Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Mkoa wa Dodoma unashiriki katika Kliniki maalum ya kutatua kero na changamoto mbalimbali za wananchi iliyoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, inayofanyika tarehe 3 hadi 6 Machi, 2026 katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma.
Kupitia kliniki hiyo, TBA inakutana na wateja wake ambao ni wapangaji wa nyumba zake kwa lengo la kusikiliza na kutatua changamoto pamoja na kero mbalimbali zinazojitokeza katika maeneo wanayoishi.
Aidha, kliniki hiyo imekuwa fursa kwa taasisi mbalimbali za Serikali kutoa elimu kwa wananchi pamoja na kueleza mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa majukumu yao ndani ya siku 100 za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tangu kuingia madarakani.
Katika kliniki hiyo, TBA kama zilivyo taasisi nyingine za Serikali imeweka banda maalum kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu yake pamoja na kueleza miradi mbalimbali iliyotekelezwa na wakala huo katika kipindi hicho.
Akitembelea mabanda ya taasisi mbalimbali katika viwanja hivyo leo Machi 5, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, ameipongeza TBA kwa kutekeleza miradi mikubwa ya Serikali katika mkoa wa Dodoma, ikiwemo ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba pamoja na mradi wa ujenzi wa nyumba 3,500 za makazi ya watumishi wa umma katika eneo la Nzuguni.
Kwa upande wao, wananchi waliotembelea banda la TBA wamepongeza utekelezaji wa mradi wa nyumba za makazi katika eneo la Nzuguni, wakisema umechangia kusogeza huduma za kijamii na biashara karibu na wananchi pamoja na kuimarisha hali ya ulinzi na usalama katika eneo hilo.