LICHA ya kipa namba moja wa Dodoma Jiji, Ally Salim kukosekana uwanjani kutokana na majeraha ya bega, lakini kocha Amani Josiah amesema hatakuwa na haraka ya kumtumia, kwani lengo ni kumuona akiwa fiti zaidi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Josiah amesema kipa huyo anaendelea na programu maalumu ya madaktari wa kikosi hicho, ingawa muda si mrefu mashabiki watamuona tena uwanjani.
“Kwa sasa anaendelea vizuri chini ya uangalizi wa jopo letu la madaktari kutokana na majeraha yanayomkabili, kitu cha kufurahisha kwetu sisi benchi la ufundi ni kuona kila nafasi uwanjani ina wachezaji bora maeneo yote,” amesema.
Kipa huyo aliyejiunga na Dodoma Jiji, Septemba 7, 2025, akitokea Simba, alipata majeraha ya bega, wakati akiwa katika harakati za kuuokoa mpira, katika mechi ya Ligi Kuu Bara, kati ya kikosi hicho dhidi ya Mbeya City, Februari 3, 2026.
Katika mechi hiyo iliyopigwa Kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya na kuisha sare ya kufungana bao 1-1, Ally alipata majeraha hayo alipokuwa anauokoa mpira, baada ya kukutana na mchezaji wa Mbeya City aliyempiga kichwa kwenye bega lake.
Tangu ajiunge na Dodoma Jiji, Ally Salim amekuwa kipa wa kikosi cha kwanza, ambapo hadi sasa ana ‘Clean Sheets’ tano za Ligi Kuu, akipitwa na makipa, Erick Johola wa Mashujaa mwenye sita na kinara, Djigui Diarra wa Yanga ambaye ana saba.
Makipa wengine wenye ‘Clean Sheets’ tano za Ligi mbali na Ally, ni Yona Amos wa Pamba Jiji na Mussa Mbisa wa Tanzania Prisons, huku kwa sasa nafasi yake katika kikosi hicho cha ‘Walima Zabibu’, ikichukuliwa na Daniel Mgore.