AG awataka watumishi wa umma kulinda taswira ya Serikali

Dar es Salaam. Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, amewataka watumishi wa umma kuepuka vitendo vinavyoathiri taswira ya Serikali na utumishi wa umma.

Amewataka watumishi hao kuhakikisha wanawajibika ipasavyo kama kanuni na taratibu za utumishi wa umma zinavyowaelekeza.

Johari ametoa wito huo leo Machi 6, 2026, wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD), jijini Dar es Salaam.

“Nitoe wito kwa watumishi wa umma kuhakikisha wanazingatia Katiba, sheria, kanuni, na miongozo mbalimbali ili Tanzania iendelee kuenzi amani, demokrasia, umoja, upendo, na mshikamano wa taifa, na kuendelea kuwa wazalendo,” amesema.

Kupitia maagizo yake, Johari ameitaka Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria kuboresha mifumo ya Tehama ili kuendana na kasi ya dunia katika ukuaji wa teknolojia.

Mbali na hayo, amesisitiza watumishi kuendelea kupatiwa mafunzo ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya dunia.

Ameipongeza taasisi hiyo kwa kuendelea kutekeleza majukumu yake na kuleta tija kwa Serikali.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Hamza Johari (wapili kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na Mwandishi Mkuu wa Sheria, Onorius Njole wa kwanza kushoto. Watatu kushoto ni Mkurugenzi wa Mashtaka DPP Sylvester Mwakitalu. Wengine kwenye picha ni watumishi wa Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria



Ameitaka Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria kuendelea kuboresha hali ya rasilimali watu katika maeneo yanayoonekana kuwa na uhitaji wa watumishi.

“Serikali imefanya ugatuaji wa madaraka kwa kuwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali,” amesema, akiongeza kuwa hilo ni jambo muhimu lenye tija.

Johari amesema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria kuhakikisha inapata bajeti inayotosheleza kutekeleza majukumu yake na kuleta tija kwa taifa kupitia uandishi wa sheria.

“Tunajua mambo ya bajeti yana changamoto zake, lakini dhamira ikiwa kubwa tutaitekeleza na kufanikisha,” amesema.

Naye Mwandishi Mkuu wa Sheria, Onorius Njole, amesema ofisi yake ina jukumu la msingi la kubadili sera kuwa sheria ambazo zinasaidia upatikanaji wa haki, usawa, na maendeleo.

“Huduma zetu zinalenga kutoa sheria bora, zinazopatikana kwa urahisi na kwa usahihi, kwa ajili ya kujenga msingi imara kwa maendeleo endelevu. Tunashirikiana kwa karibu na Bunge, Mahakama, taasisi za Serikali, na wadau wengine kuhakikisha sheria zinapatikana kwa lugha rahisi ili kukidhi dhamira yetu ya upatikanaji wa sheria bora kwa kila mtu,” amesema.

Amesema Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria imepewa uzito mkubwa na Serikali kutokana na kwamba sheria ni maisha ya watu.

“Mtu akitaka kukuharibia maisha yako, anatunga sheria ambayo ikitekelezwa maisha yako yanabadilika moja kwa moja. Unafanya biashara yoyote, mtu akiamua kukutoa kwenye mstari anasimamia sheria; ndiyo maana eneo la uandishi wa sheria Serikali imelishikilia kwa nguvu zote,” amesema.

Amesema majukumu ya uandishi wa sheria yalikuwepo nchini hata kabla ya Tanganyika kupata uhuru, na shabaha kuu ilikuwa kuhakikisha jamii haiathiriki kutokana na uwepo wa sheria.

Njole amesema ofisi hiyo imedhamiria kukuza ushirikiano utakaochangia uthabiti wa kiuchumi, ukuaji wa maendeleo, haki za binadamu, pamoja na kujenga msingi endelevu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania (DPP), Sylvester Mwakitalu, amesema baraza la wafanyakazi ni jukwaa muhimu linalounganisha watumishi na menejimenti na hutoa mwanya wa mambo mengi kujadiliwa.

Amesema baraza la wafanyakazi ni mahali ambapo masuala mengi yanayohusu utumishi yanajadiliwa, akidokeza kuwa vikao hivyo huleta tija kwa taasisi.