Mbaroni akidaiwa kumuua mtoto mchanga baada ya kujifungua

Morogoro. Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za mauaji, akiwemo mwanamke anayedaiwa kumuua mtoto wake mchanga baada ya kujifungua.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 6, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama, amesema jeshi hilo linamshikilia mkazi wa Mlima, wilaya ya Kilombero, Elizabeth Leonard Colnery (17), akidaiwa kumuua mtoto wake mchanga baada ya kujifungua.

Amesema mtuhumiwa huyo alijifungua mtoto wa kike, kisha kumuua akiwa na umri wa siku moja, na baadaye kumtupa kwenye korongo katika eneo la Tazara, kijiji cha Mlima wilayani humo.

“Hili tukio limetokea Machi 5, 2026, majira ya alfajiri. Baada ya kufanya tukio hilo, mtuhumiwa alijaribu kutoroka, lakini alikamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi. Uchunguzi zaidi unaendelea ili hatua za kisheria zichukuliwe,” amesema Kamanda Mkama.

Kamanda Mkama amesema uchunguzi wa awali unaonesha chanzo cha tukio hilo ni mmomonyoko wa maadili katika jamii, huku akitoa wito kwa wazazi na walezi kuendelea kutoa malezi bora kwa vijana ili kuepuka matukio ya aina hiyo.

Katika tukio lingine, Kamanda Mkama amesema jeshi hilo limemkamata Dki Emmanuel David Ibrahimu (33), mkazi wa Mzumbe, wilaya Mvomero, kwa tuhuma za kusababisha ajali ya barabarani iliyogharimu maisha ya mtu mmoja.

Kamanda Mkama amesema ajali hiyo ilitokea Machi 5, 2026, majira ya usiku, katika kijiji cha Changalawe, kata ya Mzumbe, wilaya ya Mvomero, kwenye barabara ya Mzumbe kuelekea Mlali.

Mtuhumiwa alikuwa akiendesha gari aina ya Toyota Spacio akitokea Mlali kuelekea Mzumbe alipogongana na pikipiki aina ya Haojue iliyokuwa ikiendeshwa na Samson Efrem (16).

Kamanda Mkama amemtaja aliyefariki kwa kugongwa na gari kuwa ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Mongola. “Kutokana na ajali hiyo, dereva wa pikipiki alifariki dunia papo hapo, huku pikipiki hiyo ikipoteza mwelekeo na kumgonga Elisha Moses John (24),” amesema.