Na Ruth Kyelula, Manyara
Mkoa wa Manyara unatarajia kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kimkoa tarehe 8 Machi 2026 katika Wilaya ya Simanjiro, huku Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Queen Sendiga, akitoa wito kwa jamii kuhakikisha haki za wanawake na wasichana zinalindwa na kuheshimiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari Machi 3, 2026 ofisini kwake mjini Babati, Sendiga alisema maadhimisho hayo ni fursa muhimu ya kuhamasisha jamii kushiriki katika juhudi za kukuza usawa wa kijinsia, kuwawezesha wanawake kiuchumi na kuimarisha ustawi wao katika jamii.
Alisema Mkoa wa Manyara umekuwa ukikabiliwa na changamoto ya matukio ya ukatili wa kijinsia, lakini juhudi mbalimbali zimeendelea kufanyika ili kukabiliana na tatizo hilo. Alisisitiza kuwa wazazi na jamii kwa ujumla wanapaswa kuhakikisha watoto, hususan wasichana, wanapata haki zao na kulindwa dhidi ya vitendo vya ukatili.
Sendiga alieleza kuwa chimbuko la Siku ya Wanawake Duniani linatokana na harakati za wanawake wafanyakazi waliopigania haki zao kazini, jambo linaloifanya siku hiyo kuwa jukwaa la kuhimiza uwajibikaji kwa wanawake pamoja na kuwakumbusha waajiri, taasisi na serikali kuhakikisha mazingira ya kazi yanazingatia usawa wa mishahara, maslahi na fursa.
Aliongeza kuwa Tanzania imekuwa ikiadhimisha siku hiyo tangu mwaka 1997 kwa lengo la kutambua mchango wa wanawake katika maendeleo ya taifa, huku kaulimbiu ya mwaka huu ikiwa ni “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana: Msingi Jumuishi kufikia Dira 2050.”