Dar es Salaam. Wafanyabiashara wa Soko la Kawe wameanza kupata matumaini mapya baada ya Serikali kutangaza kukamilika kwa ujenzi wa soko jipya la muda kufuatia soko la awali kuteketea kwa moto.
Hatua hiyo inatarajiwa kuwapa nafuu wafanyabiashara waliopoteza maeneo yao ya biashara kwa tukio la moto kwa sasa kuwaruhusu kuingia eneo lililoboreshwa kuendelea na shughuli zao za kiuchumi.
Mbali na hilo, wanafunzi wa shule za msingi wilaya ya Kinondoni wanatarajiwa kuondokana na changamoto ya upungufu wa madarasa, kufuatia ujenzi unaoendelea wa vyumba vipya vya madarasa katika kata mbalimbali zenye shule za msingi.
Ujenzi huo unalenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani, hali inayotarajiwa kuongeza ufanisi katika utoaji wa elimu ya msingi.
Kauli ya kukamilika kwa soko hilo ilitolewa mbele ya Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kinondoni na Mhandisi wa Manispaa ya Kinondoni, Charles Masedoya, alipokuwa akitoa taarifa kuhusu mwenendo wa ujenzi wa miundombinu mbalimbali katika wilaya hiyo.
Ikumbukwe kwamba mwaka jana, usiku wa kuamkia Septemba 15, 2025, moto ulizuka katika Soko la Kawe na kuteketeza sehemu kubwa ya soko hilo, na kusababisha hasara kwa wafanyabiashara, huku chanzo cha moto huo kikiwa hakijafahamika.
Masedoya amesema baada ya soko la Kawe kuungua walianza ujenzi wa mabanda sita ya kisasa yenye vizimba 60 na matundu 13 ya vyoo.
“Soko hili ni la muda na limegharimu Sh700 milioni. Tayari mradi umekamilika, kilichobaki ni kumalizia fremu za chini. Kupitia mradi huu, watu 121 walipata ajira,” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule amesema baada ya soko la Kawe kuungua Manispaa hiyo ilitafuta eneo kwa haraka ili kuwajengea wafanyabiashara hao soko la muda.
“Wananchi wana shauku kubwa ya kuingia katika soko hili. Kwa sasa wanafanya biashara pembezoni mwa barabara, lakini miundombinu ya soko tayari imekamilika,” amesema.
Kuhusu soko hilo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kinondoni, Shaweji Mkumbula amesifu hatua ya Serikali kujenga soko hilo kwa haraka ili kuwaondolea changamoto wafanyabiashara, akisema hata ujenzi wa soko kubwa ukikamilika soko hilo liendelee kutumika.
“Pamoja na kwamba soko hili ni la muda, tuendelee kulitumia hata soko lingine likijengwa. Tuhakikishe walengwa pekee ndio wananufaika ili tuepushe malalamiko ya watu wasiohusika kuingia katika soko hili,” amesema.
Naye Katibu wa CCM Wilaya ya Kinondoni, Jacob Siay ameshauri kabla ya soko hilo kuanza kufanya kazi kuwe na utaratibu wa kuruhusu magari kuingia ndani ili kulichangamsha.
“Niitake Serikali kuhakikisha ndani ya soko hili linawekwa stendi ili soko lichangamke na wanufaika wawe ni wale walioathirika na janga la moto,” amesema.
Ili kuleta utulivu kwa wafanyabiashara, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Songoro Mnyonge, amesema katika soko hilo wanatarajia kujenga fremu nyingine 60 pamoja na machinjio.
“Sasa tuwaombe wenzetu wa Shirika la Taifa la Nyumba (NHC), kwa kuwa eneo hili ni lao, waliridhie liwe chini ya Manispaa ya Kinondoni. Pia nimuombe Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, aridhie eneo hili liwe chini ya Manispaa ya Kinondoni,” amesema.
Kwa upande wake, mfanyabiashara katika Soko la Kawe, Shaban Sebastian, amesema kukamilika kwa soko jipya la muda kunatoa matumaini mapya kwa wafanyabiashara waliopoteza maeneo yao ya biashara baada ya soko la awali kuungua kwa moto.
Amesema kwa kipindi kilichopita walikabiliwa na changamoto kubwa ya kuendesha biashara katika mazingira yasiyo rasmi, hali iliyosababisha baadhi yao kupata hasara na kupoteza wateja.
“Kukamilika kwa soko kutatusaidia kurejea katika mazingira bora ya kufanyia biashara na kuendelea kujipatia kipato kwa utulivu zaidi,” amesema.