Wakulima Bonde la Kalenga walia na uharibifu wa mazao baada ya mvua kubwa

Iringa. Baadhi ya wakulima wanaolima katika Bonde la Kalenga mkoani Iringa wameeleza kilio chao kufuatia mafuriko yaliyosababisha maji kujaa mashambani na kuharibu sehemu kubwa ya mazao yao, hali ambayo imewaacha wengi wakiwa katika wakati mgumu kiuchumi.

Wakulima wengi katika eneo hilo wamesema hutegemea kilimo cha bonde kama chanzo kikuu cha chakula na kipato, hivyo uharibifu wa mazao hayo umeibua hofu ya upungufu wa chakula na kuporomoka kwa kipato cha familia nyingi.

Wakizungumza leo Machi 6, 2026 na Mwananchi baada ya kufika katika bonde hilo na kujionea hali halisi ya mashamba, wakulima hao wamesema mvua kubwa zilizoanza kunyesha katika siku za hivi karibuni zimeongeza kwa kiasi kikubwa kiwango cha maji katika mto uliopo karibu na mashamba yao.

Upendo Nyanginywa, mkulima wa mazao kutoka bonde hilo amesema “Kutokana na hali hiyo, maji yalivuka kingo za mto na kuingia moja kwa moja katika mashamba, hali iliyosababisha mazao mengi kuharibika kabla hata hayajakomaa”

Wakulima hao wamesema walikuwa tayari wamewekeza gharama kubwa katika kununua mbegu, mbolea na kulima mashamba yao wakitegemea kupata mavuno mazuri katika msimu huu wa kilimo.

“Tumepata hasara kubwa sana kwa sababu maji yameingia ghafla mashambani na kufunika mazao yetu na tulitegemea mavuno haya kwa ajili ya chakula cha familia na pia kuuza ili kupata kipato, lakini sasa tunahofia kuwa hatutapata chochote,” amesema Yohana  Ndazi mmoja wa wakulima waliokutwa katika bonde hilo.

Baadhi ya shamba ambalo limejaa maji baada ya mvua kubwa kunyesha na kusababisha mto Ruaha kujaa na kujaza maji mashamba yaliyopo jirani na mto huo katika Bonde la Kalenga Wilayani Iringa. picha na Christina Thobias



Wakati Mwananchi Digital ikitembelea eneo hilo, ilishuhudia maji katika sehemu kubwa ya mashamba yaliyopo ndani ya bonde hilo huku baadhi ya mazao kama mahindi na nyanya yakiwa yamefunikwa na maji.

Aidha baadhi ya wakulima walionekana wakihangaika kuvuna mazao yao kwa haraka huku wengine wakiyabeba kwenye ndoo na mifuko wakitarajia kuyapeleka sokoni wakitarajia kuyauza bei ya chini.

“Tunalazimika kuvuna hata kama mazao hayajakomaa vizuri ili tuweze kuyauza, tukiyaacha mashambani yataharibika kabisa kwa sababu maji yamejaa sana,” amesema Peter Haji mkulima aliyekuwa akivuna mazao yake katika bonde hilo.

Mwenyekiti wa Bonde hilo, Ojuku Mgumba amesema changamoto ya mafuriko imekuwa ikijitokeza katika eneo hilo, hasa wakati mvua zinaponyesha na kuwa kwa sasa hali imekuwa mbaya kutokana na mvua nyingi zinazoendelea kunyesha katika maeneo hayo ambayo huchangia kuongezeka kwa maji katika mto unaopita karibu na bonde hilo.

Akizungumzia hali ya miaka iliyopita, Mgumba amesema tatizo hilo halijaanza sasa bali limekuwa likijitokeza na jitihada za kupunguza madhara ya mafuriko hayo, wakulima kwa kushirikiana na viongozi wa eneo hilo waliwahi kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kujenga tuta la kuzuia maji yasivuke na kuingia mashambani.

Diwani wa Kata ya Ulanda, Philemon Temaigwe amesema uongozi wa kata unatambua uwepo wa changamoto hiyo na unaendelea kufuatilia kwa karibu ili kuona namna bora ya kuwasaidia wakulima hao.

“Kuna changamoto katika bonde hili na bado tunaendelea kuangalia namna ya kuwasaidia wakulima ili hata miaka ya baadaye isitokee changamoto,” amesema Diwani Temaigwe.

Hata hivyo, uongozi wa Bonde la Maji Rufiji mkoani Iringa umesema wakulima hawaruhusiwi kufanya shughuli za kilimo ndani ya mita 60 kutoka kandokando ya mto.

Kauli hiyo imetolewa na Ofisa Uhusiano kwa Umma wa taasisi hiyo, Jacqueline Mmbiki kuwa kwa mujibu wa sheria za usimamizi wa bonde ya maji, kufanya shughuli za kilimo ndani ya eneo hilo ni kinyume na sheria zilizowekwa kwa lengo la kulinda vyanzo vya maji pamoja na kupunguza athari za mafuriko katika maeneo ya karibu na mito.

“Sheria ya mabonde ya maji inamtaka mkulima kutolima ndani ya mita 60 kutoka kandokando ya mto na kama kuna wakulima wamefanya kilimo ndani ya eneo hilo basi ni makosa, lakini timu yetu itafika katika eneo hilo kupima na kujua umbali wa mashamba hayo kutoka mtoni na kuona namna ya kutatua changamoto hiyo,” amesema Jacqueline.