Mahakama yawaachia huru washtakiwa vurugu Oktoba 29

Mwanza. Watu saba waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya kufanya vurugu wakati wa Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025, wameachiwa huru na Mahakama ya Wilaya ya Magu, mkoani Mwanza, baada ya mahakama kutoridhika na ushahidi uliotolewa dhidi yao.

Washtakiwa hao pia walikuwa wakikabiliwa na tuhuma za kuchoma majengo ya Serikali, likiwemo la Mahakama ya Mwanzo Kisesa na ofisi nyingine za umma wilayani humo.

Uamuzi huo umetolewa Ijumaa, Machi 6, 2026, na Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Magu, Erick Kimaro, baada ya kusikiliza hoja za pande zote katika shauri hilo.

Washtakiwa walioachiwa huru ni Peter Masulya (33), mwalimu na mkazi wa Buzuruga, Sebastian Luchagula (47), mkazi wa Bujora, Zacharia Jumanne (20), mkazi wa Kanyama; Amos Mwita (29), mkazi wa Kisesa, Emmanuel Malagila (34), mkazi wa Nyankumbu; Delphine Muganyizi, mkazi wa Mwahuli A na Fred Ndege (29), mkazi wa Isangijo.

Akizungumza baada ya hukumu hiyo, kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi, Erick Mutta, amesema washtakiwa hao walitetewa na mawakili watatu, akiwamo yeye, Godfrey Kishosha na Gaston Galubindi.

Upande wa mashtaka uliongozwa na Wakili Japhet Ngusa, akisaidiwa na Wakili Nuru Julius.

Kwa mujibu wa Wakili Mutta, mahakama imejiridhisha pasipo kuacha shaka kuwa upande wa Jamhuri haukuweza kuthibitisha mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili washtakiwa hao saba.

Amesema katika shauri hilo, upande wa Jamhuri uliwasilisha mashahidi 14 wakilenga kuthibitisha tuhuma dhidi ya washtakiwa. Mutta amesema mashtaka hayo yalitokana na tukio la Oktoba 29, 2025, wakati wa uchaguzi mkuu, ambapo majengo kadhaa ya Serikali yalidaiwa kuchomwa moto.

Miongoni mwa majengo yaliyoharibiwa ni Mahakama ya Mwanzo Kisesa, Ofisi ya Tarafa ya Sanjo, Ofisi ya Kata ya Kisesa, pamoja na gari dogo lililokuwa limeegeshwa karibu na mahakama.

Washtakiwa walikamatwa siku hiyo ya Oktoba 29, na baada ya kusomwa kwa hoja za awali, mahakama ilipanga kusikiliza shauri hilo mfululizo kwa siku 21 kabla ya kupanga tarehe ya hukumu.

“Mahakama imejiridhisha pasipo shaka kuwa washtakiwa wote saba hawana hatia kutokana na mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili, hivyo inawaachia huru,” amesema hakimu.

Wakili Godfrey Kishosha ameishukuru mahakama kwa kutoa uamuzi huo, akieleza kuwa licha ya changamoto walizokutana nazo wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, wameridhishwa na hukumu iliyotolewa.

Katika vurugu hizo zilizotokea wilayani Magu, majengo kadhaa ya umma yaliharibiwa, yakiwemo Ofisi ya Kata ya Kisesa, Mahakama ya Mwanzo Kisesa, Ofisi ya Tarafa ya Sanjo, jengo la Kata ya Bujora, pamoja na ofisi za watendaji wa vijiji na shule mbili za msingi, ikiwemo Shule ya Msingi Bujora.

Ofisi hizo zinatoa huduma kwa wananchi zaidi ya 65,335, zikiwemo za kikodi, ardhi, vikundi vya maendeleo, huduma za ugani, mabaraza ya ardhi ya kata pamoja na huduma za kimahakama kwa wakazi wa maeneo hayo.

Desemba 5, 2025, wakati akitoa taarifa kwa Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, aliyekuwa mkoani Mwanza kukagua athari za vurugu hizo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, alisema vurugu hizo zilianzia Kisesa, wilayani Magu, ambapo vijana waliharibu mali kabla ya kusambaa katika maeneo mengine ya mkoa huo.