Waziri ataka wananchi Zanzibar wasichague kazi

Unguja. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawa Bora Zanzibar, Haroun Ali Suleiman amewataka wananchi kuchangamkia kazi za hoteli kwa kuwa Serikali imewekeza zaidi katika eneo hilo.

Haroun ameyasema hayo leo Ijumaa Machi 6, 2026 katika mkutano na waandishi wa habari uliolenga kueleza mafanikio ya siku 100 za Dk Hussein Ali Mwinyi katika kipindi chake cha pili, uliofanyika Mjini Unguja.

Haroun amesema wananchi kisiwani hapa wamejikita zaidi kufanya biashara pekee na sio kuchangamkia kazi za aina ya hoteli, ndio maana nafasi zao zinachukuliwa na wageni.

“Sio kama kazi hazipo, zipo nyingi husuani za mahoteli lakini wananchi hawawezi kufanya kazi ngumu na wana mitazamo hasi juu ya kazi za mahoteli ndio maana zinachukuliwa na wageni,” amesema

Hivyo, waziri huyo amesema Serikali ina jukumu kubwa la kubadilisha mitazamo ya wananchi ili kuwa tayari kujipambania kupitia kazi za aina zote na hawatakiwi kuchangua kazi.

Amesisitiza kuwa, vijana wamegemea zaidi kutafuta kazi za vikosi, ingawaje wengi wao wanashindwa wakiwa kambini kufanya kazi ngumu ikiwemo kulima.

Amesema, Serikali imewasihi vijana kujiajiri katika kilimo lakini bado wameshindwa kufanya hivyo, wamebaki kulalamika wakisema hakuna ajira. 

“Vijana wanaofanikiwa ni wale ambao hawachagui, hivyo nawashauri kufanya kazi ambayo unapata kipato halali bila kujali ugumu wake,” amesema 

Kadhalika, Waziri huyo amesema wizara hiyo imefanikiwa kuongeza majaji kutoka wanane mwaka 2021 hadi kufikia 14 mwaka 2025, kati yao wanawake watano na wanaume tisa, jambo ambalo linarahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Hata hivyo, amesema Serikali kujenga mahakama nyingi za mkoa na wilaya  haimaanishi Zanzibar uhalifu umeongezeka, bali ni kwa ajili ya kuwasogezea wananchi huduma.

Amesema, awali wananchi walikuwa wanapata changamoto katika kutafuta haki zao kwani iliwalazimu kutembelea masafa marefu kufuata huduma za mahakama ambapo wengi walishindwa.

Pia, ameeleza kuwa wizara hiyo inajipanga kuanza kupima utendaji wa kazi wa mtu mmoja mmoja kwa wafanyakazi na kuongezewa masilahi kwa watakaostahili.

Amesema, kwa sasa uboreshaji wa masilahi kwa wafanyakazi hauzingatii utendaji kazi wa mtu ndio maana wote wanapata nyongeza ikiwemo ya mishahara.

Sambamba na hilo, amesema wapo viongozi ambao wanatumia madaraka vibaya kwa kuwaumiza wafanyakazi kwa chuki zao binafsi, hivyo amewataka kuacha tabia hiyo.

Waziri huyo amewataka watendaji kujenga nidhamu ya utumishi kwa wafanyakazi kwenye taasisi zao kwa lengo la kujenga heshima baina yao.

Naye, Mkurugenzi wa Idara Habari Maelezo Zanzibar, Salum Ramadhani Abdallah amesema wizara hiyo inajitahidi kuhakikisha wananchi  wanapata haki zao kwa urahisi, ndio maana inaimarisha utendaji kazi kwa kuboresha ustawi wa jamii.