BoT YAFAFANUA SABABU ZA KUNUNUA NA KUUZA DHAHABU


Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) amesema kuwa hatua ya benki hiyo kununua na wakati mwingine kuuza dhahabu ni utekelezaji wa matakwa ya sheria pamoja na usimamizi madhubuti wa akiba ya fedha za kigeni ya taifa.

Akizungumza wakati wa hafla ya futari iliyoandaliwa na benki hiyo, gavana huyo alifafanua kuwa kwa mujibu wa sheria ya benki kuu, kifungu cha tano kinaelekeza benki kununua dhahabu kama sehemu ya kuhifadhi akiba ya fedha za kigeni kwa ajili ya mustakabali wa uchumi wa nchi.

Alisema kifungu cha 52 cha sheria hiyo kinaeleza wazi kuwa benki inapokuwa imehifadhi dhahabu au mali nyingine za fedha za kigeni, inaruhusiwa kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo kununua, kuuza, kuwekeza au kuagiza mali hizo kulingana na mahitaji ya usimamizi wa akiba ya taifa.

Gavana huyo ameeleza kuwa uamuzi wa kununua au kuuza dhahabu hutegemea mwenendo wa bei katika soko la dunia. Alifafanua kuwa wakati bei ya dhahabu inapopanda kwa kiwango kikubwa, benki inaweza kuuza sehemu ya akiba hiyo ili kupata fedha za kigeni, hasa dola za Marekani, na baadaye kununua tena dhahabu endapo bei itashuka.

Ameongeza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya usimamizi wa hatari zinazotokana na mabadiliko ya bei katika masoko ya fedha duniani, akibainisha kuwa soko la dhahabu lina tabia ya kubadilika kwa kasi (volatility), hivyo maamuzi hayo hufanywa kwa misingi ya kitaalamu kama ilivyo katika biashara na uwekezaji wa masoko ya fedha.

Aidha, gavana huyo amekiri kuwa baadhi ya wananchi wasiokuwa na uelewa wa kina kuhusu masoko ya fedha wanaweza kuwa na maswali kuhusu hatua hizo. Hata hivyo, alisema benki inaendelea kutoa elimu kwa umma ili kuongeza uelewa na kuwahamasisha wananchi kushiriki katika uwekezaji na masoko ya fedha.

Katika hatua nyingine, amesema kuwa katika kipindi cha miaka 60 ya utekelezaji wa majukumu yake, Benki Kuu ya Tanzania imeendelea kuwa miongoni mwa taasisi zinazoheshimika kimataifa kutokana na utendaji wake mzuri.

Amebainisha kuwa benki hiyo imeendelea kusimamia ukuaji wa uchumi, kudhibiti mfumuko wa bei, kulinda uthabiti wa thamani ya shilingi pamoja na kuimarisha mifumo ya malipo ya kisasa.

Pia amesema benki imekuwa ikichapisha na kusambaza fedha kwa viwango vinavyohitajika na kusimamia mifumo ya malipo kwa kutumia teknolojia za kisasa kwa uadilifu na uwajibikaji.

Gavana huyo ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kuliombea taifa amani, upendo na mshikamano pamoja na kudumisha uzalendo na ushirikiano katika kujenga uchumi wa nchi, hasa katika kipindi ambacho uchumi wa dunia unakabiliwa na changamoto mbalimbali.

Ametaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na vita, mivutano ya kisiasa duniani, athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na misukosuko ya kiuchumi ya kimataifa.

Aidha, amesisitiza kuwa benki kuu inathamini mchango wa taasisi za dini katika kujenga maadili mema kwa waumini wake, akisema maadili hayo ni msingi muhimu wa kuwa Watanzania wema na watumishi bora katika taasisi mbalimbali wanazozitumikia.