
Wafanyakazi wanawake wa Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji Umeme (ETDCO) wakiongozwa na Kaimu Meneja wa Rasilimali Watu na Utawala wa Bi. Grace Sondi wakikabidhi mahitaji mbalimbali kwa Mkuu wa Gereza la Mahabusu Segerea, Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Hamis Robert Ngaukia kwa ajili ya kuwafariji wafungwa wanawake na watoto wanaoishi gerezani hapo.
Kaimu Meneja wa Rasilimali Watu na Utawala Kampuni ya ETDCO Bi. Grace Sondi akizungumza kuhusu kampuni hiyo inavyoshiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii na kuendelea kuunga mkono makundi yenye uhitaji maalum katika jamii.
Meneja wa Huduma za Sheria wa ETDCO, Wakili Joyce Mwakijale (kushoto) akizungumza jambo wakati wa kukabidhi mahitaji kwa Mkuu wa Gereza la Mahabusu Segerea, Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Hamis Robert Ngaukia
Mkuu wa Gereza la Mahabusu Segerea, Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Hamis Robert Ngaukia akiishukuru Kampuni ya ETDCO kwa kuwafariji wafungwa na kuwakumbusha kuwa bado ni sehemu ya jamii inayowajali.

Wafanyakazi wanawake wa Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji Umeme (ETDCO) wakiwa katika picha ya pamoja
……
Wafanyakazi wanawake wa Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji Umeme (ETDCO) wametembelea na kutoa msaada katika Gereza la Mahabusu Segerea, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kuelekea Siku ya Wanawake Duniani inayotarajiwa kufikia kilele Machi 8, 2026.
Msaada waliotoa ni pamoja na sabuni, shehena ya magodoro, maziwa ya watoto, mafuta, malapa, taulo za kike, dawa za meno, miswaki, pempasi na nguo.
Akizungumza leo Machi 6, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa kukabidhi msaada huo katika Gereza la Mahabusu Segerea, Kaimu Meneja wa Rasilimali Watu na Utawala wa Kampuni ya ETDCO, Bi. Grace Sondi, amesema kuwa wanawake wa Kampuni hiyo wameguswa kutoa msaada huo kwa wahitaji, kwani wanaamini kile walichotoa kitasaidia wafungwa pamoja na watoto waliopo katika gereza hilo.
Naye Meneja wa Huduma za Sheria wa ETDCO, Wakili Joyce Mwakijale, amesisitiza umuhimu wa kuwasaidia wahitaji katika jamii, huku akishukuru kupata nafasi ya kufika gerezani hapo na kuwaona waliopo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Gereza la Mahabusu Segerea, Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Hamis Robert Ngaukia, ameishukuru Kampuni ya ETDCO kwa kutoa msaada huo katika gereza hilo kwa ajili ya wafungwa ambao wapo hapo kujifunza na kujirekebisha.
Amesema zawadi walizotoa zitatumika vizuri kwa kusudio lililokusudiwa, huku akieleza kuwa gereza hilo katika Mkoa wa Dar es Salaam ni gereza la pekee linalohudumia wazee, wanaume, wanawake pamoja na watoto.
“Mmefanya jambo la msingi kwani mnakwenda kuwasaidia wenzenu. Lengo la kuwapo hapa ni kuhakikisha wanapomaliza muda wao wanakuwa raia wema, hawarudii kufanya makosa tena na badala yake wanajishughulisha na kazi halali ili taifa liendelee kusonga mbele,” amesema ACP Ngaukia.