Dar es Salaam. Askari Polisi mwenye namba G 2325, Sajenti Joseph (41) ameieleza Mahakama jinsi mshtakiwa, Respicius Magesa (54) na mwenzake Andrew Kamugisha (47) walivyokiri kutenda kosa la kughushi na kuhamisha Sh159 milioni, kutoka akaunti binafsi kwenda katika akaunti ya Sekondari ya Macmillian.
Joseph, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Alhamisi Machi 5, 2026, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa usikilizwaji.
Kamugisha, ambaye ni mkazi wa Mbezi na Magesa, mkazi wa Kinondoni Manyanya kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka manne, yakiwemo kuongoza genge la uhalifu, kughushi, kuwasilisha taarifa za uongo na kujitambulisha.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Monica Ndekidemi, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya shahidi huyo ambaye ni mpelelezi, alidai Septemba 9, 2023, akiwa Ofisi ya Mkuu wa Kipolisi Temeke akiendelea na majukumu yake, aliitwa na Mkuu wa Upelelezi Mkoa na kumkabidhi watuhumiwa wawili.
Shahidi huyo alidai alikabidhiwa watuhumiwa hao na jalada la kesi ambalo lilifunguliwa Kituo cha Polisi Kibada, Kigamboni Dar es Salaam.
“Baada ya kukabidhiwa watuhumiwa hao niliwaweka chini ya ulinzi na kuanza kuwahoji kuhusu tuhuma zilizokuwa katika jalada ambalo lilitokea Kibada na katika mahojiano ya awali walikiri,” amedai.
Shahidi huyo amedai baada ya washitakiwa kukiri aliendelea kumhoji mshitakiwa Andrew Kamugisha huku mwingine alihojiwa na Sajenti Hassan.
Joseph, amedai alipomuhoji Kamugisha alimweleza walipotaka kufanya tukio la wizi wa kuhamisha fedha katika benki ya CRDB tawi la Kibada waliishia kujaza fomu za kutolea fedha.
”Walitaka kufanya matukio ya kuhamisha fedha kutoka katika akaunti Khepha Miti kwenda akaunti ya Shule ya Sekondari ya Macmillan kwa ajili ya kujinufaisha wenyewe na Kamugisha ndiye mmiliki, ambapo waliishia hatua za kujaza fomu za kutolea.
Shahidi huyo aliendelea kudai kuwa Septemba 12, 2023, alikwenda eneo la tukio CRDB Kibada kupata ushahidi na vielelezo ambavyo ni fomu walizokuwa wamejaza.
”Nilionana na Meneja wa benki hiyo Isaya Lyimo aliyewahudumiwa washitakiwa hao kwa lengo la kutoa fedha katika akaunti,” amedai
Amedai Meneja alimkabidhi fomu hizo na kisha aliondoka hadi Kituo cha Polisi Temeke ambapo aliwaonyesha washitakiwa na walizitambua.
Ameendelea kudai kuwa katika upelelezi wake alibaini kwamba aliyejaza fomu hiyo alikuwa ni Magesa, ambapo maandishi yalipelekwa kufanyiwa uchunguzi kwa mtaalamu wa maandishi.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 17, 2026 na washtakiwa wako nje kwa dhamana.
Katika shtaka la kuongoza genge ka uhalifu, wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Agosti Mosi na Septemba 9, 2023, katika benki ya CRDB tawi Kibada Kigamboni Dar es Salaam, ambapo kwa nia ovu waliongozwa mtandao wa uhalifu kwa kufanya vitendo vya udanganyifu na kujipatia Sh159, 525,000 kutoka benki ya CRDB.
Shtaka la tatu ni kughushi ambapo washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa Septemba 9,2023 katika benki ya CRDB tawi la Kibada, Kigamboni kwa nia ovu aliweza kuandaa taarifa za uongo (Deposit Withdraw Slip-Cash Only) ya tarehe hiyo wakiwa na lengo la kuonesha Mwiti alitaka kutoa dola za Marekani 19,200 sawa na Sh159 milioni kwenye akaunti yake binafsi tawi la Mikocheni ili ziingizwe kwenye akaunti namba 0150460392500 yenye jina la shule ya Sekondari Macmillan iliyopo tawi la Quality Center huku wakitambua kuwa ni uongo.
Inadaiwa fedha hizo zilitakiwa kuingizwa katika akaunti yenye jina la shule hiyo ambayo mmiliki wake ni mshitakiwa Kamugisha.
Pia wanadaiwa kuwasilisha nyaraka hizo, ambapo inadaiwa siku hiyo wakiwa tawi la CRDB Kibada, Kigamboni waliwasilisha nyaraka kwa ofisa wa benki Stephen Mponeja, wakionyesha kuwa Mwiti anataka kutoa fedha hizo wakati wakijua kuwa sio kweli.