Na Mwandishi Wetu, Tunduru
Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, amempa siku 14 mkandarasi anayetekeleza mradi wa kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Songea hadi Mahumbika kupitia Tunduru na Masasi kurejea eneo la mradi na kuendelea na kazi mara moja.
Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo unaotekelezwa na kampuni ya Kalpataru Projects International Limited, ambayo ina jukumu la kujenga vituo vya kupoza umeme katika wilaya za Tunduru, Masasi na Mahumbika.
Akitoa agizo hilo Machi 7, 2026 wilayani Tunduru mkoani Ruvuma, Ndejembi amesema mkandarasi huyo hapaswi kupewa kazi nyingine yoyote ya serikali hadi atakapokamilisha mradi huo ambao utekelezaji wake umechelewa kinyume na masharti ya mkataba.
Aidha, Waziri huyo amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati kumuandikia barua ya onyo mkandarasi huyo, akieleza kuwa tayari walikutana na uongozi wa kampuni hiyo jijini Dodoma na kukubaliana kuwa wangeanza kazi ndani ya siku 25 baada ya kulipwa fedha walizokuwa wanadai tangu Desemba 2025.
Hata hivyo, amesema hadi sasa mkandarasi huyo hajarejea katika eneo la mradi wala kuanza kazi.
“Huyu mkandarasi anafanya kazi kwa kusuasua sana. Walilipwa fedha mwezi Desemba na tukakubaliana ndani ya siku 25 wawe wamerudi site na kazi ianze, lakini muda wote umeisha na hakuna kinachoendelea,” amesema Ndejembi.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, mradi huo ulipaswa kukamilika ndani ya kipindi cha miaka miwili na kukabidhiwa mwishoni mwa mwaka huu, lakini hadi sasa utekelezaji umefikia takribani asilimia 50 pekee.
Amesema mradi huo ni sehemu ya mpango wa serikali wa kuunganisha mikoa ya kanda ya kusini ambayo ni Ruvuma, Lindi na Mtwara kwenye gridi ya taifa ili kuboresha upatikanaji wa umeme wa uhakika.
“Wananchi wa Kusini wanahitaji umeme wa uhakika na serikali imeweka kipaumbele katika kutatua changamoto hiyo kwa kutoa fedha za kutekeleza mradi huu. Haiwezekani mkandarasi akachelewesha kazi hii,” amesema.