Wakuu EAC kuja na jina la Katibu Mkuu, ugumu wa kumpa watajwa

Arusha. Mkutano wa 25 wa dharura wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), utakaofanyika kesho Machi 7, 2026, pamoja na mambo mengine, unatarajiwa kuja na jina la Katibu Mkuu mpya atakayeongoza Sekretarieti ya EAC kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Ugumu wa kumpata katibu mkuu mpya unatokana na desturi iliyokuwepo kukiukwa katika awamu iliyomalizika, ambayo ilikua ni zamu ya Sudani Kusini. Hata hivyo, hawakumteua katibu mkuu kwa sababu nchi hiyo haikuwa tayari kubeba dhamana hiyo, na nafasi yake kuchukuliwa na Kenya kwa awamu ya pili.

Utaratibu wa nafasi ya Katibu Mkuu wa EAC huwa ni wa kupokezana miongoni mwa nchi wanachama. Iwapo itahitajika, nchi tatu waanzilishi—Kenya, Uganda, na Tanzania wateue kwa awamu ya pili kabla nchi mpya zilizojiunga baadaye, nafasi hiyo inaweza kuwa ya Uganda au Tanzania.

Nchi waanzilishi zimekuwa na rekodi nzuri za kutekeleza wajibu wao wa kikanuni wa kulipa michango ya kila mwaka, ili kuiwezesha Sekretarieti, Bunge, na Mahakama pamoja na taasisi zake zilizopo kwenye nchi wanachama kutekeleza wajibu wake, ikiwa ni pamoja na kulipa mishahara ya wafanyakazi, gharama za uendeshaji, na stahiki nyingine za wafanyakazi.

Tangu kuanzishwa kwa EAC mwaka 1999, nafasi ya katibu mkuu imekuwa ya kupokezana kutoka nchi moja hadi nyingine, hatua iliyolenga kuimarisha umoja na mshikamano ili kufikia malengo makuu ya kuanzishwa kwake.

Waliowahi kuwa makatibu wakuu ni Francis Muthaura (Kenya), Amanya Mushega (Uganda), Balozi Juma Mwapachu (Tanzania), Dk Richard Sezibera (Rwanda), Balozi Liberat Mfumukeko (Burundi), Dk Peter Mathuki na Veronica Nduva (Kenya), ambaye awamu yake inakoma Aprili mwaka huu.

Mhadhiri mwandamizi wa sheria za kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Makumira (Tuma), Profesa Elifuraha Laltaika, amesema kipaumbele cha nafasi ya katibu mkuu kiwe kwa nchi ambayo haijawahi kupata nafasi hiyo, lakini sifa zake za kitaaluma na uwezo wa kiungozi ndio ziwe msingi wa kumpata bila kujali anatoka nchi ipi mwanachama.

“EAC ilipofikia inahitaji katibu mkuu atakayeikwamua ilipo na kuipa sura mpya inayoangalia wananchi zaidi, kushawishi nchi wanachama kuchangia kwa wakati, na kuongeza ufadhili kutoka nchi wahisani,” amesema Profesa Laltaika.

Rais wa Kenya, Dk William Ruto, ambaye ni mwenyekiti wa wakuu wa nchi za EAC, ameitisha mkutano huo unaofanyika jijini Arusha, makao makuu ya jumuiya hiyo iliyoasisiwa mwaka 1999 na marais watatu— Rais Ali Hassan Mwinyi (Tanzania), Rais Daniel Arap Moi (Kenya), na Rais Yoweri Museveni (Uganda).

Baraza la Mawaziri wa EAC lilipendekeza njia mbadala ambayo nchi wanachama wachangie kulingana na kiwango cha uchumi wake (GDP), kama zinavyochangia michango yake kwenye Umoja wa Afrika (AU), jambo ambalo lingeifanya Kenya kutoa fedha zaidi ya nchi nyingine.

Naye, mwanasheria wa biashara za kimataifa na uwekezaji, Elipokea Urio, amesema ni muhimu nchi wanachama wa EAC zinapopanga bajeti zao za kila mwaka, kutenga kipaumbele cha michango yao kwa ajili ya EAC. ili kuonesha utashi wa kisiasa na kutekeleza wajibu wa msingi wa kutoa michango kisheria.

Amesema ili nchi za EAC zijitegemee kwenye malengo ya bajeti zake, hazina budi kukuza uchumi wa kila nchi kwa kuuziana bidhaa miongoni mwa nchi wanachama badala ya kuagiza bidhaa nje, na kushauri viwango vipya vitakavyopendekezwa viwe vinavyofaa kuzingatia ukuaji wa kiuchumi wa kila nchi.

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) inaundwa na nchi nane ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudani Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), na Somalia.