TIKETI ya kuisaka michuano ya kimataifa msimu ujao, inaanza leo Ijumaa kwa mechi za raundi ya 32 bora ya Kombe la Shirikisho la CRDB, huku JKT Tanzania, Dodoma Jiji na TRA United zinazoshiriki Ligi Kuu Bara, zikishuka viwanja mbalimbali.
JKT Tanzania iliyoichapa Pan African mabao 7-0, katika mechi ya raundi ya 64 bora, itakuwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam kucheza dhidi ya Hausung FC ya Njombe, iliyoitoa West Singers ya jijini Mwanza kwa kuichapa mabao 2-1.
Kwenye Uwanja wa Black Rhino jijini Arusha, wenyeji TRA United iliyoitoa Rhino Rangers ya Tabora kwa bao 1-0, itacheza dhidi ya Kijiwe Nongwa ya Songwe, iliyoichapa Barberian FC kwa penalti 4-2 baada ya sare ya 1-1 ndani ya dakika 90.
Mechi ya mwisho leo itapigwa Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma na Dodoma Jiji baada ya kuitoa Kilimanjaro Wonders ya Kilimanjaro kwa kuichapa mabao 3-1, inakutana na African Sports ya Tanga iliyoitoa Kilimo FC ya Singida kwa mabao 4-1.
Kocha wa Dodoma Jiji, Amani Josiah alisema licha ya heshima kubwa kutokana na bingwa kupata nafasi ya kuiwakilisha nchi katika michuano ya CAF, ila nidhamu ndiyo kitu muhimu cha kuzingatia, hususan unapocheza na timu za madaraja ya chini.
“Unapocheza na timu za chini jambo la kwanza kwa wachezaji huchukulia ni mechi nyepesi na wanayoweza kufanya chochote, sasa hii ni hatari kwa sababu unapozidi kujiamini ndivyo ambavyo mpinzani wako pia anakushangaza,” alisema Josiah.
Kwa upande wa Kocha Mkuu wa African Sports, Khalid Adam alisema mechi dhidi ya Dodoma Jiji itakuwa ngumu kutokana na ubora wa wapinzani wao, ingawa hawatacheza kwa kuwahofia, isipokuwa watajilinda vizuri na kushambulia kwa kuwashtukiza.
TRA United vs Kijiwe Nongwa (Saa 10:00 Jioni)
Dodoma Jiji vs African Sports (Saa 10:00 Jioni)
JKT Tanzania vs Hausang (Saa 10:00 Jioni)
Pamba Jiji vs Transit Camp (Saa 10:00 Jioni)
Mashujaa vs Kengold (Saa 10:00 Jioni)
Geita Gold vs Nyika (Saa 10:00 Jioni)
Simba SC vs B19 (Saa 1:15 Usiku)
Namungo vs Kagera Sugar (Saa 10:00 Jioni)
Mbeya City vs Bandari Tanzania (Saa 10:00 Jioni)
Fountain Gate vs Gunners (Saa 10:00 Jioni)
Mtibwa Sugar vs Mbuni (Saa 10:00 Jioni)
Tanzania Prisons vs TMA Stars (Saa 10:00 Jioni)
Azam FC vs Mbeya Kwanza (Saa 3:15 Usiku)
Singida BS vs Songea United (Saa 10:00 Jioni)
Coastal Union vs Stand United (Saa 10:00 Jioni)
Yanga vs Polisi Tanzania (Saa 1:15 Usiku)