AZAM FC baada ya kucheza mechi mbili za Ligi Kuu Bara ugenini na kutoka sare zote, leo Jumapili itakuwa nyumbani ikiikaribisha Mbeya Kwanza katika hatua ya 32 Bora ya Kombe la Shirikisho la CRDB, huku kocha wa kikosi hicho, Florent Ibenge akisema kuna kitu amekishtukia kwa washambuliaji wake.
Pointi mbili ilizovuna Azam kwenye mechi hizo ikianza na sare ya 2-2 dhidi ya Pamba Jiji iliyochezwa jijini Mwanza na 0-0 mbele ya Tanzania Prisons pale Mbeya, zimemshtua Ibenge.
Matokeo hayo yamempa hesabu mpya kocha wa Azam Florent Ibenge ambaye ameliambia Mwanaspoti kuwa hajafurahishwa na sare hizo mbili lakini bado hazijawaharibia malengo yao.
Ibenge amesema bado kuna kazi wanatakiwa kuifanya kuiongezea nguvu safu yake ya ushambuliaji ili iweze kutumia nafasi ambazo wanatengeneza kwenye mechi zao zinazoendelea.
Ibenge aliongeza kuwa, safu yake ya ushambuliaji inaendelea kuzoea ugumu wa ligi kutokana na washambuliaji wake kuwa wapya, ambapo wanatakiwa kuongezewa ufanisi ili wafunge zaidi kwenye mechi za ugenini.
“Huwezi kufurahishwa na hatua ya kuangusha pointi nne ugenini tena mfululizo, si matokeo ambayo tunastahili lakini kutokana na mazingira unayapokea, tunatakiwa kujiimarisha zaidi.
“Tunatengeneza nafasi lakini kwenye robo ya mwisho hatujaweza kuwa na makali zaidi, tuna washambuliaji wapya ambao wanaendelea kuzoea mazingira ya mechi kama hizi za ugenini, tunatakiwa kujipanga zaidi,” amesema Ibenge.
Washambuliaji halisi wa Azam ni Nassor Saadun ambaye huu ni msimu wa pili yupo na kikosi hicho lakini sasa anuguza majeraha. Mwingine ni Zidane Ally Sereri, huku Taieb Ben Zitoun, Aimar Hafidh Abubakar, Jean-Jacques Ngita na Jephte Kitambala wakitua msimu huu.
Katika orodha ya washambuliaji kikosini hapo Ngita aliyeanza kuitumikia Azam baada ya dirisha dogo la usajili la Januari 2026, anaongoza akiwa na mabao manne Ligi Kuu Bara akifuatiwa na Kitambala (2) na Saadun (1). Aimar aliyetua dirisha dogo hajafunga kama ilivyo kwa Ben Zitoun aliyeanza mwanzo wa msimu.
Azam inayoshika nafasi ya tatu na pointi 24 katika msimamo wa Ligi Kuu Bara huku ikifunga mabao 18, ikimalizana na Mbeya Kwanza, itasafiri hadi Dodoma kuifuata Dodoma Jiji itakayocheza nayo Machi 11, 2026 katika mwendelezo wa Ligi Kuu Bara, baada ya hapo itarudi nyumbani kuikaribisha, Yanga Machi 15, 2026.