Falsafa ya “Anarchism” ni somo kwenye sayansi ya siasa. Waumini wa Anarchism (anarchists) hujengwa na mtazamo kuwa Serikali ni kikundi cha kijambazi, maana hujiendesha kwa mabavu, hukusanya mapato kwa raia (kutoza kodi) bila utashi, na hudhibiti dola kwa nguvu za kijeshi.
Serikali ni kikundi cha kijambazi kilichohalishwa, hiyo ndiyo tofauti yake na majambazi wa kawaida. Mwanafalsafa wa Ufaransa, Pierre-Joseph Proudhon, ndiye alileta nadharia hii, na ulimwengu ukamtambua kama “Baba wa Anarchism.”
Ukiifahamu nadharia ya Anarchism, utaona umuhimu wa Serikali kuendeshwa na watu waadilifu, makini, wenye ubinadamu na wazalendo.
Vinginevyo, jambazi anaposhika Serikali, ujambazi lazima utatamalaki. Inakuwa sawa na nadharia ya “Stationary Bandit”, kama ilivyoanzishwa na mwanazuoni wa Marekani, Mancur Olson, alipojenga taswira ya haramia kushika mamlaka.
Dunia inashuhudia mapigano, watu wanapoteza maisha, miundombinu inaharibiwa, na wananchi wanakosa makazi. Nyuma ya kadhia hiyo kuna wahalifu wawili wanaoongoza Serikali–Donald Trump na Benjamin Netanyahu.
Trump ni mhalifu. Mei 30, 2024, Mahakama Kuu ya Jimbo la New York, Marekani, ilimkuta Trump na hatia ya makosa 34 makubwa Marekani, yenye kuhusu matumizi ya fedha chafu, udanganyifu wa biashara, ukwepaji kodi na rushwa.
Ndani ya mahakama ilithibitika kuwa Trump si mtu mwenye maadili ya kijamii, kwani alijamiiana na mwanamke mcheza filamu za ngono, Stormy Daniels, akiwa ni mume na baba wa familia.
“Ikulu ni mahali patakatifu,” alisema Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, akimaanisha urais unamfaa mtu adili. Alisema pia wakati mwingine, “Uongozi ni kazi ya wananchi.
“Huwezi kufanya kazi ya wananchi halafu ukawa unahangaika na wanawake wa barabarani. Ukitaka uongozi lazima ujiheshimu.”
Kwa nini Trump ni Rais badala ya kuwa jela? Jibu la swali hilo ni kipimo cha udhaifu mkubwa wa mifumo ya kisheria na matundu ya demokrasia ya Marekani. Trump anajua kucheza na mifumo ya kisheria, na kupitia mizunguko yake anayoicheza, sasa hivi ni bilionea, mali nyingi akinyakua kutoka kwa watu wengine.
Trump anayajua matundu ya demokrasia ya Marekani, kiasi hata mhalifu anaweza kuwa Rais, kazi namba moja ya nchi.
Novemba 21, 2024, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), iliyopo The Hague, Uholanzi, ilitoa hati ya kukamatwa kwa Netanyahu kwa makosa ya uhalifu aliyoyatenda dhidi ya binadamu, kuanzia Oktoba 8, 2023 mpaka Mei 20, 2024. Pamoja na Netanyahu, mwingine anayetakiwa kukamatwa ni aliyekuwa Waziri wa Ulinzi wa Israel, Yoav Gallant.
Sasa, watu hao wawili ambao wasifu wao upo dhahiri, walianzisha mashambulizi dhidi ya Iran na kumuua aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa Iran (Rahbar), Ayatollah Ali Khamenei. Kisha wanajisifu kuwa wamemuua mtu hatari zaidi duniani.
Watu wawili ambao, kama mifumo ya sheria na haki ingekuwa sawa na yenye kuongozwa na misingi, wangepaswa kuwa jela. Wanamshambulia mtu akiwa ofisini kwake, akiwa hajaanzisha shambulizi lolote, halafu wanajisifu kumuua mwovu wa dunia.
Ori Goldberg ni mwanazuoni mbobevu wa masuala ya Mashariki ya Kati. Ni raia wa Israel, mkazi wa Tel Aviv, na mtunukiwa wa shahada ya uzamivu (PhD) ya Masomo ya Mashariki ya Kati kutoka Chuo Kikuu cha Reichman, kilichopo Herzliya, Israel.
Profesa Ori, katika andiko lake kwenye mtandao wa Al Jazeera lenye kichwa, “Maslahi ya Marekani na Israel hivi karibuni yanaweza kutofautiana kuhusu Iran,” anaeleza kuwa mashambulizi ya Marekani na Israel kwa Iran yalianzishwa kwa matamanio ya muda mfupi.
Ndani ya andiko hilo, Profesa Ori anaeleza kuwa si kwamba Trump na Netanyahu wanaaminiana, kila mmoja ana jicho la mashaka dhidi ya mwenzake, lakini imewalazimu kukubaliana kuanzisha vita ili wapate nusura ambayo kila mmoja wao anaitafuta.
Trump anamtegemea Netanyahu kwa uchokozi wake wa kivita. Netanyahu anamtumainia Trump kwa nguvu za kijeshi za Marekani.
Faida inayolengwa kwa kila mmoja ni nini? Netanyahu anaunda matukio ya kivita ili kuchelewesha mjadala wa uwezo wake wa kiuongozi baada ya kampeni zake za kijeshi Gaza na Ukanda wa Magharibi, Palestina, kufeli. Wakati huohuo, mauaji ya halaiki ya Wapalestina yanaendelea.
Lazima Netanyahu atafute kondoo wa kafara. Iran wamegoma kuwa kondoo wa kafara. Hali ni mbaya.
Mtazamo wa Profesa Ori unalandana na wa Rais wa 42 wa Marekani, Bill Clinton, aliyesema kuwa Netanyahu huanzisha chokochoko za vita ili aendelee kubaki madarakani.
Msingi wa hoja ni kwamba Israel isipokuwa vitani, Netanyahu atakabiliana na upinzani wa kisiasa, hivyo kuondolewa mara moja.
Upande wa Trump, anataka vita ili kujinasua kwenye bomu lenye kila dalili ya kumlipukia katika siku za usoni. Bomu hilo ni kashfa ya Mafaili ya Epstein. Wamarekani wengi wanamtazama Trump kama mhusika, na mmoja wa wahalifu wa kingono walioshirikiana na mhalifu wa kingono kwa mabinti wadogo, Jeffrey Epstein, ambaye amefariki dunia.
Uthubutu mkubwa wa kuingia Venezuela na kumnyakua aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Nicolas Maduro, na ushujaa wote ambao Trump alijivalisha kuwa amemkata “kigogo wa genge kubwa la wauza dawa za kulevya”, haukufifisha Mafaili ya Epstein. Hata sasa ni kama watu wameshasahau kuwa Maduro alikamatwa. Trump akaona afanye jipya, kumuua Ayatollah Khamenei.
Kuna nyimbo mbili zinaimbwa na waimbaji wawili walioamua kuizuga dunia kuwa wao ndiyo watetezi wa usalama na amani ya ulimwengu—Trump na Netanyahu. Wakati Trump wimbo wake ni mabadiliko ya uongozi Iran kwa usalama wa Marekani, Netanyahu anataka anguko la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akidai mafanikio yake yataipa sura bora Mashariki ya Kati.
Nyimbo hizo za Trump na Netanyahu zinaimbwa kwenye ala moja, vita! Wapenda vita wawili waliounda upacha usio mtakatifu wanaamini kuwa heri damu imwagike, vifo vizagae, na uharibifu wa miji utokee, lakini kile kilicho ndani ya akili zao na utashi wao kitimie.
Sadaka ambayo wanaitoa kupitia damu za watu ni kubwa. Nusura yao ni ushindi. Jinsi Iran inavyojibu mapigo kwa kuishambulia Israel na nchi jirani zenye kambi za kijeshi za Marekani, ni dhahiri ushindi hautakuwa jambo jepesi wala linaloweza kutokea hivi karibuni.
Uamuzi wa Trump uliundwa na kamari kwamba baada ya kuuawa kwa Ayatollah Khamenei, wananchi wangeingia barabarani na kuuangusha utawala.
Kinyume chake, maelfu ya Wairan walimiminika barabarani kwa majonzi wakimlilia kiongozi huyo, na kuimba nyimbo za kumtakia maisha ya peponi, wakisema amekufa shahidi, yaani mauti yalimkuta akisimamia haki.
Wairan pia waliimba na kupaza sauti kutaka mshikamano na kutoa shinikizo kwa Serikali kuwa lazima kisasi kilipwe, na hakuna kuomba msamaha wala kurudi nyuma ili kumtendea haki Ayatollah Khamenei aliyekufa shahidi.
Wakati huohuo, maofisa usalama wastaafu wa Marekani wameeleza kosa kubwa ambalo nchi hiyo imefanya ni kumuua Khamenei.
Larry Johnson ni ofisa wa zamani wa Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA), kitengo cha uchambuzi. Pia alikuwa mtumishi wa makao makuu ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, Idara ya Kupambana na Ugaidi.
Baada ya kifo cha Khamenei, Johnson amesema Marekani imemuua mtu ambaye kwa miaka 36 alizuia Iran isimiliki silaha za nyuklia.
“Mtu mmoja ndani ya Iran alizuia kwa miaka 36 Iran isiwe na uwezo wa kutengeneza silaha za nyuklia. Mtu ambaye alisimama na kusema Iran haitakuwa na silaha za nyuklia ndiye mtu ambaye Marekani imemuua. Miaka 36 iliyopita Ayatollah Khamenei alitakiwa kutoa ruhusa kwa Iran kutengeneza silaha za nyuklia, alikataa, alisema huo ni uovu, na huyo ndiye Marekani imemuua,” amesema Johnson.
Ofisa wa zamani wa Jeshi la Marekani, Scott Ritter, ameelezea kitendo cha kumuua Ayatollah Khamenei kuwa sawa na Wakatoliki kumuua Papa.
“Trump hajui Shia ni nini? Hajui Vita ya Karbala, hajui Husayn bin Ali (mjukuu wa Mtume Muhammad S.A.W). Anaharibu jina la Ayatollah Khamenei; hajui kuwa Khamenei ni sawa na Papa kwa Wakatoliki,” amesema Ritter.
Kurejea hoja ya Marekani kumuua Ayatollah Khamenei kama lengo la kulinda usalama wa Wamarekani, kuna mtu anajiuliza: Wamarekani wanalindwa ndani ya ardhi ya Iran? Lini Jeshi la Iran limewahi kuvamia mji wowote wa Marekani na kuua au kutishia uhai wa Wamarekani?
Trump alisema pia kuwa walianzisha mashambulizi kwa kuhofia wangechelewa, Iran wangeanza. Swali ni moja, ni lini Iran ilianza vita dhidi ya nchi nyingine? Tangu Mapinduzi ya Iran mwaka 1979, historia inaonesha Iran huvamiwa, kisha ndiyo hujibu mapigo.
Kuanzia uvamizi wa Iraq chini ya Saddam Hussein mwaka 1980, mpaka mapigo ya makombora na kuuawa kwa viongozi wake.
Usiku wa Alhamisi (Juni 12, 2025), kuamkia Juni 13 (Ijumaa), Israel iliishambulia Iran, shabaha ikawa maeneo ya kijeshi na serikali. Mashambulizi hayo ya Israel yakaua viongozi wengi waandamizi wa jeshi, akiwemo Mkuu wa Jeshi la Kimapinduzi (IRGC), Hossein Salami, na aliyekuwa Mnadhimu wa Jeshi la Iran, Mohammad Bagheri.
Mashuhuri wa nyuklia nchini Iran nao waliuawa. Ikawa mwanzo wa vita ya siku 12.
Juni 22, 2025, Marekani waliratibu oparesheni waliyoiita ‘Operation Midnight Hammer’. Trump akadai walifanikiwa kuharibu mitambo ya nyuklia ya Iran. Netanyahu alisema waliishambulia Iran kwa kushitukiza ili kuuwahi mpango wa nchi hiyo wa kutengeneza mabomu ya nyuklia.
Kuna mtu anajiuliza leo, ikiwa Juni 2025 Trump na Netanyahu walitamba kuwa wamesambaratisha mitambo ya nyuklia ya Iran, je, mashambulizi mapya ya nini hadi kumuua Ayatollah Khamenei?
Inafahamika Iran inaunga mkono vikosi vinavyopambana na Israel kuanzia Hezbollah, Lebanon, mpaka Hamas, Palestina.
Wakati Israel imekuwa mkono wa kulia wa kikundi cha People’s Mujahedin of Iran, ambacho itikadi yake inakinzana na mamlaka za Tehran (Iran).
Hapa ngoma sare. Sasa kwa nini ionekane Iran ndiyo watu hatari, halafu Israel na Marekani malaika?
Januari 3, 2020, Marekani walimuua Jenerali wa Iran, Qasem Soleimani, jijini Baghdad, Iraq, kwa shambulizi lililoamriwa na Trump. Halafu kifo cha aliyekuwa mwanasayansi mkuu wa Iran, Mohsen Fakhrizadeh, ambaye msafara wake ulishambuliwa jirani na Tehran, kisha akauawa na walinzi wake Novemba 27, 2020.
Ongezea kuuawa kwa aliyekuwa Kiongozi wa Hamas, Ismail Haniyeh, Julai 31, 2024, mjini Tehran.
Historia ipo dhahiri kuwa Iran ndiyo hushambuliwa. Sasa hiyo hofu ya Trump kuwa Iran ingeanzisha mashambulizi ilitokea wapi?