Kihongosi ataka ujenzi stendi Shinyanga ukamilike, ang’aka mkwamo malipo ya vibarua

Shinyanga. Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi, amesisitiza kukamilika kwa wakati kwa ujenzi wa stendi mpya ya mabasi ya Shinyanga Mjini, huku akitoa maelekezo kwa wahusika kuhakikisha vibarua katika mradi huo wanalipwa malipo yao kabla hajaondoka mkoani humo kesho, Machi 7, 2026.

Kwa mujibu wa mkataba wa ujenzi, mradi huo unatarajiwa kukamilika Oktoba mwaka huu, lakini mpaka sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 35.

Kihongosi yuko mkoani Shinyanga kwa ziara ya siku nne inayolenga kufuatilia uimarishaji wa uhai wa chama, kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa fedha za Serikali, pamoja na kusikiliza kero za wananchi.

Leo Ijumaa, Machi 6, 2026, ameanza ziara yake ya ukaguzi kwa kutembelea mradi wa ujenzi wa stendi hiyo iliyopo katika Kata ya Kizumbi. Baadaye alipanga kukagua mradi wa ujenzi wa uwanja wa ndege uliopo Kata ya Ibadakuli, kisha kufanya kikao cha chama na mabalozi wa chama katika Kata ya Lubaga, kabla ya kuhutubia mkutano wa hadhara katika uwanja wa Shule ya Msingi Town, Kata ya Mjini, Shinyanga Mjini.

Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi akikagua  ujenzi wa stendi mpya ya Shinyanga mjini.



Akiwa katika eneo la mradi wa ujenzi wa stendi hiyo, Kihongosi ametoa maelekezo matatu, likiwamo la kukamilika kwa mradi huo kwa wakati na kuhakikisha vibarua wanalipwa malipo yao kwa wakati.

Amesema Serikali imetoa zaidi ya Sh26 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika eneo hilo, ambayo ni pamoja na ujenzi wa stendi hiyo na barabara za Nguzonane–Mwawaza na Sywinatone–Ndala.

“Serikali imetoa zaidi ya Sh26 bilioni katika ujenzi huu na ule wa barabara ya Nguzonane–Mwawaza na Sywinatone–Ndala. Mradi huu unaendelea vizuri na majengo yanajengwa kwa ubora, sijaona mapungufu katika majengo haya,” amesema Kihongosi.

Ameongeza kuwa, kwa mujibu wa mkataba, mradi huo umebakiwa na miezi 15 kukamilika, hivyo ni lazima umalizike ndani ya muda uliopangwa.

“Mkataba wa mradi ni wa miezi 15 na unatakiwa kukamilika Oktoba. Mmenieleza kuwa changamoto kubwa imekuwa mvua, lakini nitoe rai ya kuongeza kasi ya kazi na vifaa ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati,” amesisitiza.

Kuhusu malipo ya vibarua, Kihongosi amesema ni muhimu wahusika kuhakikisha wanawalipa haraka iwezekanavyo, ikiwezekana kabla hajaondoka mkoani Shinyanga kesho Jumamosi.

Kauli hiyo ilishangiliwa kwa nguvu na baadhi ya vibarua waliokuwepo katika eneo la mradi huo.

Baadhi ya vibarua hao, ambao wameomba kuhifadhiwa majina yao ili kulinda ajira zao, wamedai kuwa hawajalipwa malipo yao kwa zaidi ya wiki moja, huku wakisema ujio wa kiongozi huyo umewapa matumaini.

“Hatimaye tutalipwa malipo yetu na familia zetu zitafurahia matunda ya kazi zetu. Tunamshukuru sana kiongozi wetu kwa kutusikiliza,” amesema mmoja wa vibarua hao kwa niaba ya wenzake.

Kufuatia malalamiko hayo, Kihongosi amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, kusimamia suala hilo na ahakikishe vibarua wote wanalipwa kwa wakati kabla hajaondoka mkoani humo kesho.

Kwa mujibu wa wahusika wa mradi huo, kila kibarua hulipwa Sh16,050 kwa siku na malipo hayo hutolewa kila wiki.

Mhandisi mshauri wa mradi huo amesema vibarua hao wanafanya kazi chini ya mkandarasi mdogo (sub-contractor).

Mbali na maelekezo hayo, Kihongosi amewataka pia wananchi kuhakikisha wanaitunza stendi hiyo pindi itakapokamilika, pamoja na miundombinu mingine ya maendeleo, akisisitiza kuwa miradi hiyo ni kwa manufaa ya wananchi wa sasa na vizazi vijavyo.

“Sisi kama chama tutaendelea kuisimamia Serikali ili miradi kama hii itekelezwe kwa ufanisi. Mradi huu pia upo katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi,” amesema.

Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi akikagua  ujenzi wa stendi mpya ya Shinyanga mjini.



Akitoa maelezo kuhusu maendeleo ya mradi huo, mshauri wa mradi, Emmanuel Kisimba, amesema ujenzi wa majengo mengi umefikia hatua ya boma, ikiwamo kufunga lenta juu ya madirisha na kuendelea na kozi za juu ya lenta.

Amesema hadi sasa utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 35, huku changamoto kubwa ikiwa ni mvua zinazoathiri ratiba ya kazi zilizopangwa.

“Ili kukabiliana na changamoto hiyo, tumepanga kufanya kazi ambazo haziathiriwi na mvua katika kipindi hiki, pamoja na kuendelea na shughuli katika maeneo ambayo tayari miundombinu imeondolewa,” amesema Kisimba.

Ameongeza kuwa mkandarasi ameweka mikakati ya kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati, ikiwamo kufanya kazi kwa mfumo wa zamu mchana na usiku (shift system) ili kuongeza kasi ya utekelezaji.

Pia amesema idadi ya mafundi na wafanyakazi imeongezwa mara mbili ili kupunguza muda wa utekelezaji wa shughuli mbalimbali za ujenzi.