Upangishaji wa vizimba wachochea masoko kuwa wazi

Dar es Salaam. Licha ya Serikali kutumia fedha nyingi kujenga masoko ya kisasa, likiwamo Soko Kuu la Kariakoo, bado baadhi ya vizimba na maduka yameendelea kuwa matupu.

Kutokana na hali hiyo, uongozi wa soko hilo umetangaza kuwa vizimba ambavyo wamiliki wake hawatavifanyia biashara ndani ya kipindi cha miezi mitatu vitapigwa mnada.

Hoja hiyo imekuja baada ya ufunguzi wa Soko Kuu la Kariakoo lililofunguliwa rasmi Februari 8, 2026 na Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kukamilika kwa ukarabati wake na kugharimu Sh28 bilioni.

Soko hilo liliungua moto mwaka 2021 na kusababisha wafanyabiashara zaidi ya 1,500 kuhamishiwa katika masoko mengine ambayo ni Machinga Complex na Kisutu.

Siku ya uzinduzi zaidi ya asilimia 80 ya wafanyabiashara walirejeshwa sokoni kwa kupatiwa vizimba na maduka, hadi sasa si wafanyabiashara wote wameshafungua biashara zao.

Gazeti hili lilifanya uchunguzi katika Soko Kuu la Kariakoo, lililofunguliwa mwezi mmoja uliopita na kubaini kuwa sehemu nyingi bado hazina wafanyabiashara.

Hata hivyo, baadhi ya wafanyabiashara leo Alhamisi Machi 5, 2026 wameeleza sababu mbalimbali zinazochangia hali hiyo.

Mfanyabiashara katika soko hilo, Sandra Adam amesema vizimba vilivyowazi si kwamba havina watu bali wanasubiri wateja wa kuwapangisha kwa gharama ya juu.

“Vizimba vyote vina watu na wenyewe wapo katika masoko ambako tulipelekwa awali, kwa kuwa huko wamepata wateja huku kwingine wanashikilia kwa ajili ya kuwapangisha wengine kwa gharama ya juu,”amesema Sandra.

Amesema watu wanaofika katika soko hilo wanaelezwa kuwa nafasi zimejaa, lakini wakizunguka wanakuta maduka yamefungwa na vizimba havina watu.

Sandra amesema kulikuwa na kilio kikubwa cha kufunguliwa kwa soko na watu wakilalamika kuhujumiwa kwa kutolewa majina yao, ni mwezi unaelekea lakini wenye vizimba hawapangi bidhaa.

“Mtu ambaye alilalamika muda mrefu kuhusu upatikanaji wa vizimba leo hii hana muda wa kuja kuweka bidhaa zake, huu ni uhujumu uchumi kama inawezekana Serikali itoe muda kwa wasiofika sokoni,”amesema.

Mfanyabiashara mwenye kizimba Soko la Kariakoo, Habibu Pazi amesema wameshindwa kwenda na vizimba vyao kwa sababu waliambiwa wasubiri.

 “Sisi wa viungo na nafaka tuliambiwa tusubiri vizimba vyetu bado havijakamilika ambavyo vipo ghorofa ya tatu kwa hiyo hatuna haraka siku wakituambia twende tutafanya hivyo,”amesema Pazi.

Amesema tayari wameshapewa kila kitu ikiwano kumbukumbu namba za malipo,  kilichobaki ni wao kwenda kwenye vizimba kwa kupata ruhusa kwa eneo lao, ndiyo maana wameendelea kubaki Machinga.

Kwa upande wake, mfanyabiashara wa pembejeo Shukuru Shembojo amesema katika maeneo ambayo walikuwa awali katika Soko la Kariakoo hawajapata muafaka na kujikuta wakibaki njia panda.

“Sisi tulikuwepo Kariakoo ndani, eneo la chini kwa ajili ya shughuli za kilimo lakini leo hii, lile eneo unakuta biashara ya nguo hapo ni kuwachanganya wateja,”amesema.

Amesema wapo ambao wamechukua fremu za maduka na kuamua kuzipangisha kwa watu wengi kwa kuwa hawajawapa utaratibu mtu anaweka bidhaa yoyote.

Kwa mfanyabiashara katika Jengo la Machinga Complex, Maduhu Maganga amesema masoko yanayojengwa kubaki wazi kunatokana na utaratibu uliopo wa wafanyabiashara kupangisha wengine kwa bei ya juu.

Akitolea mfano Machinga Complex, amesema wapo wafanyabiashara waliochukua vizimba na kuwapangishia watu wengine kwa kodi ya Sh50,000 wakati kodi halisi ni Sh20,000.

“Hapa waliofanya hivyo wamesaidia kuongeza watu japokuwa awali ilikuwa ni changamoto na hatukuwa na uhakika wa wateja, lakini tulikaa na uongozi na kukubaliana kila ghorofa iwe na bidhaa yake ambayo haitaingiliana na wengine,”amesema.

Maganga amesema ongezeko hilo limetokana na makubaliano yaliyowekwa na uongozi wa jengo kuhusu mpangilio wa biashara katika kila ghorofa.

Vizimba kumilikiwa na ‘wazito’

Kuhusu hoja ya vizimba kumilikiwa na watu wakubwa wasiokuwa wafanyabiashara, Philibert Mosha mfanyabiashara katika Soko la Kariakoo, ameielezea hoja hiyo kwa kutoa mfano wa soko hilo.

Amesema soko hilo si kwamba wafanyabiashara wanasuasua kwenda kufanya biashara, bali vizimba vingi vinamilikiwa na watu wenye uwezo mkubwa, na ili kuvipata ni lazima kulipa gharama kubwa; hali inayosababisha sehemu nyingi za soko hilo kukosa wafanyabiashara.

“Sehemu nyingi za soko hili hakuna watu, isipokuwa madalali wanaotafuta wapangaji watakaofikia bei wanayotaka. Hata ukipanga kwa mwezi, nao wanataka ulipie sehemu yao bila kujali kwamba, tayari unalipa kwa uongozi wa soko,” amesema.

Amesema hali hiyo ndiyo inayochelewesha watu wengi kuanza kufanya biashara katika soko hilo. Ameeleza kuwa, hata mamlaka zikifanya ufuatiliaji, wengi wanaofanya biashara humo si wale wanaotambuliwa rasmi na uongozi wa soko.

Amesema hali hiyo ndiyo inayoleta tofauti kati ya masoko hayo na majengo ya watu binafsi, ambako taratibu huwa wazi na hakuna madalali wengi.

Said Miraji, mfanyabiashara anayefanyia biashara eneo lisilo rasmi, amesema kuna viongozi wanaonufaika moja kwa moja na wao kufanya biashara katika maeneo yasiyo rasmi kwa kupita kukusanya ushuru kila uchwao.

“Wanaofanya hivyo ni viongozi wakubwa na wanahusika moja kwa moja katika vyombo vya uamuzi. Wanaona tukifanya biashara katika maeneo rasmi hawatanufaika kwa sababu, fedha hupitia kwenye mifumo rasmi, hivyo wanaona bora tufanye biashara katika maeneo mbalimbali ili nao wanufaike,” amesema.

Miraji ameongeza kuwa mara nyingi kumekuwa na operesheni za kuwaondoa wamachinga, lakini hazidumu kwa muda mrefu. Amehoji iwapo sababu yake si baadhi ya wanaofanya maamuzi kunufaika na hali hiyo.

Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko Kariakoo, Ashiraf Abdulkarim amekanusha madai kuwa vizimba vya soko hilo vinamilikiwa na watu ambao si wafanyabiashara.

“Maeneo yale tulitangaza kupitia mfumo wa mtandao na tumewapa muda wa mwezi mmoja unaoisha mwishoni mwa mwezi huu. Ikiwa hawatayaendeleza, watapewa notisi tatu kabla ya kutangazwa tena kuuzwa kupitia mfumo wa mtandao,” amesema.

Amesema iwapo baada ya kupewa notisi hizo tatu maeneo hayo hayatakuwa yameendelezwa, nafasi zitakazokuwa wazi zitatangazwa tena kupitia mfumo wa mtandao kwa wanaohitaji.

“Baadhi ya vizimba katika soko hili watu wamejaa kwa sababu havikuwa na matengenezo yoyote, na wengi wao ni wale waliokuwa wanapanga bidhaa zao barabarani kama nyanya,” amesema.

Katika maelezo yake, Ashiraf amefafanua kuwa, hali hiyo ni tofauti na wamiliki wa maduka, kwa mfano wauzaji wa simu, ambao hawakujua soko litafunguliwa lini; lakini baada ya kufunguliwa wanaendelea na maandalizi ya kufungua biashara zao.

“Kufanya matengenezo ya maduka yao kunagharimu si chini ya Sh3 milioni. Kuna wanaohitaji kuweka nembo (logo), rangi wanazotaka kupamba, pamoja na meza za kuzunguka. Katika Soko la Kariakoo, asilimia 80 wanatakiwa kurudi sokoni na asilimia 20 iliyobaki ni wapya,” amesema.

Amesema si sahihi kusema waliopatiwa maeneo hayo si wafanyabiashara, akieleza kuwa asilimia kubwa walikuwepo tayari. Ameongeza kuwa, kinachochelewesha baadhi ya wafanyabiashara kuanza shughuli zao katika soko hilo ni kufanya matengenezo, huku wengine wakiwa bado wanaagiza mizigo yao.

“Hata ukienda jengo la DDC, fremu bado hazijaisha kwa sababu maduka yale yanahitaji matengenezo. Pia kuagiza mizigo kunahitaji gharama kubwa tofauti na wale wanaouza bidhaa kama nyanya,” amesema.

Amesema wanaendelea kuwahimiza na kuwapa taarifa wafanyabiashara hao kuwa wamepewa muda wa mwezi mmoja unaoisha mwishoni mwa mwezi huu, na tayari wameanza kuwatumia barua kwa kuwa wana mikataba nao.

Mhadhiri wa Uchumi katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Timothy Lyanga amesema Watanzania wengi wanaona kuwa bidhaa zinazouzwa barabarani ni nzuri na huuzwa kwa gharama nafuu ikilinganishwa na zile zinazopatikana katika maeneo rasmi ya biashara.

“Pia, kuna ulegevu mkubwa katika usimamizi wa sheria zilizopo. Mara nyingi zimekuwa zikifanywa operesheni ambazo hazileti mafanikio. Ni lazima sheria isimamiwe kikamilifu ili kuhakikisha wanaopanga biashara katika maeneo yasiyo rasmi wanapewa adhabu kubwa,” amesema.

Sababu nyingine aliyoitaja ni kuwepo kwa tozo kubwa, akishauri Serikali inapaswa kukubali kupunguza tozo katika masoko hayo ili kuvutia wafanyabiashara na kuhakikisha kiwango kinakuwa cha chini.

“Unajua wamachinga wanafanya biashara kwa ajili ya kusaka mkate wa kila siku. Ni lazima wapewe elimu na waelekezwe kufanya shughuli zao katika maeneo rasmi. Naamini baadaye Watanzania watazoea kwenda kununua katika masoko hayo.”