ZIKIWA zimepita siku mbili baada ya Singida Black Stars kumfutia adhabu kiungo Khalid Aucho ya kumsimamisha kwa miezi mitatu kutokana na utovu wa nidhamu na utoro kazini, pia imefanya hivyo kwa kipa Amas Obasogie aliyekuwa akituhumiwa na ishu ya upangaji matokeo.
Hatua hiyo inakuja baada ya Februari 27, 2026, taarifa ya Singida Black Stars iliyotolewa na Ofisi ya Mtendaji Mkuu, Jonathan Kassano kubainisha kuwachukulia hatua za kinidhamu wachezaji hao kwa makosa tofauti.
Katika taarifa hiyo, ilisema Aucho ameadhibiwa kwa utovu wa nidhamu na utoro kazini, hivyo amesimamishwa kazi kwa miezi mitatu, huku Obasogie akisimamishwa kazi kwa miezi mitatu pia kupisha uchunguzi wa tuhuma za upangaji wa matokeo.
Mwisho kabisa, taarifa hiyo ilisitiza klabu inawakumbusha wachezaji na watumishi wake wote kuzingatia nidhamu, uwajibikaji na heshima kwa klabu.
Siku sita baada ya kusimamishwa wachezaji hao, Aucho alirudishwa kazini Machi 5, 2026, baada ya kukiri na kuomba radhi ambapo Kamati ya Nidhamu ya Singida Black Stars ilikaa na kujadili suala hilo kwa kina na kumsamehe.
Kisha Machi 7, 2026, zikipita siku nane tangu asimamishwe, Obasogie naye amesamehewa na kurudishwa kazini huku taarifa ya Singida Black Stars iliyotolewa na Kassano, ikisema baada ya uchunguzi wa awali, utetezi wa mchezaji pamoja na taarifa ya uhakika kutoka kwa Meneja Mkuu wa Klabu hiyo, imebaini hakuna ushahidi wa upangaji matokeo wala mchezo wa bahati nasibu.
“Klabu ya Singida Black Stars inapenda kuujulisha umma kuwa kulikuwepo na wasiwasi miongoni mwa uongozi, mashabiki na wadau kufuatia makosa ya kujirudia rudia katika baadhi ya michezo ya hivi karibuni, ikiwemo dhidi ya Flambeau du Centre (Kombe la Shirikisho Afrika), Pamba Jiji na Namungo FC (Ligi Kuu Bara).
“Kutokana na hali hiyo, Menejimenti ya Klabu kupitia Kamati ya Nidhamu ilichukua hatua ya kufanya uchunguzi wa awali kuhusiana na taarifa za wasiwasi zilizomhusu mchezaji wetu Amas Obasogie.
“Baada ya uchunguzi wa awali, utetezi wa mchezaji pamoja na taarifa ya uhakika kutoka kwa Meneja Mkuu wa Klabu, imebainika kuwa hakuna ushahidi wa upangaji wa matokeo wala mchezo wa bahati nasibu. Matukio yaliyoibua wasiwasi huo yamebainika kuwa ni makosa ya kiufundi ya ndani ya mchezo.
“Hata hivyo, mchezaji Amas Obasogie ameomba radhi kwa mazingira yaliyoibua tafsiri hizo na ameahidi kufanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza ili kuimarisha kiwango chake na kurejesha imani kwa mashabiki na wadau.
“Kwa kuzingatia hilo, Klabu imeamua kutengua uamuzi wa awali wa kusimamishwa kwa miezi mitatu, na mchezaji ameruhusiwa kuendelea na majukumu yake kikosini,” imesema taarifa hiyo ya Singida Black Stars iliyotolewa jana Machi 7, 2026.