Mjadala wa ubora wa wahitimu wawekwa mezani

Dar es Salaam. Wakati mjadala kuhusu ubora wa wahitimu wanaozalishwa na vyuo vikuu nchini ukiendelea kushika kasi, Serikali imeitaka Bodi mpya ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kuimarisha usimamizi na mifumo ya uthibiti wa ubora wa elimu ya juu ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira.

Kauli hiyo imetolewa leo Machi 6, 2026, jijini Dar es Salaam na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, wakati akizindua bodi mpya ya TCU itakayoongozwa na mwenyekiti, Profesa Makenya Maboko.

Wito huo unakuja wakati wadau wa elimu, waajiri, na wachambuzi wakizidi kujadili ubora wa baadhi ya wahitimu wa vyuo vikuu nchini, huku baadhi ya waajiri wakilalamikia ukosefu wa ujuzi wa vitendo na uwezo wa kukidhi mahitaji ya soko la ajira kwa baadhi ya wahitimu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Profesa Mkenda amesema TCU ina nafasi ya kimkakati katika kusimamia, kuratibu, na kuthibiti ubora wa elimu ya chuo kikuu ili kuhakikisha vyuo vinazalisha wahitimu wenye maarifa, ujuzi, na ubunifu unaohitajika katika maendeleo ya Taifa.

“Tume imebeba jukumu kubwa la kulinda ubora wa elimu ya juu pamoja na imani ya umma katika vyuo vikuu vyetu,” amesema Profesa Mkenda.

Amesema katika mazingira ya sasa, ambapo sekta ya elimu ya juu imekua kwa kasi, ni muhimu kuhakikisha vyuo vikuu vinaendesha shughuli zake kwa kuzingatia utawala bora na mifumo madhubuti ya uthibiti wa ubora wa elimu.

Ameongeza kuwa lengo ni kupata wahitimu wenye uwezo wa kushindana, sio tu ndani ya nchi bali pia katika ngazi ya kikanda na kimataifa.

Kwa upande wake, Profesa Maboko ameishukuru Serikali kwa imani iliyoiweka kwa Bodi hiyo, akisema makamishna watafanya kazi kwa karibu na Sekretarieti ya TCU kuimarisha mifumo ya ndani ya uthibiti wa ubora wa elimu ya chuo kikuu.

Waziri wa Elimu Profesa Adolf Mkenda akimkabidhi mkoba wenye vitendea kazi Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) Profesa Makenya Maboko wakati wa uzinduzi wa bodi mpya ya tume hiyo.



Amesema pamoja na changamoto zinazoibuliwa katika mjadala wa ubora wa wahitimu, taasisi za elimu ya juu zina jukumu la kuendelea kuboresha mitaala, mbinu za ufundishaji, na ushirikiano na sekta ya ajira ili kuhakikisha wahitimu wanapata ujuzi unaohitajika katika ulimwengu wa kazi.

“Jukumu letu si la kiutawala pekee, bali ni la kimkakati kuhakikisha elimu ya chuo kikuu nchini inabaki kuwa yenye kuaminika, yenye ushindani, na inayokidhi mahitaji ya soko la kitaifa, kikanda, na kimataifa,” amesema Profesa Maboko.

Kabla ya uzinduzi huo, makamishna wa TCU walishiriki warsha ya kimkakati iliyofanyika Machi 5 hadi 6, 2026, iliyolenga kutathmini hali ya elimu ya juu nchini na kuilinganisha na mifumo ya elimu ya juu ya baadhi ya nchi za Afrika, ikiwamo Mauritius, Afrika Kusini, na Kenya, kwa lengo la kujifunza mbinu bora za kuimarisha ubora.