Watanzania kunufaika mikopo ya nyumba bila dhamana

Dar es Salaam. Watanzania wenye kipato cha chini ambao awali walishindwa kupata mikopo ya nyumba kutokana na masharti magumu yaliyowekwa na taasisi za kifedha, sasa wanaweza kunufaika na suluhisho jipya la kifedha lililozinduliwa rasmi.

Fursa hii imekuja kufuatia uzinduzi rasmi wa mpango wa Wholesale Housing Microfinance chini ya Kampuni ya Mikopo ya Nyumba Tanzania (TMRC) kwa kushirikiana na Habitat for Humanity International.

Mpango huu umetengenezwa mahsusi kusaidia watu waliokuwa wakishindwa kupata mikopo ya nyumba kwa sababu walikosa hati miliki au dhamana rasmi zinazohitajika na benki.

Kupitia mpango huu mpya, TMRC itatoa Sh30 bilioni kwa taasisi za fedha ambazo sasa zitaondoa ulazima wa mkopaji kuwa na hati miliki ya ardhi pekee ili aweze kupata mkopo, badala yake zitapima uwezo wa mkopaji kwa kuzingatia kipato chake na aina nyingine za dhamana zinazokubalika.

Takwimu zinaonyesha ni takriban asilimia tatu pekee ya Watanzania wanaostahili kupata mikopo ya nyumba huku wadau wakisema njia hii mpya inatarajiwa kupanua kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa mikopo ya nyumba, hasa kwa wananchi wanaofanya kazi katika sekta isiyo rasmi ambao mara nyingi hawana nyaraka rasmi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Naibu Waziri wa Fedha, Mshamu Munde amesema upatikanaji wa makazi bora na salama ni haki ya msingi ya binadamu na nguzo muhimu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

 “Kwa upande wa Wizara ya Fedha, tunaunga mkono juhudi hizi kwa vitendo. Tumeidhinisha mapendekezo ya timu ya wataalamu ya kuhamisha sehemu ya Mradi wa Fedha za Makazi (HFP) ambao hapo awali ulikuwa unasimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), hasa Mfuko wa Mikopo Midogo ya Makazi kupelekwa TMRC ili mfuko huo uendelee kukua na kuwawezesha Watanzania wengi zaidi wenye kipato cha chini kupata makazi salama na bora,” amesema.

Ameongeza wizara imetambua changamoto zilizotajwa na wadau na ipo tayari kushirikiana na washirika wote katika sekta ya mikopo midogo ya makazi kuhakikisha mpango huo unatekelezwa ipasavyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa TMRC, Elibariki Ndossi amesema programu hiyo itawawezesha wananchi wenye kipato cha chini kumiliki nyumba au kukamilisha nyumba ambazo bado hazijakamilika. Alifafanua kuwa TMRC tayari imesaini mikataba na taasisi mbili za fedha na inatarajia nyingine zaidi kujiunga.

Ameeleza pia kuwa kabla ya uzinduzi huu, utafiti ulifanyika na kuthibitisha kuwa kuna mahitaji makubwa ya makazi miongoni mwa wananchi wenye kipato cha chini.

Wakati wa awamu ya majaribio na taasisi hizo mbili, zaidi ya Sh1 bilioni zilitolewa kwa wananchi kwa ajili ya ujenzi wa nyumba.

“Kuna mahitaji makubwa sana ya makazi. Tutatoa mikopo kwa riba nafuu na wakopaji hawatalazimika kuwa na hati miliki ya ardhi sharti ambalo hapo awali lilikuwa kikwazo kikubwa kwao kupata mikopo ya benki na tutazingatia zaidi kipato cha mkopaji,” amesema.

Kwa upande mwingine, Daniel Mhina ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi wa Masuala ya Fedha za Makazi wa Habitat for Humanity International Afrika amesema zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania hujenga nyumba zao hatua kwa hatua na wengine huchukua hadi miaka 18 kukamilisha ujenzi.

Amesema kuwa bidhaa hii mpya itasaidia familia kumaliza ujenzi wa nyumba zao na kumiliki makazi yao kwa muda mfupi zaidi.

Ameongeza kuwa uzinduzi huu si tu utambulisho wa bidhaa ya kifedha, bali ni majibu kwa uhitaji wa muda mrefu wa familia nyingi, hasa zile zenye kipato kisicho thabiti au zinazofanya kazi katika sekta isiyo rasmi.