Unguja. Licha ya Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (EA) kuzalisha tafiti nyingi, vipaji na miliki bunifu, imeelezwa ni uvumbuzi mchache unaofanikiwa kuingia sokoni kama biashara endelevu na zenye uwezo wa kukua.
Ili kubadilisha hali hiyo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP Tanzania) na Chuo cha Indian Institute of Technology Madras Zanzibar (IIT Madras Zanzibar), wamewakutanisha viongozi wa vyuo vikuu, watunga sera na wadau wa mifumo ya ubunifu kutoka Afrika Mashariki katika mpango wa kubadilishana utaalamu.
Lengo la mpango huo ni kuvigeuza vyuo vikuu kuwa injini za kuanzisha biashara bunifu changa na kukuza ujasiriamali.
Akizungumza wakati wa jukwaa hilo leo Machi 5, 2026 Katibu Mkuu, Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu, Fatma Mabrouk Khamis amesema mpango huo unalenga kuziba pengo hilo la kimfumo kwa kuimarisha mifumo ya taasisi, vivutio na ushirikiano unaowezesha uanzishaji wa biashara ndani ya taasisi za elimu ya juu.
“Tunapofungua programu hii, ningependa kusisitiza kuhusu hatua kadhaa za kuchukua, kwanza ushirikiano uzalishe matokeo halisi ikiwemo tafiti za pamoja, programu za kubadilishana wahadhiri na miradi shirikishi ya ubunifu,” amesema.
Naye Mkuu wa Ofisi Ndogo ya UNDP Zanzibar, Godfrey Nyamrunda, amesisitiza umuhimu wa kimkakati wa mpango huu katika vipaumbele vya maendeleo ya Taifa.
“Hapa UNDP, tunaona vyuo vikuu kama kiunganishi muhimu ndani ya mfumo wa ubunifu wa Tanzania.
“Kupitia mipango kama funguo, tunawekeza katika mifumo, ushirikiano na nyenzo za kifedha zinazowezesha wabunifu vijana kupiga hatua kutoka wazo mpaka kuwa biashara,” amesema.
Mshauri wa Utafiti na Ubunifu katika Kituo cha Utafiti na Ubunifu Afrika Mashariki kutoka ofisi ya ubalozi wa Uingereza jijini Nairobi, Kenya, Dk Jacqueline Owigo, ameeleza umuhimu wa kujenga mifumo imara ya ubunifu kupitia ushirikiano wa kimataifa.
“Kote katika ukanda huu, tumejifunza kuwa mifumo hai ya biashara bunifu haijitokezi kwa bahati mbaya; hujengwa kwa makusudi.
“Vyuo vikuu vina nafasi ya msingi katika kulea vipaji vya ujasiriamali, kuimarisha njia za kukuza tafiti mpaka kuwa katika uendelezaji wa kibiashara, na kuwaunganisha wabunifu na sekta binafsi pamoja na wawekezaji,” amesema.
Kaimu Mkurugenzi, Chuo cha IIT Madras, Kampasi ya Zanzibar, Profesa Prabhu Rajagopal, amesema vyuo vikuu vinapaswa kubadilika kutoka kuwa wazalishaji wa maarifa hadi kuwa waanzilishi wa biashara hai bunifu.
“Kwa kutumia motisha, kuimarisha mifumo ya uhamishaji wa teknolojia, na kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi, tunaweza kujenga njia endelevu kutoka utafiti mpaka biashara; tunatarajia kuona mbeleni wahitimu wanakuwa waajiri, na sio watafuta ajira pekee,” amesema Profesa Rajagopal.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake mwanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salam, Happy Weston, amesema mradi huo una manufaa makubwa kwao kwani utawawezesha pale watakapomaliza chuo kujiajiri wenyewe na kusaidia jamii.
Mpango huu unaviweka vyuo vikuu kama nguzo muhimu za ubunifu, uendelezaji wa teknolojia na ukuaji wa biashara.
Utekelezaji wake unafanyika kupitia Mradi wa Ubunifu wa Funguo, ambao ni wa kimkakati unaofadhiliwa kwa pamoja na Serikali ya Uingereza (FCDO), na kutekelezwa na UNDP Tanzania.