Moshi. Shahidi wa pili wa upande wa Jamhuri katika kesi ya makosa ya kimtandao inayomkabili Mchungaji Godfrey Malisa, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi jinsi alivyoenda kupekua nyumbani kwa Malisa na kukusanya vielelezo vinne ambavyo ni simu, kompyuta (laptop) mbili pamoja na chaja moja ya laptop.
Shahidi huyo, Mkaguzi wa Polisi, Nickson Mwamnyasi wa Kituo cha Polisi Majengo, ameeleza kuwa mchakato huo wakati alipokuwa akitoa ushahidi wake katika kesi hiyo Machi 6, 2026.
Katika kesi hiyo, Malisa anatuhumiwa kuchapisha taarifa kwenye mtandao wake wa YouTube, akidai Rais Samia Suluhu Hassan anatakiwa kujiuzulu kwa kusimamia mauaji ya maelfu ya Watanzania.
Katika kosa la kwanza, upande wa mashtaka unadai kuwa Mchungaji Malisa alitenda kosa hilo Novemba 15, 2025 huko Miembeni, Wilaya ya Moshi na alichapisha maneno hayo katika akaunti ya YouTube yenye jina Godfrey Malisa.
Hati ya mashtaka inanukuu maneno aliyoyachapisha kuwa: “Samia Suluhu Hassan anatakiwa kujiuzulu mara moja kwa kuwa amekuwa ni Rais aliyesimamia mauaji ya maelfu ya Watanzania.”
Upande wa Jamhuri unadai alichapisha maneno hayo akijua fika kuwa taarifa hizo hazikuwa sahihi na zilikuwa na lengo la kupotosha umma wa Watanzania.
Katika kosa la pili, Malisa anatuhumiwa kufanya uchochezi kinyume na kifungu cha 35 cha Kanuni ya Adhabu sura ya 16 kama kilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023.
Maelezo ya kosa ni kuwa Novemba 15, 2025 huko Miembeni, Wilaya ya Moshi, anadaiwa kuchochea umma wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutenda kosa la jinai ambalo ni kufanya mkusanyiko usio halali kinyume cha sheria.
Jana, Jamhuri iliwakilishwa na mawakili wawili wa huku utetezi ukiwakilishwa na Wakili Deogratias Matata.
Katika ushahidi wake, shahidi huyo aliieleza Mahakama kuwa ana uzoefu wa miaka 18 kazini ambapo miongoni mwa majukumu yake ni kufanya doria, kukamata watuhumiwa na kufanya upekuzi kwenye matukio mbalimbali.
Alidai Novemba 19, 2025, akiwa doria usiku, alipigiwa simu na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO) na kumtaka afike Kituo Kikuu cha Polisi kwani kuna kazi anapaswa kwenda kuifanya.
Amedai kuwa baada ya kupokea maelekezo hayo alienda kuchukua hati ya upekuzi kwa askari mwingine, kisha akaondoka na mtuhumiwa (Malisa), ambaye alikuwa anakabiliwa na tuhuma za kuhamasisha maandamano kwa njia ya mtandao.
Ameeeleza kuwa aliondoka na mshtakiwa na askari wengine hadi nyumbani kwa mshtakiwa eneo la Majengo mjini Moshi na kuwa walipofika waliegesha gari nje ya geti na yeye akaenda kumtafuta balozi na mwenyekiti wa mtaa huo ili wakashuhudie upekuzi huo.
“Nilikuja nao hadi nje tulipokuwa tumepaki gari na Mzee Malisa alipowaona alithibitisha kuwatambua kama viongozi wa eneo hilo. Nikamuomba akafungua geti la nyumba yake na kabla sijaingia ndani nilimuomba anipekue, akafanya hivyo na kuona sina chochote, tukaingia ndani,” ameeleza shahidi.
“Katika upekuzi huo, nilikuta laptop mbili moja ni aina ya HP, rangi ya kijivu na nyingine ni nyeusi aina ya e-mashine, simu moja aina ya Infinix pamoja na chaja nyeusi moja ya laptop, nikajaza hati na kumkabidhi mshtakiwa asome kama vitu nilivyoandika ndivyo vyenyewe, akasaini na mashahidi huru wakasaini tukaondoka.”
Alidai kuwa walimchukua mshtakiwa na vielelezo hivyo ambavyo viliwekwa kwenye bahasha za kaki na kubandikwa karatasi nyeupe kwa juu na kuwa vielelezo hivyo vilikuwa na kesi namba Moshi/IR/6544/2025, vikiwa na jina lake aliyevikamata, jina la mshtakiwa (Malisa) ambapo pia mahakamani hapo alivitambua vielelezo hivyo na mshtakiwa pia.
Baada ya kumaliza ushahidi wake wa msingi, shahidi huyo aliulizwa maswali ya dodoso kutoka kwa wakili wa utetezi ambapo kutokana na mahojiano hayo shahidi huyo alieleza mahakama kuwa hafahamu iwapo kunapaswa kutolewa kibali maalumu cha kupekua mshtakiwa usiku.
Amesema utaratibu anaoufahamu ni kuwa askari mwenye cheo kuanzia cha mkaguzi anaweza kwenda kupekua kwa mshtakiwa usiku ila hafahamu kama kuna kibali cha mahakama kinachotolewa kwa ajili hiyo.
Amedai kuwa upekuzi huo uliofanyika saa 4 usiku na kuwa licha ya kutambua vielelezo hivyo mahakamani, hafahamu namba ya utambulisho wa simu (Imei) wala IP adress ya kompyuta mpakato alivyokamata.
Mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi, Ally Mkama, shahidi huyo ameieleza Mahakama kuwa wakati wote wa upekuzi katika nyumba hiyo, alikuwa na Malisa pia.
Baada ya shahidi huyo kumaliza kutoa ushahidi wake, Hakimu Mkama aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 18, 2026 itakapoendelea kusikilizwa ambapo upande wa Jamhuri umeieleza Mahakama kuwa watakuwa na mashahidi wanne.
Mbali na kesi hiyo, Mchungaji Malisa anakabiliwa na kesi ya uhaini chini ya kifungu 39(2)(d) cha Kanuni ya Adhabu sura ya 16 kama kilivyofanyiwa marejeo na Bunge mwaka 2023, akituhumiwa kuhamasisha mkusanyiko usio halali.
Februari 10, 2025, Mchungaji Malisa alifukuzwa uanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) baada ya kupinga uamuzi wa mkutano mkuu wa CCM uliomteua Rais Samia kuwa mgombea urais.
Uamuzi wa kumfukuza uanachama ulitangazwa na Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Merce Mollel, akiegemea uamuzi ya Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kilimanjaro iliyomuondolea sifa ya kuendelea kuwa mwanachama.
“Malisa amefukuzwa kutokana na kukosa sifa za kuendelea kuwa mwanachama kwa sababu mara kwa mara amekuwa akibeza uamuzi halali uliofanywa na mkutano mkuu wa CCM taifa uliofanyika Januari 19, 2025,” alieleza Mollel.
Katibu huyo alinukuliwa akidai Malisa amekuwa akitoa matamko ambayo hayaleti umoja na mshikamano ndani ya chama na nchi kutokana na kudai mkutano huo uliomteua Samia kuwa mgombea pekee ulivunja katiba ya chama, jambo ambalo si la kweli.
Pamoja na kufukuzwa uanachama, bado aliendelea kupinga uteuzi huo kwa kujaribu kufungua kesi mahakamani ambazo hata hivyo hakufanikiwa, ndipo alihamia katika mitandao ya kijamii akiendelea kupinga uteuzi huo.