Karatu. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amemwagiza Kamishna Jenerali wa Uhamiaji nchini, kumtafuta popote alipo mkandarasi wa kampuni ya Tunnel Sade Ariana na kumnyang’anya hati yake ya kusafiria kwa kushindwa kutekeleza mradi wa ujenzi wa bwawa katika mradi wa umwagiliaji wa Ziwa Eyasi.
Akizungumza leo Ijumaa, Machi 6, 2026 katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Mazingira, mjini Karatu mkoani Arusha, Waziri Mkuu Mwigulu amesema mkandarasi huyo amelipwa fedha za Serikali, lakini hajaanza kazi licha ya kukusanya vifaa vya ujenzi pekee.
“Huyu mtu amelipwa fedha na Serikali, lakini amepata wapi ujasiri wa kutufungulia kesi mahakamani wakati amekusanya vifaa tu na hajaanza kazi? Hii haikubaliki, ni dharau kwa nchi. Nimemwagiza Kamishna wa Uhamiaji amtafute popote alipo na anyang’anywe pasi yake ya kusafiria ili asiende kokote,” amesema kiongozi huyo.
Amesema mkandarasi huyo alipaswa kujenga mradi huo wenye thamani ya Sh21 bilioni na tayari ameshapokea malipo ya awali ya Sh3 bilioni lakini utekelezaji wa kazi haujaanza.
Dk Mwigulu amesema Serikali imebaini kuwapo kwa baadhi ya makandarasi wanaochelewesha miradi kwa sababu mbalimbali, ikiwamo kutaka malipo ya fedha kupelekwa katika akaunti zao zilizopo nje ya nchi.
“Ipo michezo ya baadhi ya wakandarasi, hasa wale wanaotaka walipwe fedha kwenye akaunti zao za nje. Nilishatoa maelekezo kuwa kuanzia sasa malipo yote ya wakandarasi yafanyike kupitia akaunti zao zilizopo kwenye benki za hapa nchini,” amesisitiza.
Mapema, Waziri Mkuu aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa skimu za umwagiliaji katika Bonde la Eyasi, lililopo takribani kilometa 50 kutoka mjini Karatu.
Amesema mradi huo ni sehemu ya miradi 780 ya umwagiliaji inayotekelezwa na Serikali katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa kilimo na kuboresha maisha ya wakulima.
“Mradi huu ni kama miradi mingine inayoendelea kutekelezwa katika maeneo ya Isimani na Msingi. Miradi hii siyo ya Serikali peke yake, bali ni kwa ajili ya kuwahudumia wakulima wa vijijini. Serikali haitavumilia uzembe, wizi wala udokozi katika miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa fedha za walipakodi,” amesema.
Kwa mujibu wa taarifa ya mradi iliyowasilishwa, unaotekelezwa na Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji unatarajiwa kugharimu Sh38.4 bilioni.
Hadi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 30 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba mwaka huu.
Kukamilika kwa mradi huo kunatarajiwa kuwanufaisha zaidi ya wakulima 2,500 kutoka skimu za Mang’ola Barazani, Maleckchand, Laghangareri, Mbuga Nyekundu, Jobaji na Dumbechand zenye jumla ya zaidi ya hekta 5,000.
Aidha, utekelezaji wa mradi huo utasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa upotevu wa maji unaotokea katika mifereji ya asili, hatua itakayoongeza ufanisi wa matumizi ya maji na kuimarisha uzalishaji wa mazao katika eneo hilo.