Kuna kombe linatafutwa | Mwanaspoti

BAADA ya mabingwa mara tatu wa Kombe la Shirikisho la FA, Simba kutoka suluhu (0-0), dhidi ya watani zao wa jadi, Yanga katika mechi ya Ligi Kuu, iliyopigwa Machi 1, 2026, kikosi hicho kinashuka tena uwanjani leo kuiwinda tiketi ya michuano ya CAF.

Katika mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa kwa mara ya kwanza Kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani, Zanzibar, ilikuwa ya mwisho kwa kikosi hicho, ambapo leo itaikaribisha B19 FC, inayoshiriki Championship katika hatua ya 32 bora ikiwa inatokea Dar es Salaam.

B19 iliyotinga hatua ya 32 bora kibabe baada ya kuichapa Dhujau FC ya Katavi mabao 7-0, itakuwa ugenini Kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamhuyo Mbweni, kucheza dhidi ya kikosi cha Simba, kilichoitoa pia Greenland FC ya Kagera kwa mabao 3-0.

Katika Ligi ya Championship msimu huu, B19 FC ambayo zamani ni Tanesco, imekuwa haina mwenendo mzuri, baada ya timu hiyo kucheza mechi 20, ambapo imeshinda minne, sare sita na kupoteza 10, huku kikosi hicho kikiwa nafasi ya 13 na pointi 18.

Timu hiyo imekuwa haina muunganiko mzuri katika maeneo yote mawili ya kujilinda na ushambuliaji, kwani katika mechi hizo 20, ilizocheza hadi sasa, washambuliaji wa kikosi hicho wamefunga mabao 18 tu, huku nyavu zao zikitikiswa pia mara 33.

Simba chini ya Kocha Mkuu, Steve Barker, imekuwa haina mwenendo mzuri katika michuano hii, baada ya kulikosa taji hili mara nne mfululizo na kushuhudia likienda kwa watani zao Yanga, huku mara ya mwisho kulichukua ni msimu wa 2020-2021.

Kocha wa B19, Twaha Beimbaya, amesema licha ya kutarajia mechi ngumu kutokana na ubora wa wapinzani wao, ila watacheza kwa tahadhari na kwa nidhamu kubwa, hasa katika eneo la kujilinda, huku wao wakitengeneza mashambulizi ya kuwashtukiza.

Mechi nyingine leo, Transit Camp iliyoichapa Chama la Wana mabao 4-0, raundi iliyopita, itakuwa ugenini jijini, Mwanza kucheza dhidi ya kikosi cha Pamba Jiji ‘TP Lindanda’, iliyoitoa Alliance FC kwa penalti 4-2, baada ya sare ya bao 1-1.

KenGold kutoka jijini, Mbeya iliyofika hatua ya 32 bora, baada ya wapinzani wao, Magereza FC kushindwa kufika uwanjani, itakuwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma, kucheza dhidi ya Mashujaa iliyoichapa Nkim FC kutokea Tanga bao 1-0. 

Kwenye Uwanja wa Nyankumbu mjini, Geita, wenyeji, Geita Gold iliyofika hatua hii baada ya kuichapa Kajuna FC ya Kigoma bao 1-0, itaikaribisha Nyika FC ya Ligi Daraja la tatu Mkoa wa Pwani, iliyoichapa Bigman FC ya Championship kwa bao 1-0.

Mechi ya mwisho leo, itapigwa Kwenye Uwanja wa Majaliwa, Lindi, ambapo wenyeji, Namungo iliyoifunga Magnet FC ya Dar es Salaam mabao 4-1, itacheza dhidi ya vinara wa Championship, Kagera Sugar iliyoichapa Mighty Elephant ya Ruvuma mabao 3-0.