Sababu Lissu kuomba kuunganishwa kesi ya mali Chadema

Dar es Salaam. Mahakama Kuu imepanga kutoa uamuzi wa maombi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, kujumuishwa katika kesi ya madai ya mgawanyo usio sawa ndani ya chama hicho baina ya Bara na Zanzibar Machi 26, 2026.

Tarehe hiyo ya uamuzi wa maombi hayo imepangwa na Jaji Hamidu Mwanga anayesikiliza kesi leo Ijumaa, Machi 62026 baada ya kukamilisha usikilizwaji wa maombi hayo.

Kesi hiyo ya madai namba 8323 ya mwaka 2025, imefunguliwa na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Said Issa Mohamed na wajumbe wawili wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu.

‎Wadaiwa katika kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Hamidu Mwanga, Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, ni Bodi ya Wadhamini wa Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho.

Lissu amewasilisha maombi akiomba kuunganishwa kwenye kesi hiyo kama mdaawa wa lazima kwa kuwa ana masilahi katika kesi hiyo.

Wajibu maombi katika shauri hilo ni pamoja na wadai katika kesi ya msingi, yaani Said na wenzake kwa upande mmoja na Wadhamini wa Chadema na Katibu Mkuu ambao ni wadaiwa katika kesi ya msingi.

Wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo leo Ijumaa Machi 6, 2026, Lissu ametoa ufafanuzi wa sababu za kuomba kujumuishwa katika kesi hiyo.

Katika hoja zake, Lissu amesema yeye ni mtu muhimu kuwepo katika kesi hiyo, kwa kuwa ndiye mwenyekiti Taifa wa Chadema na kiongozi mkuu wa chama hicho, kufuatia uchaguzi wa ndani ya chama hicho uliofanyika Januari 21, 2025.

Lissu amesema amekuwa mwanachama wa chama hicho tangu Julai 2004 na katika kipindi chote hicho cha takribani miaka 21 ameshika nyadhifa mbalimbali za juu katika chama chake, kama vile Mkurugenzi wa Sheria, Mwanasheria Mkuu wa chama, Makamu Mwenyekiti wa chama Tanzania Bara.

Lissu amesema nje ya nyadhifa hizo, amekuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema tangu mwaka 2004 alipojiunga na chama.

 Hivyo, amesema kwa kushika nyadhifa zote hizo kwa kipindi cha miaka 21 ambayo amekuwa ndani ya chama, ameshiriki na anafahamu masuala yote makubwa na muhimu ambayo yameamuliwa na chama hicho.

“Mheshimiwa Jaji, nimeshiriki na nafahamu kila jambo ndani ya Chadema, iwe masuala ya muungano, iwe masuala ya Zanzibar yote,” amesema Lissu na kusisitiza:

“Na hao wajibu maombi wa kwanza (Mohamed); wa pili (Khamis) na wa tatu (Komu) ninawafahamu na nimefanya nao kazi kwa kipindi chote hicho isipokuwa wa pili ni mgeni mgeni, ila wengine ninawafahamu fika tena kwa kipindi kirefu.”

Amesema kwa nafasi yake kama Mwenyekiti wa chama Taifa, ndiye mwenyekiti wa vikao vyote vya uamuzi vya chama viwe vya kisera au vya utekelezaji, yaani Kamati Kuu, Baraza Kuu na Mkutano Mkuu wa Taifa.

Lissu amesema amelazimika kuieleza Mahakama hayo yote kwa kuwa ni muhimu kwa sababu shauri la msingi linazungumzia hayo, kuna sera za matendo ya kibaguzi, ukiukwaji wa sheria, maamuzi ya vikao vya chama ambavyo yeye mwombaji ndiye mwenyekiti wake.

Amesema shauri la msingi linahusu uongozi wake wa chama moja kwa moja, kwa sababu limefunguliwa mara tu baada ya kuwa mwenyekiti na siku nne tu baada ya kukamatwa na kufunguliwa kesi ya uhaini.

Amesisitiza kuwa kwa nafasi yake ya uenyekiti wa chama ndiye anategemewa kusimamia na kutekeleza uamuzi wowote utakaotolewa na Mahakama hiyo katika kesi hiyo, hata kama ni suala la mgawanyo wa mali.

Hivyo, amesema kuwa uamuzi wowote au amri ya mahakama dhidi ya mjibu maombi wa tano (Bodi ya Wadhamini Chadema) na wa tano (Katibu Mkuu Chadema) ambao ndio walalamikiwa katika kesi ya msingui utamuathiri yeye moja kwa moja.

“Mheshimiwa Jaji amri yoyote ambayo utaipitisha ambazo zimeombwa ukikubali maombi kwamba shughuli za chama zisimame maana yake ni kwamba mwenyekiti hatoweza kuongoza vikao ikiwemo mkutano mkuu,” amesema Lissu na kusisitiza:

“Hivyo ni moja kwa moja nitaathirika na uamuzi wowote, iwe hukumu, uamuzi au amri itakayotolewa, Mheshimiwa Jaji huo ndio ushahidi uliopo mbele yako uliotolewa kwa kiapo.”

Huku akiielekeza mahakama katika uamuzi wa Mahakama ya Rufani katika mashauri mbalimbali, Lissu amedai kwa ushahidi huo, ni wazi yeye kama mwombaji ni mdaawa wa lazima na haepukiki kuwepo kwenye kesi hiyo kwa kuwa ni mtu muhimu sana.

Ameongeza kuwa kwa ushahidi huo kwa mujibu wa Amri ya I kanuni ya II, mahakama inapaswa imujumuishe katika kesi hiyo kwa masharti ambayo itaona ni ya haki.

“Rai yangu kama mleta maombi ni kwamba, Mahakama hii iamuru kwamba mleta maombi aingizwe kwenye kesi. Kwa kuwa suala hili lina masilahi makubwa sana katika umma wa nchi hii basi uamuru kila upande ubebe gharama zake,” ameomba Lissu.

Wakijibu hoja za Lissu, mawakili Shaban Marijan na Alvin Fidelis wanaowawakilisha wajibu maombi, wamepinga hoja za Lissu wakiitaka mahakama isimruhusu aingizwe kwenye kesi hiyo.

‎Wakili Marijan amedai Lissu hana sifa za kuunganishwa katika kesi hiyo kwa kuwa maombi yake ameyawasilisha kwa namna isiyo faa, yaani kama mtu binafsi na si kama mwenyekiti, hivyo hana masilahi katika kesi hiyo.

‎Kuhusu hoja ya Lissu kuwa kesi hiyo imefunguliwa kwa ajili yake baada ya kuwa mwenyekiti, Marijani amedai si sahihi kwa kuwa mambo ambayo wateja wao wanayalalamikia kama yalivyobainishwa katika kiapo chao kinzani, ni ya tangu mwaka 2016.

Jaji Mwanga baada ya kusikiliza hoja za pande zote, amepanga kutoa uamuzi Machi 26, mwaka huu ambao ndio utakaotoa hatima ya Lissu kuruhusiwa au kukataliwa kuingia katika kesi hiyo, kwa sababu ambazo mahakama itazitoa.

‎Katika kesi ya msingi, wadai wanadai kuwa  kumekuwa na  mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Zanzibar na Tanzania Bara, kinyume na Sheria ya Vyama vya Siasa na Katiba ya chama hicho.

‎Pia wanadai kuna ubaguzi wa kidini na kijinsia; pamoja na kutoa maoni na matamko yaliyo na nia ya kuvuruga muungano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hivyo wanaomba Mahakama hiyo itamke kuwa wadaiwa wamekiuka kifungu cha 6A(1), (2), (5) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 Marejeo ya mwaka 2019 na iwaelekeze wazingatie kifungu hicho.

Pia, wanaiomba Mahakama hiyo itamke kwamba ugawaji wa fedha, mali na rasilimali kwa ajili ya shughuli za kisiasa na kiutawala kati ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar unaofanywa na wadaiwa ni kinyume cha sheria na ni batili.

Vilevile wanaomba mahakama isitishe kwa muda shughuli zote za kisiasa mpaka maagizo ya Mahakama yatakapotekelezwa, na zuio la kudumu dhidi ya matumizi ya mali, fedha na rasilimali za chama hadi walalamikiwa watakapotekeleza matakwa ya sheria husika na gharama za kesi.