Kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake, wanawake kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) wametembelea Gereza la Wanawake Segerea jijini Dar es Salaam na kutoa msaada wa vifaa na mahitaji mbalimbali kwa ajili ya kuwafariji wafungwa wanawake na watoto wanaoishi gerezani hapo.
Katika ziara hiyo, wanawake hao walikabidhi mahitaji muhimu kwa uongozi wa gereza ikiwemo vyakula, mavazi, taulo za kike, maziwa ya watoto pamoja na vifaa vya usafi, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za kuboresha ustawi wa wafungwa wanawake na watoto waliopo gerezani.
Kwa niaba ya Mkuu wa Gereza, Mrakibu Msaidizi wa Magereza, Ngajebule Mbuguru, aliishukuru TCAA kwa msaada huo akibainisha kuwa unaleta faraja kwa wafungwa na kuwakumbusha kuwa bado ni sehemu ya jamii inayowajali.
Aliongeza kuwa vifaa na mahitaji yaliyotolewa vitasaidia kukidhi baadhi ya mahitaji muhimu ya kila siku ya wafungwa wanawake na watoto waliopo gerezani, huku Jeshi la Magereza likiendelea kutoa mafunzo ya ujuzi mbalimbali kwa wafungwa ili kuwaandaa kujitegemea pindi watakaporejea katika jamii.
Kwa niaba ya uongozi wa TCAA, Afisa Rasilimali Mkuu, Grace Kiunsi, alisema hatua hiyo ni sehemu ya utamaduni wa Mamlaka kushiriki katika shughuli za kijamii na kuendelea kuunga mkono makundi yenye uhitaji maalum katika jamii.
Alisema TCAA inaamini kuwa kuwatia moyo na kuwasaidia wanawake walioko katika mazingira mbalimbali ni sehemu ya kuchangia ujenzi wa jamii yenye mshikamano, utu na kujali.
Wafanyakazi wanawake wa TCAA wakiongozwa na Afisa Rasilimali Mkuu, Grace Kiunsi wakikabidhi msaada wa vifaa na mahitaji mbalimbali Mrakibu Msaidizi wa Magereza, Ngajebule Mbuguru kwa niaba ya Mkuu wa Gereza kwa ajili ya kuwafariji wafungwa wanawake na watoto wanaoishi gerezani hapo.
Mrakibu Msaidizi wa Magereza, Ngajebule Mbuguru akiishukuru Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kwa kuwafaraji kwa wafungwa na kuwakumbusha kuwa bado ni sehemu ya jamii inayowajali.
Afisa Rasilimali Mkuu, Grace Kiunsi akizungumza kuhusu Mamlaka inavyoshiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii na kuendelea kuunga mkono makundi yenye uhitaji maalum katika jamii.
Baadhi ya misaada iliyotolewa na TCAA katika gereza la Segerea







