Programu ya Mwanamke wa Wakati ujao ambayo ilianzishwa mwaka 2015 imefikia kundi (Cohort) la 11 ikiwa inajumuisha wanawake wasomi kutoka makampuni mbalimbali, ilianzishwa Chama cha Waajiri Tanzania(ATE) kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Waajiri nchini Norway na katika kipindi cha muda mfupi imekuwa msaada mkubwa katika kuwajengea uwezo katika utawala katika sehemu zao za kazi.
Akihojiwa kuhusu ushiriki katika progamu hiyo mmoja wa wahitimu kutoka mgodi wa Barrick North Mara, Edith Biita, alisema anajivunia kuajiriwa na kampuni kubwa kama Barrick ambayo imekuwa mstari wa mbele kuwapatia wafanyakazi wanawake nafasi za uongozi na nafasi inayomuwezesha kutoa maamuzi ambayo yeye na wafanyakazi wenzake wanawake ndani ya kampuni wanayo fursa ya kutoa mawazo yao na yamekuwa yakiheshimiwa bila kujali jinsia na umri wao.
Akiwa ni msomi wa fani ya uhandisi wa madini akifanya kazi katika kitengo cha Uchimbaji na milipuko (Drill and Blast) alisema mafunzo aliyopapata kupitia programu hiyo ni ya aina yake kwa kuwa yanawezesha kupata maarifa ya masuala mbalimbali hususani utawala kwa kuwa katika fani zote suala la utawala na uongozi lipo.
Naye Sella Mwangomole mtaalamu wa metolojia na maabara alisema mafunzo yanayotolewa na program hii yanawezesha kujiamini zaidi katika utawala na alitoa ushauri kuwa kuna haja ya kuwa na programu nyingi za aina hii ili ziwafikie wanawake wengi popote walipo nchini ili wasibaki nyuma katika utawala kwenye sekta mbalimbali.
“Ili wanawake wengi kutobaki nyuma silaha pekee ya kuwakwamua ni elimu na ninaposema elimu simaanishi kupata shahada za juu pekee bali ni kujifunza mambo mbalimbali na kupata maarifa, kuungana na kushirikiana ambapo watapata fursa ya kubadilishana uzoefu wa masuala mbalimbali,kupeana moyo na kupanga mikakati ya kutatua changamoto zinazowakabili”.Alisema Mwangomole.
Naye Noela Mataro alishukuru Barrick kupitia mgodi wa North Mara kwa kumpatia fursa ya kupata mafunzo haya ya utawala na kuongeza kuwa anavutiwa na sera ya kampuni ya kuwapatia nafasi za uongozi wanawake katika vitengo mbalimbali ambapo wanaendelea kufanya vizuri na kudhihirisha kuwa ujuzi hauna jinsia.
Mshiriki mwingine kutoka Barrick, Patricia Vullah, alisema Mpango wa kuwapatia wanawake mafunzo ya utawala ya Female Future Programme ni moja ya jukwaa la kuwanyanyua wanawake wa Tanzania na kuwafikisha kwenye nafasi za juu za uongozi na kutoa maamuzi.
Kwa upande wake Elda Mahenda alisema kupitia Programu hii alisema wanafundishwa masuala mengi hususani utawala wenye kuleta ufanisi kwa makampuni, kujiaamini na jinsi ya kushiriki na kuchangia mawazo katika vikao vya juu vya bodi za makampuni “Mtaala wa kufundishia unaotumika ni mzuri na ndani ya kipindi cha muda mfupi unaweza kumbadilisha mtu kuwa na maarifa na upeo mkubwa na kujiamini”, alisema.
Kampuni ya Barrick nchini imekuwa mstari wa mbele kutekeleza sera imara ya kukuza usawa wa kijinsia kwa kuwawezesha wanawake kushika nafasi za uongozi na kiufundi katika migodi yake ya Bulyanhulu,North Mara na Buzwagi ambao uko katika mchakato wa kufungwa pia inazingatia ushirikishwaji wa wanawake, mafunzo, na programu za ndani na nje zinazolenga kukuza vipaji vyao ili kuongeza uwakilishi katika ngazi za maamuzi.
Katika kuadhimisha Siku yaWanawake Duniani, Kampuni inatumia siku hii kama jukwaa la kutathmini na kuendeleza juhudi za wanawake kazini, kusaidia jamii zinayozunguka migodi na Kuchochea wanawake kuingia katika sekta ya madini ambayo awali ilitawaliwa na wanaume.
Juhudi hizi za uwezeshaji wanawake zinaendana na sera ya serikali ya kuongeza ushirikishwaji wa Watanzania (Local Content) na kuimarisha uwakilishi wa wanawake katika mnyororo wa sekta ya madini.



