Wanawake Maswa watoa vifaa tiba hospitali, wakisherehekea siku yao

Maswa. Wanawake wa Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu wametoa vifaa tiba pamoja na misaada mbalimbali kwa wagonjwa katika Hospitali ya Wilaya hiyo, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanayotarajiwa kufanyika Machi 8, 2026.

Akizungumza leo, Machi 6, 2025 wakati wa kukabidhi msaada huo, Mwenyekiti wa wanawake hao wilayani humo, Caroline Shayo, amesema wameamua kusaidia hospitali na wagonjwa baada ya kubaini kuwa bado kuna mahitaji mbalimbali muhimu yanayoweza kupunguza changamoto kwa wagonjwa.

Amesema msaada waliotoa umezingatia mahitaji yaliyotolewa na uongozi wa hospitali pamoja na hali halisi ya wagonjwa waliolazwa.

Mkaguzi wa polisi wilaya ya Maswa, Magreth Mwinuka akitoa msaada kwa mama ambaye amejifungua katika hospitali ya wilaya ya Maswa ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani. Picha na Samwel Mwanga



“Tumekuja kuwafariji wagonjwa, lakini pia kusaidia huduma za afya kwa kutoa vifaa tiba na mahitaji mengine muhimu. Tumetoa kifaa cha kusaidia kupatikana kwa mishipa kwa watoto wanaohitaji kuongezewa damu, jagi la kuchemshia maji kwa kutumia nishati ya umeme, mashuka na mablanketi kwa ajili ya wagonjwa, hususan watoto na akinamama waliojifungua, pamoja na mahitaji mengine,” amesema.

Mbali na vifaa tiba, wanawake hao pia wamekabidhi mahitaji kwa wagonjwa waliolazwa, hususan katika wodi ya wazazi, wodi ya watoto na wodi ya watoto njiti, ikiwemo chandarua kwa watoto, sabuni za kufulia, pampas, juisi na mafuta ya kujipaka.

Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Hollo Ngeme, amesema wanawake wa wilaya hiyo wameonesha mshikamano mkubwa kupitia michango yao mbalimbali, bila kujali shughuli wanazofanya, na wameungana kuamua kutoa misaada katika hospitali hiyo.

“Ninawashukuru wanawake wote kwa makundi mbalimbali na kwa mama mmoja mmoja kwa kuungana, kuchangia na kununua mahitaji mbalimbali kwa ajili ya wagonjwa, hususan wakinamama na watoto katika Hospitali ya Wilaya ya Maswa. Naomba mshikamano huu uendelee,” amesema.

Ofisa Maendeleo ya jamii halmashauri ya wilaya ya Maswa, Hollo Ngeme akizungumza baada ya wanawake wa wilaya hiyo kutembelea hospitali ya wilaya na kutoa misaada mbalimbali ya vifaa tiba kwa hospitali na misaada kwa wagonjwa. Picha na Samwel Mwanga



Akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Katibu wa hospitali hiyo, Emanuel Kusaga, amepongeza jitihada hizo na kusema msaada huo utasaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa wagonjwa, hususan watoto.

“Tunawashukuru sana wanawake wa Maswa kwa moyo wao wa kujitolea. Vifaa walivyotoa vitatusaidia katika kuwahudumia wagonjwa, hasa kifaa cha kusaidia kupata mishipa kwa watoto, ambacho ni muhimu katika kuwaongezea damu watoto wachanga,” amesema.

Ameongeza kuwa ushiriki wa jamii katika kusaidia sekta ya afya ni jambo muhimu linalochangia kuboresha huduma kwa wananchi.

Mmoja wa wagonjwa waliolazwa katika wodi ya wazazi, Rehema John, amesema msaada huo umewafariji na kuwapa matumaini zaidi wakati wanapopatiwa matibabu.

“Tunawashukuru sana wanawake waliokuja kututembelea na kutuletea mahitaji haya. Kwa kweli yametupa faraja na kutuonyesha kuwa bado jamii inatukumbuka,” amesema.

Kwa uPande wake, Neema Elias, aliyelazwa katika wodi ya watoto, amesema mahitaji waliyopata yatawasaidia katika kumhudumia mtoto wake.

“Pampas na sabuni tulizopewa zitatusaidia sana sisi akina mama tunaowahudumia watoto hapa hospitalini,” amesema.

Naye Halima Said, mgonjwa mwingine aliyelazwa hospitalini hapo, amesema ziara hiyo imeongeza hamasa kwa wagonjwa kuendelea kupambana na changamoto za afya.

“Kuona watu wanakuja kutuona na kutusaidia kunatupa nguvu ya kuendelea na matibabu,” amesema.

Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani hufanyika kila mwaka Machi 8 yakilenga kutambua mchango wa wanawake katika maendeleo ya jamii pamoja na kuhimiza usawa wa kijinsia.