Aliyekataa bao, aliyefunga wafungiwa | Mwanaspoti

BODI ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), imetoa adhabu kwa klabu, wachezaji na waamuzi kufuatia matukio yaliyojitokeza katika michezo mbalimbali  ikiwemo Dabi ya Kariakoo iliyopigwa wikiendi iliyopita, Zanzibar.

Katika uamuzi huo uliotangazwa Machi 6, 2026, Simba imeadhibiwa kwa makosa yaliyotokea katika michezo tofauti ya Ligi Kuu Bara.

Katika mchezo dhidi ya Dodoma Jiji, Simba imetozwa faini ya Sh5 milioni baada ya mashabiki wake kuwarushia chupa za maji mchezaji wa Dodoma Jiji na wahudumu wa huduma ya kwanza wakati wakitekeleza majukumu uwanjani.

Pia, katika dabi dhidi ya Yanga iliyochezwa kwenye Uwanja wa New Amaan, Simba imepigwa faini ya Sh5 milioni kwa kuingia uwanjani kupitia mlango usio rasmi.

Pia, timu hiyo imetozwa Sh5 milioni kwa kukataa kutumia chumba rasmi cha kubadilishia nguo na badala yake kutumia kile cha mikutano ya waandishi wa habari kabla ya kuanza kwa mchezo.

Mbali na hilo, makomandoo wa Simba walihusika kwenye vurugu na walinzi wa Yanga wakati timu hiyo ikiwasili uwanjani, jambo lililosababisha kila upande (Simba na Yanga) kutozwa faini ya Sh5 milioni kwa kuchafua taswira ya mchezo.

Kwa upande wa wachezaji, mshambuliaji wa Simba, Seleman Mwalimu amefungiwa michezo mitatu na kutozwa faini ya Sh1 milioni kwa kumpiga kiwiko mchezaji wa Dodoma Jiji wakati wa mchezo baina ya timu hizo.

vilevile, beki wa timu hiyo, David Kameta  ametozwa faini ya Sh1 milioni baada ya kuonekana akimwaga kimiminika uwanjani kabla ya mchezo dhidi ya Yanga, kitendo kilichotafsiriwa kuwa ni imani za kishirikina.

Katika tukio lingine, baadhi ya waamuzi wa mechi  ya dabi wameadhibiwa akiwamo mwamuzi msaidizi Kassim Mpanga aliyefungiwa miezi sita kwa kukataa bao halali la Simba lililofungwa na Mwalimu, huku mwamuzi msaidizi mwingine, Hamdan Said akifungiwa miezi mitatu kwa kosa la kutafsiri vibaya sheria ya kuotea.

Mbali na Simba na Yanga, timu na maofisa wengine wamekumbana na adhabu mbalimbali, ambapo Dodoma Jiji imetozwa faini ya Sh5 milioni baada ya wahudumu wa huduma ya kwanza kuchelewa kuingia uwanjani mara kadhaa wakati wa mchezo dhidi ya Simba, kitendo kilichotafsiriwa ni kupoteza muda.

Dodoma Jiji pia imetozwa faini ya Sh5 milioni kwa kufanya mabadiliko ya wachezaji mara nne badala ya tatu kama kanuni zinavyotaka.

Beki wa kati wa timu hiyo, Abdi Banda  amefungiwa michezo mitatu na kutozwa faini ya Sh1 milioni kwa kujirusha kutoka kwenye machela ili kupoteza muda, ilhali mwamuzi wa akiba wa mechi hiyo, Charles Simon amefungiwa miezi mitatu kwa kuruhusu mabadiliko manne.

Mwamuzi wa kati Abdallah Mwinyimkuu ameshushwa daraja baada ya kushindwa kutafsiri vyema sheria katika mchezo kati ya Namungo FC na Yanga uliochezwa Ruangwa, Lindi.