Manyara watakiwa kuchukua tahadhari ya uviko – 19

Babati. Wananchi wa Mkoa wa Manyara wametakiwa kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa ya maambukizi ya mfumo wa upumuaji, ukiwemo Uviko-19, licha ya kutokuwapo kwa kisa chochote kilichoripotiwa kwa sasa mkoani humo.

Wito huo umetolewa leo Ijumaa, Machi 6, 2026 mjini Babati na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dk Andrew Method wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa kuendelea kujikinga na magonjwa ya kupumua.

Dk Method amesema hadi sasa hakuna mgonjwa wa Uviko-19 aliyeripotiwa katika mkoa huo, lakini wananchi wanapaswa kuwa waangalifu na kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya ili kujilinda dhidi ya magonjwa ya maambukizi ya mfumo wa upumuaji.

“Wananchi wa Manyara wanatakiwa kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa ya mlipuko, ikiwemo Uviko-19 ambao uliripotiwa hivi karibuni katika baadhi ya maeneo hapa nchini,” amesema.

Ameongeza kuwa katika kipindi cha mvua kumekuwa na ongezeko la magonjwa mbalimbali, hali inayolazimu wananchi kuzingatia kanuni za afya ili kujikinga.

“Mpaka sasa hakuna kisa chochote kilichoripotiwa katika mkoa wetu, lakini kutokana na hali ilivyo, ni muhimu kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa ya kupumua, ikiwemo Uviko-19,” amesema.

Kwa upande wake, Ofisa Afya wa Mkoa wa Manyara, Switen Mwabulambo amewahimiza wananchi kuzingatia kanuni za usafi wa mazingira na mwili ili kupunguza hatari ya maambukizi.

Mwabulambo amesema ni muhimu kwa wananchi kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono, pamoja na kuepuka kusalimiana kwa kushikana mikono.

Amesema kushikana mikono kunaweza kuchangia kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza, hivyo ni vyema jamii ikachukua tahadhari katika mawasiliano ya karibu.

Baadhi ya wakazi wa Babati wamewapongeza wataalamu wa afya kwa kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu namna ya kujikinga na magonjwa ya maambukizi.

Mkazi wa mtaa wa Ngarenaro mjini Babati, Elizabeth Bura amesema ni muhimu elimu hiyo ikaendelea kutolewa mara kwa mara ili kuwasaidia wananchi kukumbuka na kuzingatia tahadhari za kiafya.

Amesema licha ya kuwa ni jukumu la wataalamu wa afya kutoa elimu kwa jamii, wanastahili pongezi kwa juhudi wanazofanya za kuelimisha wananchi kuhusu kujikinga na magonjwa.