SWAHILI: ICEA LION Yazindua Simba Wa Bima, Ikisisitiza Ulinzi Katika Kila Hatua ya Maisha

Mkurugenzi wa Matekelezo na Huduma za Uthaminishaji wa TIRA, Alex Rocky (mwenye skafu) aliyemuawakilisha Kamishna wa TIRA, Dk. Baghayo Saqware akipokea zawadi kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya kampuni ya bima ya ICEA Lion Group, James Ndegwa (kushoto) ikiwa ni  uzinduzi wa kampeni ya Simba Wa Bima inayolenga   kujua umuhimu wa   kulinda familia, kupanga maisha baada ya kustaafu na kukuza biashara kwa kutumia bima. Kulia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa ICEA Lion, Jared Awando. Hafla ya uzinduzi huo ilifanyika  jijini Dar es salaam kwa kufuturisha  wadau wa bima nchini.

Dar es Salaam, Tanzania | Jumatatu, 2 Machi 2026

Katika hatua ya kuleta mapinduzi kwenye sekta ya bima nchini, kampuni ya ICEA LION inazindua Simba Wa Bima, kampeni inayolenga kuiweka kampuni hii kama mshirika anayesimama na Watanzania katika kila hatua muhimu ya maisha.

Uzinduzi huo unafanyika jioni ya Jumatatu tarehe 2 Machi 2026, Serena Hotel Marquee, ukihudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya bima, viongozi wa serikali, washirika wa biashara pamoja na vyombo vya habari. Mgeni rasmi katika tukio hilo atakuwa Dr. Baghayo Saqware, Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), kudhirisha umuhimu wa kampeni hii kwa sekta ya bima na uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Simba Wa Bima ni zaidi ya kampeni; ni mtazamo unaoakisi nguvu, umakini na fahari inayowakilishwa na alama ya simba. Kampeni hii inalenga kuwakumbusha Watanzania kuwa iwe ni kuanzisha familia, kukuza biashara, au kupanga maisha ya kustaafu, ICEA LION inatembea pamoja nao katika kila hatua.

Akizungumzia uzinduzi huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa ICEA LION, Jared Awando, anasema kampeni hii inaonyesha uelewa wa kina wa maana halisi ya ulinzi katika maisha ya watu. “Maisha yana hatua mbalimbali. Kuanzia elimu na kazi, hadi kuanzisha familia, biashara, na hatimaye kustaafu – kila hatua inakuja na fursa pamoja na majukumu yake,” anasema Awando. “Wakati watu wanafanya mipango ya maisha yao, bima inawapa ujasiri wa kusonga mbele kwa amani. Kupitia Simba Wa Bima, ICEA LION inathibitisha nafasi yake kama mshirika anayesimama na Watanzania katika kila hatua ya safari ya maisha.”

Tangu ilipoingia katika soko la Tanzania mwaka 1999, ICEA LION imejizolea sifa kwa uadilifu na kutoa kipaumbele kwa mteja. Kupitia huduma mbalimbali kama bima za magari, afya na mali, kampuni imeendelea kuongoza nchini, na kampeni hii mpya ni mwendelezo wa miaka 25 ya huduma bora iliyojengwa juu ya misingi ya kuaminika kwa watu wa Tanzania.

Kwa kuheshimu mwezi huu mtukufu, ICEA LION imeandaa hafla ya Futari kwa wageni wake waalikwa. Hafla hiyo itakuwa msingi wa utambulisho rasmi wa Simba Wa Bima, ikiashiria kuanza kwa sura mpya ya ulinzi wa uhakika sambamba na ahadi ya ICEA LION ya kuendelea kusimama na Watanzania katika kila hatua ya maisha.