Maeneo ya fursa yanayoweza kuwakuza wanawake kiuchumi

Dar es Salaam. Wadau wa maendeleo wamebainisha maeneo muhimu yenye fursa yanayoweza kuongeza ushiriki wa wanawake katika shughuli za kiuchumi, ikiwemo kilimo chenye soko la uhakika ndani na nje ya nchi.

Mbali na kilimo, wadau hao wanaweka wazi masuala ambayo yakifanyiwa kazi kikamilifu, yatasaidia wanawake kushiriki ipasavyo katika ukuzaji wa uchumi na kuwa na jamii yenye ustawi mzuri.

Akizungumza katika mjadala maalumu Machi 6, jijini Dar es Salaam, Waziri wa Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo alisema kilimo cha kibiashara ni eneo ambalo wanawake na wananchi wengi wanaweza kushiriki kwa urahisi na wakawa na uwezekano mkubwa wa kujipatia kipato.

Mjadala huo ulikuwa ni sehemu ya jukwaa la sita la The Citizen Rising Woman, lililoandaliwa na Kampuni Mwananchi Communications Limited (MCL).

“Afrika ina soko kubwa la chakula, mwaka jana pekee bara la Afrika liliagiza chakula chenye thamani ya dola 110 bilioni za Marekani (Sh282 trilioni, jambo linaloonyesha fursa kubwa ya uzalishaji ndani ya bara ambayo watu wanaweza kuitumia kufanya uzalishaji na kuwekeza ili kujipatia kipato,” amesema.

Amesema eneo lingine linaloweza kutumiwa na wanawake kwa manufaa ni viwanda, hususani wakati huu ambao sera inalenga kuongeza thamani ya bidhaa kupitia usindikaji wa mazao ya kilimo na madini.

“Rais amesisitiza kwamba tusisafirishe tena malighafi bila kuziongezea thamani, hivyo ni sehemu ambayo inaweza kuangaliwa na katika eneo la usindikaji wa mazao ya kilimo na hata kule kwenye madini itakuwa na nafasi kubwa na tayari wanawake wengi wanaanza kushiriki,” amesema.

Baadhi ya wadau wakiwa katika jukwaa la sita la The Citizen Rising Woman, lililoandaliwa na Kampuni Mwananchi Communications Limited (MCL).



Amesema sekta ya huduma ambayo inayojumuisha biashara, teknolojia za kidijitali, utalii na ukarimu pia wanawake wanao uwezo mkubwa wa kufanya kazi katika sekta hizo, hivyo ni fursa nzuri kwao kuanzisha biashara, kupata kipato na kuchangia katika kuongeza ustawi wa jamii kwa ujumla.

Hili linawekwa wazi wakati ambao anakiri kuwa katika miaka 20 iliyopita ya utekelezaji wa Dira 2025, uchumi ulikuwa kwa kasi ya wastani wa takribani asilimia 6.2 kwa mwaka ambayo ni kiwango kizuri kimataifa na hata ndani ya Afrika hata hivyo pamoja na ukuaji huo, kupungua kwa umaskini kulikuwa polepole kuliko ilivyotarajiwa.

Ukuaji huo wa uchumi nao haukuweza kuzalisha ajira nyingi kama ilivyotarajiwa.

“Utafiti ulionyesha kwamba sekta zilizokuwa zinaongoza ukuaji wa uchumi hazikuwashirikisha Watanzania wengi. Ndiyo maana tukachagua dhana ya ushirikishwaji ili kuhakikisha kwamba kuanzia sasa tutalenga sekta ambazo zinawahusisha wananchi wengi, wakiwemo wanawake,” amesema.

Amesema na hiyo ndiyo sababu katika Dira 2050 neno “wanawake” limetajwa mara 25, wakati wanaume halijatajwa kwa sababu huwezi kupambana na umaskini bila kushughulikia umaskini wa wanawake.

Amesema kufanya hivyo walilenga kuweka msisitizo maalumu kwa wanawake ili kushughulikia masuala ya ajira na umaskini.

Amesema ili kufanikisha hilo, kuna maeneo manne muhimu ya uwekezaji ambayo yatasaidia sana kupunguza umaskini na kuongeza ushiriki wa wanawake ambapo la kwanza ni elimu kwa kila mtu katika jamii lakini hasa kwa wanawake.

“La pili ni umeme, ambao ni muhimu sana kwa maendeleo ya wanawake katika shughuli za kiuchumi na kijamii. La tatu linahusu kudhibiti kasi ya ukuaji wa idadi ya watu. Kwa sasa idadi ya watu inaongezeka kwa wastani wa asilimia 3 kwa mwaka na kiwango cha uzazi ni karibu watoto 4.3 kwa mwanamke. Tafiti zinaonyesha kuwa familia yenye watoto wengi huwa na uwezekano mdogo wa kufikia ustawi wa haraka,” amesema.

Amesema njia muhimu ya kukabiliana na hali hii ni kuwekeza zaidi katika elimu ya wasichana kwani wanapobaki shuleni kwa muda mrefu zaidi, kiwango cha uzazi hupungua na fursa za maendeleo huongezeka.

Kuhusu uwezeshaji wanawake

Profesa Mkumbo amesema kwa zaidi ya miaka 20 sasa, nchi imekuwa ikiendeleza juhudi za kuwawezesha wanawake, hata hivyo licha ya hatua zilizochukuliwa katika sera na mifumo ya kisheria, bado kuna changamoto ya mitazamo ya kijamii.

“Kwa mfano, si jambo la ajabu kwenda katika taasisi fulani na kukuta viongozi wote ni wanaume na hakuna anayeshangaa wala kuuliza swali lolote. Lakini ukienda katika taasisi ambayo viongozi wake wote ni wanawake, watu wengi huanza kuuliza, hapa kuna nini kinaendelea, hii inaonyesha kwamba bado tuna changamoto ya mtazamo katika jamii,” amesema.

Amesema ni vyema kutambua kuwa kama watu wana uwezo, wanastahili na wana sifa zinazohitajika, haipaswi kuwa tatizo hata kama wote ni wanawake lakini pia haipaswi kuwa kawaida kuona viongozi wote ni wanaume bila kuhojiwa.

Suala la elimu liliungwa mkono na Kaimu mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wanawake (Un Women), Karen Giath, ambaye amesema kuwekeza katika elimu ya wasichana kuna faida ya muda mrefu kwani anaamini wanapofikia kiwango fulani cha elimu wanapata uwezo wa kujitegemea na kuleta mabadiliko.

“Wanakuwa na uwezo wa kuleta mabadiliko katika familia zao na katika maisha yao. Pia, wanashiriki katika maeneo mengi yenye uzalishaji mkubwa wa uchumi,” amesema.

Amesema elimu inaongeza rasilimali watu kwa nchi, lakini pia inachangia ukuaji wa uchumi wa muda mrefu na kupunguza umasikini.

“Hii ni kwa sababu wanawake mara nyingi wanawekeza kwenye familia zao na nyumbani, hivyo uchumi unafaidika na familia zinapoongezeka ustawi wake,” amesema.

Baadhi ya wadau wakiwa katika jukwaa la sita la The Citizen Rising Woman, lililoandaliwa na Kampuni Mwananchi Communications Limited (MCL).



Eneo lingine alilotaka liangaliwe kwa karibu ni uwepo wa eneo la malezi ya watoto wa wanawake waliopo kazini, kwa kuwa hilo linaweza kusaidia kuongeza ufanisi wao katika majukumu waliyopewa.
Amesema mara kadhaa wanawake wanapotakiwa kushiriki kikamilifu katika maisha ya kazi, wanalazimika kupanga ratiba ngumu asubuhi ili kuhakikisha kazi zinaenda huku malezi ya watoto yakiendelea.

“Tunashukuru kwa baadhi ya kampuni zinazotoa huduma za malezi ya watoto katika mahali pa kazi. Hali hii inarahisisha wanawake kushiriki kikamilifu katika kazi zao bila kuchelewesha au kupunguza uzalishaji,”

“Vinginevyo, pale wanawake wanapolazimika kufikiria jinsi ya kuweka nguvu katika malezi, mara nyingi uzalishaji wao hupungua.

Mjumbe wa Bodi ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Aisha Mohammed amesema uwepo wa jukwaa la The Citizen Rising woman unaendana kwa karibu na matarajio ya maono ya Umoja wa Mataifa ambayo yanakusudia kuona Tanzania ikiwa nchi yenye ustawi, ushirikishwaji na ushindani wa kiuchumi.
Amesema ili kufikia maono hayo inahitajika kutumia kikamilifu vipaji na uwezo wa wananchi wote.

“Wanawake ni wajenzi, wabunifu, wataalamu na viongozi katika jamii zetu. Hivyo basi, kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika uongozi na shughuli za kiuchumi ni jambo muhimu kwa mafanikio ya ajenda yetu ya maendeleo ya taifa,” amesema.

Katika upande wa uwezeshaji wanawake kiuchumi, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Foundation, Tully Mwambapa alisema taasisi hiyo ilianzishwa baada ya kubaini kuwa wanawake wengi, hasa wale wanaoishi maeneo ya vijijini, nusu vijijini na vijiji halisi hawahudumiwi vya kutosha au hawahudumiwi kabisa na huduma za kifedha.

Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Foundation, Tully Mwambapa.



Lengo la kuanzishwa kwa taasisi hiyo ni kukuza ubunifu na maendeleo ya ujasiriamali na sasa wameweza kuwapatia wanawake fursa ya kupata huduma za kifedha, kuwapa mafunzo ya uongozi, na kuendeleza uwezo wao.

“Kupitia CRDB Bank Foundation, ili kuhakikisha wanawake wanapata huduma za kifedha, tulilazimika kubuni bidhaa maalumu ya kifedha inayolenga kundi la watu wasiohudumiwa vya kutosha na waliotengwa kiuchumi. Hawa ni watu ambao mara nyingi hawawezi kufikia vigezo vya chini vinavyotakiwa na sekta ya benki,” amesema.

 “Kwa hiyo tulianzisha mpango tuliouita Imbeju. Imbeju ni mbegu tunapanda mbegu ya mabadiliko ili kuleta ujumuishi wa kifedha kwa watu wengi zaidi, hasa wanawake na vijana. Kupitia Imbeju, tunafanya mambo kadhaa muhimu. “Tunawaunganisha wanawake katika vikundi rasmi, tunavisajili, na tunawapatia mafunzo ya kina ya kifedha pamoja na ujuzi wa kidijitali. Matokeo yake yamekuwa mazuri sana,” amesema.

Mapema,  Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Rosalynn Mndolwa – Mworia alisema kaulimbiu ya mwaka huu ya siku ya kimataifa ya wanawake duniani ya “Give to Gain,” inawakumbusha watu kuwa pale wanapotoa fursa inaweka urahisi kwa kupata bunifu.

“Pale tunapotoa mitaji, tunapata biashara. Pale tunapotoa mwonekano, tunapata kizazi kipya cha viongozi. Huu ni mwendelezo wa ushirikiano wa kimkakati wa ujenzi wa taifa,” alisema.

Akizungumzia miaka sita ya The Citizen Rising Woman amesema jukwaa hilo limekuwa kioo kinachoonyesha mabadiliko makubwa yanayofanyika nchini.