Unguja. Katika wiki ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, mradi wa pamoja wa kukuza usawa wa kijinsia umezinduliwa ukilenga kuwanufaisha zaidi ya wanawake na watoto 41,000 nchini.
Mradi huo wa miaka mitano, unaofadhiliwa na Benki ya Dunia (WB), unalenga kutoa mikopo yenye masharti nafuu pamoja na kupambana na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia. Mbali na wanawake na watoto, watoa huduma wanaopambana na udhalilishaji na jamii kwa ujumla pia watanufaika.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo Machi 4, 2025, Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Balozi Zena Said amesema walengwa watapatiwa elimu na mafunzo ya uendeshaji wa biashara kabla ya kupokea mikopo.
“Mradi huu utaakisi dhana ya kuhakikisha haki na usawa wa mwanamke unafikiwa kwa mustakabali wa jamii kwa ujumla,” amesema Balozi Zena.
Amesema utekelezaji wa mradi huo pia utahusisha kusimamia na kufuatilia juhudi za kupambana na udhalilishaji, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Kitaifa wa kupambana na udhalilishaji wa wanawake na watoto wa awamu ya pili.
Balozi Zena amesema Serikali inatambua kuwa ukatili na udhalilishaji vinakwamisha maendeleo ya nchi, na tayari imeanza kuandaa bajeti inayozingatia usawa wa kijinsia.
Wadau mbalimbali wakishiriki uzinduzi wa mradi wa kukuza usawa wa kijinsia wa Pamoja Chuo cha Polisi Zanzibar.
“Nguvu itaongezwa katika kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji hasa kwa kina mama na watoto kwa kuimarisha miundombinu ya huduma kwa waathirika,” amesema.
Ameongeza kuwa mradi huo pia utatoa huduma za ushauri na msaada wa kisaikolojia kwa waathirika wa udhalilishaji ili kukabiliana na changamoto za msongo wa mawazo na afya ya akili. Huduma hizo zitatolewa kupitia kituo kitakachojengwa mahsusi kwa ajili ya ushauri na tiba ya kisaikolojia.
Aidha, vituo vya malezi ya kutwa vitajengwa na baadhi ya majengo kukarabatiwa ili kuwawezesha akina mama kushiriki katika shughuli za kiuchumi huku watoto wakilelewa katika mazingira salama.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa WB, Tanya Dilima amesema mradi huo ulitokana na tathmini ya jinsia na uchambuzi wa Pato la Taifa uliofanyika mwaka 2022.
Amesema licha ya wanawake kuwa na mchango mkubwa katika shughuli za kiuchumi, bado wanakabiliwa na changamoto ikiwemo upatikanaji mdogo wa fedha, majukumu ya malezi yasiyolipwa na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia.
Mmoja wa wanufaika wa mradi huo, Bahati Khamis Juma amesema mpango huo utawasaidia wanawake kuimarisha uchumi wao na kupata elimu ya kujilinda dhidi ya udhalilishaji.