Yanga yatakata Singida, Okelo afungua akaunti ya mabao Ligi Kuu

BINGWA mtetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga imeendeleza rekodi bora ya kutopoteza, baada ya kikosi hicho kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Singida Black Stars, katika mechi kali iliyopigwa leo Machi 5, 2026 kwenye Uwanja wa Airtel, mjini Singida.

Katika mechi hiyo, Prince Dube alifungua ukurasa wa mabao dakika ya 39, baada ya kupokea pasi nzuri ya Maxi Nzengeli, huku kiungo mshambuliaji, Mganda, Allan Okello akifunga la pili kwa mkwaju wa penalti dakika ya 45.

Okello aliyejiunga na kikosi hicho katika dirisha dogo la Januari 2026, akitokea Vipers ya kwao Uganda, alifunga bao hilo baada ya Dube kufanyiwa madhambi akiwa eneo la hatari na Mnigeria, Morice Chukwu.

Hata hivyo, licha ya Singida kucheza soka la kuvutia na kutengeneza mashambulizi ya mara kwa mara, lakini Yanga ilipata bao la tatu kupitia kwa kiungo, Mudathir Yahya dakika ya 54, akiunganisha mpira uliotemwa na kipa wa Singida, Metacha Mnata.

Ushindi huo kwa Yanga umeifanya timu hiyo kufikisha mechi 32 za Ligi Kuu Bara bila ya kupoteza, tangu mara ya mwisho kwa kikosi hicho kilipochapwa mabao 3-1 dhidi ya TRA United, zamani Tabora United, pambano lililopigwa, Novemba 7, 2024.

Katika mechi hiyo iliyopigwa Novemba 7, 2024, kwenye Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam, ilikuwa ni ya mwisho kwa kikosi hicho kupoteza ambapo kwa sasa imefikisha 32, huku kati ya hizo ikishinda 29 na kutoa sare tatu.


Kwenye mechi hizo 32 ilizocheza Yanga bila ya kupoteza tangu Novemba 7, 2024, kikosi hicho kimeshinda 29 na kutoka sare tatu, huku ikifunga mabao 99, wakati eneo la kujilinda limeruhusu nyavu zake kutikiswa mara nane.

Kabla ya mechi hiyo, Singida na Yanga zilikutana kwa mara ya kwanza katika uzinduzi wa Uwanja wa Airtel, Machi 24, 2025, ikiwa ni pambano la kirafiki lililoisha sare ya bao 1-1, huku ikishuhudiwa likichezwa dakika 57, baada ya kunyesha mvua kubwa.

Pia, Yanga imeendeleza rekodi bora dhidi ya Singida, kwani kabla ya mechi hiyo, mara ya mwisho zilipokutana katika Ligi Kuu, ilichapwa mabao 2-1,

Februari 17, 2025, yaliyofungwa na Clement Mzize dakika ya 14 na Prince Dube dakika ya 43.

Katika mechi hiyo, aliyekuwa mshambuliaji wa Singida, Jonathan Sowah, anayeichezea Simba msimu huu, ndiye mchezaji wa mwisho wa kikosi hicho kuifunga Yanga bao kwenye kichapo hicho cha Februari 17, 2025, ikiwa ni msimu uliopita wa 2024-2025. 

Ushindi huo kwa Yanga umeifanya kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu, baada ya kufikisha pointi 32, katika mechi 12 ilizocheza hadi sasa msimu huu ambazo ni sawa za kikosi cha Singida kinachoshika nafasi ya tisa na pointi zake 19.