Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Palamagamba Kabudi, ameongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki mikutano muhimu ya Jumuiya ya Madola inayofanyika jijini London nchini Uingereza ikilenga kujadili mustakabali wa jumuiya hiyo pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kati ya nchi wanachama.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imesema Profesa Kabudi amewasili London kushiriki Kikao cha 72 cha Kamati ya Mawaziri wa Jumuiya ya Madola (CMAG) pamoja na Mkutano wa 26 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo (CFAMM), mikutano inayowakutanisha viongozi wa kidiplomasia kutoka nchi 56 wanachama wa jumuiya hiyo.
Ushiriki wa Tanzania katika mikutano hiyo unafanyika kufuatia mwaliko rasmi kutoka kwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Shirley Botchwey.
Kikao cha CMAG kinatarajiwa kujadili utekelezaji wa maamuzi ya awali ya jumuiya hiyo pamoja na kuimarisha misingi na tunu zake, ikiwemo utawala bora, demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria katika nchi wanachama.
Kwa mujibu wa ratiba ya mikutano hiyo, Machi 8, Profesa Kabudi atashiriki Mkutano wa 26 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Madola, ambapo viongozi wa kidiplomasia watajadili masuala ya kimkakati kuhusu mustakabali wa jumuiya hiyo na namna ya kuimarisha mchango wake katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za kimataifa.
Masuala yanayotarajiwa kujadiliwa ni pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuimarisha taasisi za kidemokrasia na kuongeza mshikamano kati ya nchi wanachama katika mazingira ya dunia yanayobadilika kwa kasi.
Aidha, mkutano huo utaweka msingi wa vipaumbele vya sera kuelekea mkutano wa wakuu wa nchi na serikali wa Jumuiya ya Madola (Commonwealth Heads of Government Meeting 2026- CHOGM) unaotarajiwa kufanyika katika taifa la visiwa la Antigua na Barbuda kuanzia Novemba 1 hadi 4, 2026.
Mkutano huo wa wakuu wa nchi na serikali unatarajiwa kujadili mageuzi ya jumuiya hiyo pamoja na nafasi yake katika mfumo wa kimataifa.
Katika mikutano hiyo, Profesa Kabudi anamwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Thabit Kombo, na anatarajiwa kuwasilisha msimamo wa Tanzania katika ajenda mbalimbali zitakazojadiliwa na mawaziri wa nchi wanachama.
Mbali na kushiriki mikutano hiyo, Profesa Kabudi baada ya kuwasili tayari amefanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Botchwey, yaliyojikita katika kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na jumuiya hiyo, hususan katika maeneo ya utawala bora, demokrasia na maendeleo ya pamoja.
Katika mazungumzo hayo, Profesa Kabudi alisisitiza kuwa Tanzania inaendelea kuthamini nafasi na mchango wa Jumuiya ya Madola katika kukuza ushirikiano wa kimataifa na kuimarisha taasisi za kidemokrasia katika nchi wanachama.
Kwa upande wake, Botchwey alipongeza ushiriki na mchango wa Tanzania katika shughuli za jumuiya hiyo na kueleza dhamira ya kuendelea kuimarisha ushirikiano na nchi wanachama kwa lengo la kuleta maendeleo jumuishi.
Katika ziara hiyo ya kikazi, Profesa Kabudi ameambatana na Mshauri wa Rais katika masuala ya diplomasia, Lazaro Nyalandu. Ujumbe huo pia ulipokelewa katika ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza na Balozi wa Tanzania nchini humo, Mbelwa Kairuki, ambaye aliwasilisha taarifa kuhusu maandalizi na mwenendo wa mikutano hiyo.
Ushiriki wa Tanzania katika mikutano hiyo unatazamwa kama fursa muhimu ya kuendeleza diplomasia ya uchumi, kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kutoa nafasi kwa nchi kueleza vipaumbele vyake katika ajenda za maendeleo ndani ya Jumuiya ya Madola