Vyama vya siasa Mbeya vyaanzisha umoja kusaidiana

Mbeya. Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mbeya kimeahidi kubeba gharama za matibabu kumsaidia Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoani humo, Hamad Mbeyale, aliyelazwa katika Hospitali ya Rufaa Kanda Mbeya.

Pia kimependekeza kuundwa kwa umoja na ushirikiano baina ya vyama vya siasa mkoani humo, wenye lengo la kusaidiana wakati wa shida na raha, utakaofahamika kama ‘Chama cha Viongozi Wenye Mawazo Mbadala’, huku kikiahidi kuchangia Sh20 milioni kuendesha umoja huo.

Akizungumza wakati wa kikao cha Viongozi wa vyama vya upinzani mkoani humo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Patrick Mwalunenge, amesema kila kiongozi, kwa nafasi yake, anapaswa kutanguliza maslahi ya wananchi na kuweka kando tofauti za kisiasa.

Amesema matarajio yake katika umoja huo wa vyama vya siasa utaleta mabadiliko chanya katika jamii na kuongeza chachu ya maendeleo kwa wananchi wa jiji na mkoa kwa ujumla, akiomba vyama hivyo kumsaidia Katibu wa Chadema, Mbeyale, aliyelazwa hospitalini kwa takribani wiki mbili sasa.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya na Mbunge wa Mbeya mjini, Patrick Mwalunenge akizungumza na viongozi wa vyama vya upinzani mkoani humo katika kikao maalumu cha kujadili mwenendo wa siasa na kumsaidia Katibu wa Chadema mkoani humo, Hamad Mbeyale aliyelazwa hospitalini



“Binafsi nitabeba gharama zote, takribani Sh2 milioni, lakini naona tuwe na umoja wetu wa vyama vya siasa kwa ajili ya shida na raha. Na kwa kuanzia nitachangia Sh20 milioni kwa ajili ya kuendesha shughuli za umoja huu.

“Nisisitize kwamba tuache maslahi binafsi, badala yake, tutangulize maslahi ya wananchi wa mkoa wetu, tushirikiane kwa pamoja, tuweke pembeni tofauti zetu za kisiasa,” amesema Mwalunenge.

Mwalunenge, ambaye pia ni mbunge wa Mbeya Mjini, ameongeza kuwa lengo la kukutana na vyama vya upinzani ni sehemu ya jitihada za kuimarisha uhusiano, ushirikiano na kujenga mawasiliano, pamoja na kujenga Mbeya mpya yenye maendeleo.

Akizungumza kwa njia ya simu, Katibu wa Chadema, Mbeyale, amesema hakuhudhuria kikao hicho kutokana na kuwa hospitali kwa matibabu kwa wiki mbili sasa, huku akimshukuru Mwalunenge kwa mchango huo.

“Sikushiriki kikao hicho na sijajua kama kuna mwakilishi yeyote wa Chadema aliyefika, kwa kuwa bado nipo hospitali. Nashukuru kusikia ahadi hiyo na waniombee afya njema,” amesema Mbeyale.

Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Wananchi (CUF) Mkoa huo, Ibrahim Mwakwama, amesema umoja huo utakuwa na manufaa kuanzia mtu mmoja mmoja, kundi na hata kijamii, akieleza kuwa kinachosubiriwa ni kutungwa kanuni na kupata viongozi.

“Tunaona hata kanda ya Kaskazini, linapokuja suala la maendeleo wanashirikiana, hivyo mambo ya kitaifa yatabaki vilevile. Hapa Mbeya tuna mambo yetu, tunaamini yale madhila kwa viongozi wa vyama vya upinzani yataisha kupitia umoja huu. Lakini itasaidia wakati mtu anapokutwa na changamoto au jambo zuri linaweza kusaidia kulimudu na ushirikiano na viongozi wenzake kisiasa, na italeta jamii pamoja na kuondoa ubinafsi,” amesema Mwakwama.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chauma) mkoani humo, Ipyana Samson, amesema hatua ya kumchangia gharama za matibabu kiongozi wa Chadema ni mwanzo mzuri katika kujenga umoja na kuondoa itikadi za kisiasa.

“Iwapo umoja huu utasimamiwa vyema, unaweza kubadili hali ya siasa yetu kwa mkoa; ushirikiano na muunganiko unaweza kuleta chachu ya maendeleo, na tuombe vyama vyote vijiunge,” amesema Samson.