Bei ya kakao yaishtua Serikali, yaita wadau kusuka mikakati

Mbeya. Wakati bei ya zao la kakao ikiendelea kushuka, Serikali imeeleza sababu za hali hiyo huku ikitangaza mikakati mitano ya kuimarisha soko na kulinda thamani ya zao hilo.

Wadau na wakulima wa zao hilo pia wametoa ushauri wa hatua za moja kwa moja zinazoweza kusaidia kulinda thamani ya kakao kwa manufaa ya wakulima na Taifa kwa ujumla.

Kwa sasa, uzalishaji wa kakao nchini unafanyika zaidi katika mikoa ya Mbeya, Morogoro, Tanga na Songwe, huku Mkoa wa Kagera ukitajwa kuwa na uzalishaji mdogo. Takribani wakulima 32,500 wanajishughulisha na kilimo cha zao hilo.

Katika miaka ya hivi karibuni, Tanzania imeonesha kuongezeka kwa uzalishaji wa kakao. Taarifa zinaonesha kuwa uzalishaji umeongezeka kutoka tani 12,000 mwaka 2023 hadi kufikia tani 17,000 mwaka 2025. Serikali imeweka lengo la kuongeza uzalishaji huo hadi kufikia tani 80,000 ifikapo mwaka 2030.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao mchanganyiko (COPRA), Irene Mlola akizungumza katika kikao cha kwanza na wadau wa zao la Kakao kilichofanyika jijini Mbeya kikihusisha mikoa minne inayolima zao hilo.



Hata hivyo, kwa takribani miaka mitatu iliyopita, bei ya kakao ilifikia zaidi ya Sh32,000 kwa kilo, lakini kwa sasa imeshuka hadi Sh5,540 katika mnada wa hivi karibuni, ikiwa chini ya bei elekezi ya Sh10,000 kwa kilo. Hali hiyo imezua taharuki miongoni mwa serikali, wadau na wakulima wa zao hilo.

Kutokana na hali hiyo, Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) ilikutana na wadau kutoka mikoa inayolima kakao kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika kuendeleza tasnia ya zao hilo.

Sababu za kushuka kwa bei

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika jijini Mbeya leo, Jumamosi, Machi 7, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa COPRA, Irene Mlola, amesema kushuka kwa bei ya kakao kunatokana zaidi na mabadiliko ya soko la dunia.

Amesema miaka miwili iliyopita, nchi kubwa zinazozalisha kakao duniani, ikiwamo Ivory Coast inayozalisha takribani tani milioni mbili na Ghana yenye uzalishaji wa tani 700,000 kwa mwaka, zilikumbwa na changamoto za hali mbaya ya hewa pamoja na milipuko ya magonjwa ya zao hilo.

Kwa mujibu wa Mlola, magonjwa hayo yaliathiri takribani asilimia 40 ya uzalishaji, hali iliyosababisha kampuni kubwa za kimataifa zinazonunua kakao kununua kwa wingi zaidi ili kuhifadhi akiba kwa matumizi ya baadaye.

Wadau wakiwa katika kikao kilichowakutanisha kujadili bei ya zao la Kakao kilichofanyika leo Jumamosi Machi 7, 2026 jijini Mbeya kikihusisha mikoa minne inayolima zao hilo.



“Hawakutarajia kwamba nchi hizo zingeweza kurejesha uzalishaji wao kwa haraka, hivyo walinunua kakao nyingi na kuhifadhi katika maghala wakihofia upungufu wa bidhaa hiyo,” amesema.

Ameongeza kuwa baada ya nchi hizo kurekebisha changamoto na kurejesha uzalishaji wao katika hali ya kawaida, wanunuzi walijikuta tayari wana akiba kubwa ya kakao kwenye maghala yao, jambo lililochangia kupungua kwa mahitaji sokoni.

Pia amesema kakao ni zao lenye mahitaji makubwa duniani kutokana na matumizi yake katika utengenezaji wa bidhaa mbalimbali, ikiwemo pipi na chokoleti.

“Kwa sasa hata Ivory Coast wana takribani tani 100,000 za kakao kwenye maghala ambazo bado hazijapata wanunuzi. Hali hiyo inaathiri soko la dunia na ndiyo maana tunaona bei ikishuka,” amesema.

Ameongeza kuwa baadhi ya wanunuzi wamefunga mikataba ya muda mrefu ya ununuzi, jambo linalopunguza mahitaji mapya sokoni na kusababisha bei kushuka kutoka zaidi ya Sh32,000 hadi chini ya Sh10,000 kwa kilo.

Mlola amesema Serikali, kwa kushirikiana na wadau, imeweka mikakati kadhaa ya kuimarisha tasnia ya kakao ili kulinda uchumi wa wakulima na taifa kwa ujumla.

Mkakati wa kwanza ni kuongeza uzalishaji kutoka tani 17,000 za sasa hadi kufikia tani 80,000 ifikapo mwaka 2030, hatua ambayo itahitaji upatikanaji wa miche bora kwa wakulima. Amesema pia wakulima wanapaswa kupewa mafunzo ya kilimo bora ili kuongeza tija na kuhakikisha uzalishaji una faida kwa wadau wote katika mnyororo wa thamani wa zao hilo.

Mkakati wa pili ni kuboresha ubora wa kakao ili kuongeza ushindani wake katika soko la kimataifa, licha ya Tanzania kuwa na uzalishaji mdogo ikilinganishwa na nchi vinara kama Ivory Coast na Ghana.

Amesema COPRA imepanga kujenga makaushio saba ya kakao kabla ya Juni mwaka huu, huku bajeti ya mwaka ujao wa fedha ikilenga kuongeza makaushio hadi 20. Hatua hiyo pia itaendana na kuzingatia kanuni za Umoja wa Ulaya kuhusu ulinzi wa mazingira.

Mkakati mwingine ni kuhamasisha kilimo hai ili kukidhi mahitaji ya masoko ya kimataifa yanayozingatia usalama wa mazingira na afya ya walaji.

Mkakati wa nne ni kuendeleza kilimo cha mkataba, kitakachowezesha wakulima na wachakataji kuwa na uhakika wa soko na malighafi, sambamba na mfumo wa madaraja ya ubora kama ilivyo katika zao la kahawa.

Aidha, Serikali inapanga kuongeza thamani ya kakao kwa kuhamasisha uchakataji wa zao hilo ndani ya nchi, badala ya kuuza malighafi pekee.

“Lazima tuweke juhudi za makusudi kuhakikisha tunachakata kakao hapa nchini ili kuongeza thamani na kupanua fursa za soko,” amesema Mlola.

Katika kikao hicho, Mrajisi Msaidizi wa ushirika anayeshughulikia uhamasishaji na uratibu, Ibrahim Issa, amesema ujenzi wa viwanda vya kuchakata kakao ni hatua muhimu katika kulinda thamani ya zao hilo.

Amesema tayari ujenzi wa kiwanda umeanza katika Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya, huku maandalizi ya kujenga kiwanda kingine katika Wilaya ya Kyela yakiendelea baada ya kupatikana kwa eneo.

Issa pia amevielekeza vyama vya ushirika kusimamia ubora wa kakao na kudhibiti taarifa za wakulima ili kuweka mfumo mzuri wa masoko, kama ilivyo katika zao la kahawa.

“Tutaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuweka mikakati ya pamoja itakayosaidia kuimarisha soko la kakao na kuwanufaisha wakulima pamoja na taifa,” amesema.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa, amesema kushuka kwa bei ya kakao ni changamoto ya kimataifa, hivyo wadau wanapaswa kushirikiana na Serikali kutafuta suluhisho la kudumu. Amesema njia mojawapo ya kukabiliana na hali hiyo ni kuongeza ubora na thamani ya zao hilo.

“Kwa kuwa changamoto ya bei ni ya kimataifa, jukumu letu ni kuhakikisha tunaboresha ubora wa kakao yetu. Tunapaswa kukabiliana na hali hii kwa kutumia maarifa na ushirikiano,” amesema Malisa.

Baadhi ya wakulima wa kakao wamesema kushuka kwa bei ya zao hilo kumewashtua kutokana na tofauti kubwa ya bei iliyokuwapo awali.

Mkulima Obed Mwakatoga amesema wakulima wengi walizoea kuuza kakao kwa zaidi ya Sh32,000 kwa kilo, lakini kushuka hadi Sh5,540 kumewapa wakati mgumu.

Amesema suluhisho la kudumu ni serikali kuharakisha ujenzi wa viwanda vya kuchakata kakao ili wakulima waweze kuongeza thamani ya mazao yao kabla ya kuyauza.

“Tumesikia kwa muda mrefu kuhusu ujenzi wa viwanda vya kakao, lakini utekelezaji wake bado haujaonekana kwa kasi inayotarajiwa. Kama viwanda vitajengwa, tutachakata mazao yetu na kupunguza athari za kushuka kwa bei,” amesema.

Mwakatoga pia amesema bado kuna changamoto ya miche chakavu katika mashamba mengi ya kakao, akieleza kuwa baadhi ya wakulima bado wanatumia miti yenye umri wa kati ya miaka 40 hadi 50, wakati kitaalamu mti wa kakao unapaswa kubadilishwa baada ya takribani miaka 25.