Mkutano huo umetanguliwa na mkutano wa Baraza la Mawaziri wa EAC unaoendelea katika makao makuu ya EAC jijini Arusha unaopitia ajenda zote kabla ya kuzikabidhi kwa wakuu wa nchi kupitia na kupitishwa.