Mapigano Marekani, Israel na Iran yazidi kupanuka

Ni piga nikupige. Ndivyo unavyoweza kuelezea hali ya mambo Mashariki ya Kati ambapo mashambulizi yanayohusisha Marekani na Israel dhidi ya Iran yameendelea siku ya sita huku Iran nayo ikijibu mapigano kwa Israel na kambi za kijeshi za Marekani katika ukanda huo.

Kutokana na Iran kuzilenga kambi za Marekani, imejikuta ikirusha makombora yake hadi katika mataifa mengine ya jirani ambayo hayahusiki moja kwa moja katika mzozo huo, jambo ambalo limeifanya vita hiyo kuwa ya ukanda mzima.

Wakati Marekani ikiilenga Iran pekee katika mashambulizi yake, Israel nayo inarusha makombora kwa Iran na Lebanon ikikilenga kikundi cha Hezbollah.

Iran mbali na kuishambulia Israel pia inazilenga kambi za Marekani zilizo katika nchi za Qatar, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Kutokana na ujirani uliopo, mataifa mengine yamejikuta yakiathirika na mapigano hayo licha ya kuwa hazihusiki moja kwa moja katika mzozo huo. Mataifa hayo ni pamoja na Kuwait, Oman, Bahrain, Uturuki na Iraq.

Mashambulizi ya Marekani, Israel

Shirika la Red Crescent la Iran limerekodi mashambulizi 1,332 yaliyofanywa na majeshi ya Marekani na Israel nchini Iran tangu Jumamosi iliyopita huku mashambulizi hayo yakitua katika maeneo 636, yakiwemo 105 ya makazi ya watu.

Maeneo hayo yanajumuisha vituo 14 vya afya na majengo saba ya Red Crescent, shirika hilo limesema, likiongeza kuwa takribani miji 174 imeathiriwa na mashambulizi hayo.

Hata hivyo, majeshi ya Marekani yameripoti kushambulia karibu malengo 2,000 ndani ya Iran tangu Jumamosi, kwa mujibu wa kamandi inayosimamia majeshi hayo katika eneo la Mashariki ya Kati.

Mapema leo Machi 5, 2026, mashambulizi ya anga ya Israel yamelenga miji ya Harouf na Kfar Rumman kusini mwa Lebanon, kwa mujibu wa Shirika la Habari la Uingereza- Reuters.

Shirika hilo limesema takribani watu wanane wameuawa kutokana na mashambulizi ya Israel katika maeneo mbalimbali ya Lebanon leo.

Kwa upande wa pili, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) limesema limefanya mashambulizi dhidi ya takribani kambi 27 katika Mashariki ya Kati ambako wanajeshi wa Marekani wamewekwa, pamoja na vituo vya kijeshi vya Israel huko Tel Aviv na maeneo mengine ya nchi hiyo.

Kwa jumla, Iran imerusha makombora 500 na ndege zisizo na rubani 2,000 katika siku nne za kwanza za mapigano, kwa mujibu wa Brad Cooper, mkuu wa Centcom.

Hadi sasa, Iran imefanya mashambulizi katika nchi tisa za eneo hilo: Bahrain, Iraq, Jordan, Kuwait, Oman, Qatar, Saudi Arabia na United Arab Emirates. Ndege isiyo na rubani ya Iran pia ilipiga njia ya kurukia ndege katika kambi ya kijeshi ya Uingereza iliyopo Cyprus.

Mashambulizi mengi kati ya hayo yamezuiliwa kabla hayajafika kwenye malengo (targets) yao.

Vilevile, mifumo ya ulinzi wa anga ya Iran imeangusha ndege isiyo na rubani ya Israel aina ya Hermes, katika jimbo la Hamedan, kwa mujibu wa Shirika la Habari la Iran, Tasnim.

Ripoti hiyo inakuja wakati Israel imetangaza kuanzisha wimbi jipya la mashambulizi katika maeneo mbalimbali ya Iran.

Katika tukio jingine, IRGC imesema jeshi lake la wanamaji limeshambulia meli ya mafuta ya Marekani katika Ghuba ya Kaskazini asubuhi ya Machi 5, ikibainisha kwamba meli za kijeshi na za kibiashara za Marekani, Israel na nchi za Ulaya zinazowaunga mkono “hazitaruhusiwa kupita.”

“Ikiwa zitaonekana, hakika zitashambuliwa,” IRGC imesema.

“Awali tulisema kwamba, kwa kuzingatia sheria na maazimio ya kimataifa, wakati wa vita, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itakuwa na haki ya kudhibiti upitaji wa meli katika Mlango Bahari wa Hormuz,” IRGC imesema, kwa mujibu wa ripoti ya Tasnim News Agency.

Iran, ambayo inashambuliwa na mataifa mawili, inatajwa watu wake 1,230 wameuawa, wakiwemo watoto 175 wa shule na wafanyakazi, katika shambulio la kombora Jumamosi lililolenga shule katika mji wa Minab.

Huko Israel, watu 11 wametajwa kuuawa, wakiwemo tisa katika shambulizi la kombora la Iran lililolenga mji wa Beit Shemesh, Machi mosi, 2026.

Marekani nayo imepoteza wanajeshi wake sita kutokana na mashambulizi ya Iran yaliyoelekezwa kwenye kambi zake za kijeshi.

Lebanon, pia, imeshuhudia idadi kubwa ya vifo ambapo takribani watu 77 wameuawa kutokana na mashambulizi ya Israel tangu Jumatatu, wiki hii.

Huko Bahrain, mtu mmoja ameuawa baada ya moto kuibuka katika mji wa viwanda wa Salman kutokana na kombora la kuzuia makombora ya Iran.

Watu wanne, wakiwemo wanajeshi wawili wa Kuwait, wameuawa katika mashambulizi ya Iran dhidi ya nchi hiyo.

Huko Oman, mtu mmoja ameuawa huku watatu nao wakipoteza maisha UAE kutokana na mashambulizi ya Iran.