Watu wanapofikiria kuhusu watu wanaokwenda vituo vya mazoezini (gym) huku wakitumia steroidi, picha inayokuja akilini mara nyingi ni ya wanamume wanaonyanyua vyuma vizito, kama Arnold Schwarzenegger, au washawishi wa kisasa wa mitandao ya kijamii wanaoonyesha misuli yao.
Lakini leo taswira hiyo inabadilika. Wanawake sasa wanawakilisha sehemu inayokua ya watu wanaotumia steroidi.
Kitaalamu, steroidi kwa Kiingereza steroid ni dawa au kemikali inayotumika kubadilisha kazi za mwili.
Kwa steroidi aina ya ‘anabolic’ , hizi zinasaidia kuongeza misuli na nguvu za mwili, na baadhi ya watu wanazitumia kwa ajili ya michezo au mwonekano wa kimwili.
Matumizi yake yasiyo ya kibiashara yana hatari kubwa, ikiwa ni pamoja na kusababisha matatizo ya moyo na mishipa ya damu, mabadiliko ya homoni (kama kupungua kwa idadi ya manii kwa wanaume), kuathirika kwa ini na figo na mtu kupatwa na hali ya hasira au tabia za kihisia zisizo za kawaida.
Utafiti unaonyesha kuwa wanawake wanazidi kuongezeka katika jamii zinazotumia steroidi, ingawa takwimu sahihi za muda mrefu ni chache.
Mapitio ya mwaka 2024 ya tafiti za kimataifa yalibaini kuwa takriban asilimia nne ya wanawake wazima walikuwa wametumia steroidi (anabolic steroids) angalau mara moja, ongezeko kutoka asilimia 1.6 mwaka 2014.
Miongoni mwa wanawake wanaojenga misuli, karibu asilimia 17 yaani mmoja kati ya sita wanaripoti kutumia steroidi.
Viwango hivyo viko juu kwa wanawake wanaoshiriki michezo ya nguvu au wanaoshiriki unyanyuaji vyuma kiburudani kuliko wanawake wa kawaida.
Ushahidi huu unaoibuka unaonyesha kuwa wasifu wa kijinsia wa matumizi ya steroidi unabadilika, hata kama takwimu sahihi za kihistoria hazipo kuthibitisha kiwango kamili cha ongezeko hilo.
Mwenendo huu bila shaka unaakisi kile kinachotokea maeneo mengi yaani ukuaji unaoendelea wa jamii za watu wanaopenda kujenga mwili na ushupavu wa mwili, wakiwamo wanawake wanaoshiriki michezo ya nguvu.
Hata hivyo, matumizi ya steroidi yanaweza kuwa chanzo cha wasiwasi bila hatua madhubuti za kupunguza madhara kupitia elimu na huduma za afya.
Wakati steroidi zina hatari kwa kila mtu, wanawake wanaweza kukabiliwa na madhara ya kipekee ambayo hayawezi kutibika. Haya ni pamoja na kuota nywele usoni na mwilini, sauti kuwa nzito na mabadiliko ya hedhi au ugumba.
Hatari nyingine ni kupungua kwa tishu za matiti, kuota chunusi na kupoteza nywele, kuongezeka kwa ukubwa wa kinena na mabadiliko makali ya hisia, ikiwa ni pamoja na wasiwasi na hasira.
Zaidi ya hatari hizi, utafiti mmoja nchini Australia unaonyesha hatari nyingine: bidhaa nyingi za steroidi zinazouzwa kinyume cha sheria zina uchafuzi wa sumu kama vile madini ya risasi, aseniki na kadmiamu, vitu vinavyohusishwa na saratani, uharibifu wa viungo, na magonjwa ya moyo.
Hatari kubwa zaidi za muda mrefu ni zile ambazo watu huzungumzia kwa nadra: ugonjwa wa moyo, kiharusi, uharibifu wa ini, na matatizo ya afya ya akili.
Mahojiano na wanawake wanaotumia steroidi yanaonyesha kuwa wengi wana taarifa chache kuliko wanaume kuhusu hatari hizi, mara nyingi kwa sababu utafiti kihistoria umejikita zaidi kwa wanaume.
Pia kuna suala la unyanyapaa. Wanawake wanaripoti kuhukumiwa kwa ukali zaidi kuliko wanaume wanapotafuta msaada wa matibabu, na baadhi huepuka kabisa huduma za afya. Hilo huwafanya wawe hatarini zaidi kwa matatizo ya kiafya.
Tunawezaje kubadili mwenendo huu?
Moja, elimu kwa wanawake. Taarifa nyingi za steroidi mtandaoni zimeandikwa kwa ajili ya wanaume. Mashirika ya afya yanahitaji kutoa taarifa wazi kwa wanawake zinazoelezea hatari kwa uaminifu na bila aibu.
Mbili kuwatafuta wanawake kule waliko: Mitandao ya kijamii ndipo wanawake wengi hujifunza kuhusu dawa hizi, hivyo inapaswa pia kuwa mahali wanapoona taarifa sahihi kuhusu madhara yake.
Hii inaweza kujumuisha kushirikiana na washawishi wa mitandao wanaoaminika hasa wanawake ambao wanaweza kuelezea hatari na kukuza mbinu salama za mazoezi.
Tatu, kupunguza unyanyapaa katika huduma za afya: Wanawake wanaotumia steroidi wanaweza kuwaepuka madaktari kwa sababu ya hofu ya kuhukumiwa. Kuwafunza watoa huduma za afya kuwahudumia bila kutoa hukumu za kimaadili, kungewafanya wanawake waweze kutafuta msaada mapema.
Makala haya yaliyoboreshwa awali yalichapishwa katika mtandao wa Jarida la The Conversation.