Dar es Salaam. Alipoajiriwa kuwa mwalimu wa sekondari mwaka 2013 katika Shule ya Sekondari Mwatulole, mkoani Geita, aliamini ndoto yake ya kuajiriwa serikalini imeanza kutimia.
Lakini siku aliyosaini mkataba na kuona mshahara wake wa ‘take home’ wa Sh470,000, moyo ulishtuka. Alijua fedha hiyo isingetosha kumudu maisha ya kupanga nyumba, kusaidia familia na kujikimu kwa mahitaji ya kila siku.
“Nilipojiuliza, nitaishije?” anasimulia Nkwimba Hillu (39), ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Mando Women Group.
Maisha ya Geita hayakuwa mepesi. Kodi ya nyumba ilikuwa juu, gharama za chakula na usafiri zilikuwa kubwa, na nyumbani bado walimtegemea. Alianza kufanya biashara ndogondogo pembeni ya kazi yake ya ualimu. Ndipo safari yake ya ujasiriamali ilipoanza rasmi.
Alianza kwa kununua msitu wa miti huko Geita, aliwapa mafundi wachane mbao, lakini aligundua analipa gharama kubwa. Wazo likamjia, kwa nini asinunue mashine yake ya kuchana mbao?
Haikuwa rahisi kupata taarifa za mashine hiyo, kwani kila alipouliza aliambiwa maneno ya kukatisha tamaa au kukosa ushirikiano. Bahati ilimwangukia, alipofahamu jirani yake alikuwa akisafiri kwenda Nairobi kununua bidhaa, alimpiga picha mashine aliyokuwa akiitamani na kumuuliza kama angeweza kuipata. Jibu lilikuwa ndiyo.
Kwa kuunganisha faida ya biashara zake ndogondogo na fedha alizopata kutokana na mbao, alikusanya takribani Sh3.5 milioni. Alimkabidhi msafiri huyo Sh2 milioni, akiamini hatatapeliwa. Baada ya muda, mashine ilifika mikononi mwake, ndipo alipoanza rasmi safari ya kuwachania watu mbao vijijini.
Anasimulia jinsi alivyolala chini kwenye vibanda vya udongo, akila dagaa wasiotiwa hata chumvi au mafuta ilimradi amalize kazi. “Watu walishangaa nakula bila kulalamika, lakini nilikuwa na malengo. Nilijua hii ni hatua tu ya kupita,” anasema.
Alisimamia mafundi wa kuchana mbao, yeye akichukua Sh2,500 kwa kila ubao na kumpa fundi Sh800. Polepole akaona si lazima achane tu, anaweza pia kununua mbao na kuziuza mjini kwa faida zaidi. Mtaji ukaanza kukua.
Mwaka 2016 akaanzisha kampuni iitwayo Mando Women Group. Aliipa jina hilo kwa sababu aliamini katika nguvu ya wanawake kushirikiana. Walianza watatu—yeye, ndugu yake na mwanamke mwingine nje ya familia. Kampuni ilijikita katika kazi za leba kwenye miradi ya barabara kusafisha mitaro, kupalilia na kujenga madaraja madogo.
Fursa ilipotokea ya mmoja wao kusomeshwa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuongeza ujuzi, alimruhusu mwenzake aende kwa kuwa yeye bado alikuwa mwalimu. Hata hivyo, baada ya kurejea, mwenzake alianzisha kampuni yake na kumuacha. Ilikuwa pigo, lakini hakukata tamaa.
Majaribu makubwa yalikuja alipoomba zabuni ya kutengeneza madawati yenye thamani ya Sh177 milioni. Alipoipata, baadhi ya watu walianza kuhoji uwezo wake. “Walisema sina mtaji, siwezi kumaliza,” anakumbuka.
Alikopa mbao kutoka kwa wafanyabiashara aliowazoea, akakusanya magari mawili ya malighafi na kuanza kazi. “Nilinunua mbao nyingi nikijua nitafanyiwa fitina kwa sababu ni mgeni kwenye kazi na nimeshinda tenda,” anasema.
“Kweli kama nilivyowaza walikwenda mpaka kwa mkurugenzi kumwambia sitoweza hiyo kazi ni kubwa. Mkurugenzi akatoka na ofisa elimu na watu wengine wakaja kuangalia, wakakuta nina mbao nyingi pale na kazi inaendelea wakaridhika na kuondoka.”
Changamoto iliyobaki ilikuwa mabomba ya chuma (pipe) ambayo hakuwa nayo.
“Niliwaambia yanakuja kesho, ukweli ni kuwa sikuwa nimeagiza kwa sababu sikuwa na fedha ya kutosha,” anasema.
Alimfuata shemeji yake na kumweleza changamoto hiyo. Alikopeshwa Sh11 milioni na akanunua vifaa. “Nilikuwa nakamilisha sehemu ya kazi, nalipwa, naenda kununua vifaa vingine, naendelea hadi ilipokamilika. Nilipongezwa sana. Kuanzia hapo milango ya miradi mikubwa ikafunguka.”
Saqsa anafanya kazi na taasisi mbalimbali, zikiwamo halmashauri, Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Geita (Geuwasa) na Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Dhahabu ya Geita (GGM). Ana miradi Geita, Arusha na maeneo mengine, ikihusisha madawati, mitaro, barabara na kazi za chuma.
Anasema kuacha ualimu haikuwa uamuzi wa ghafla. Siku moja aligawanya mshahara wake wa Sh470,000 kwa siku 30, akabaini anabaki na takribani Sh10,000 kwa siku. “Nikajiuliza, hata nikifanya biashara ya nyanya naweza kupata zaidi ya hapa. Kwa nini nipoteze muda?”
Anasema kutokana na kujikita kwenye ujasiriamali mara kadhaa alikuwa akiitwa kazini, lakini hakwenda, aliogopa kusema anataka kuacha kazi mpaka baadaye alipoandikiwa barua ya kuachishwa kwa utoro, hapo ndipo safari yake ya ujasiriamali ilipoanza rasmi.
Kudharauliwa na kukatishwa tamaa
Anakumbuka siku moja wanaume wawili walimcheka hadharani wakisema anapoteza muda kuchana mbao. “Achana na hiyo kazi, huwezi kufika mbali, kuchana mbao siyo kazi rahisi kama unavyofikia,” anasema Nkwimba akikumbuka jinsi walivyomcheka kwa nguvu mbele za watu.
Anasema kabla hajaanza kufanya miradi mikubwa akiwa ameajiriwa mwanzoni alikuwa na mgahawa akiuza chakula na vinywaji.
“Hapa pia nilifanyiwa jambo ninalolikumbuka, mteja mmoja alikuja nikamuhudumia, sasa kuna mambo alikuwa ananiambia sikuwa nayapenda akakasirika, nilikuwa nimekaa alinimwagia soda kuanzia kichwani ikateremka mwili mzima.
“Niliumia, lakini sikuonesha hilo, nilimwambia asante nikajikung’uta na kuendelea na kazi,” anasema na kuongeza;
“Huwezi kuamini siku hizi nikikutana naye anabadili njia au anatazama pembeni kama hajaniona, ananiogopa ingawa nilimsamehe, kwani siku aliponimwagia soda nilijiapiza nitajitahidi ili niheshimiwe na wengine na aliyenimwagia soda pia.”
Kutimiza ndoto ya kuwezesha wengine
Licha ya kuwa na mafanikio makubwa ikiwamo kutimiza ndoto ya kufanya shughuli za usafirishaji kwa kumiliki malori ya semitrela mawili na kandarasi kubwa, bali pia kuwezesha wengine.
Anasema kupitia viwanda vya mbao, kuchomelea, maduka na usafirishaji ameajiri vijana 40.
“Nilipoanza mradi wa Sh177 milioni nilikuwa na chini ya Sh10 milioni. Kilichonitangulia ni uthubutu. Nilithubutu kwanza, fedha zikafuata,” anasema.
Anasema kwa kuwa alikuwa na ndoto ya kuona mbali tangu akiwa mwanafunzi, alianza kusaidia ndugu zake kupitia biashara alizokuwa akifanya.
“Nikiwa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT) nikisomea ualimu, kukatangazwa marufuku kuvaa suruali, nikaiona fursa kwa sababu wanafunzi wengi walikuwa na mavazi ya aina hiyo.
“Nikaanza kuuza mitumba. Nilikuwa nakwenda kununua kisha nakuja kuuza chuoni, hivyo nilianza kuhudumia wadogo zangu nikiwa nasoma. Pia nilikuwa nauza vitafunwa, karanga na vitu vidogo vidogo, ilimradi kila changamoto kwangu ilikuwa fursa. Nikajichanga na kufikisha Sh30 milioni,” anasema.
Anasema baadaye kaka yake mkubwa alimweleza kuhusu biashara ya mahindi kuyatoa Katavi na kuyauza Kahama, akimhakikishia kuwa inalipa. Kutokana na hilo, Nkwimba alimpa kaka yake Sh30 milioni kwa ajili ya kununua mzigo wa biashara hiyo, huku akiongeza Sh2 milioni za kwake, wakati yeye akiendelea na masomo.
“Baada ya hapo sikumuona tena ndiyo maana nilipoajiriwa sikuwa na kitu na nilianza upya,”anasema Nkwimba.
Nkwimba anawashauri wanawake kuwa na uthubutu, kwani alichojifunza wengi huwa na mawazo mazuri lakini hawayafanyii kazi.
“Sisi na wanaume waliokamatwa nyanja nyingi za maendeleo nchini kama siyo duniani tunatofautiana jinsia tu, lakini uwezo wa kufikiri ni sawa. Changamoto zisiwatese akili, ziwajenge.
“Biashara ni kama darasa la kwanza hadi la saba. Kadri unavyoendelea, ndivyo unavyoelewa zaidi. Muhimu ni kuanza na kuthubutu,” anasema.
Nkwimba alizaliwa mwaka 1987 mkoani Shinyanga. Alisoma Uhuru Sekondari Shinyanga, Mbezi Beach na kumalizia Tegeta High School, jijini Dar es Salaam, kisha Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine Mwanza, alikohitimu mwaka 2012.
Kwa sasa ni mama wa mtoto mmoja, akigawa muda wake kati ya familia na kazi.