Arusha. Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) imebaini kuwepo kwa upungufu katika Katiba ya Tanzania unaozuia kupingwa kwa matokeo ya uchaguzi wa urais mahakamani, ikisema kifungu kinachokataza hatua hiyo kinakiuka haki za binadamu.
Katika hukumu iliyotolewa leo Ijumaa, Machi 6, 2026, kwenye kesi ya Ado Shaibu na wengine dhidi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mahakama hiyo imeamua kuwa kifungu cha 41(7) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kinakiuka haki ya kusikilizwa kwa haki.
Kifungu hicho kinazuia mahakama yoyote nchini kuhoji au kupokea shauri la kupinga ushindi wa mgombea wa urais uliotangazwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
Kesi hiyo yenye namba 046/2020 iliwasilishwa na wanasiasa sita ambao ni Ado Shaibu, Ezekiah Wenje, Omar Musa Makame, Dorah Wangwe, Enock Suguta, na Kassim Ali Haji.
Waombaji hao walidai kuwa haki zao za kiraia na kisiasa zilikiukwa kabla, wakati, na baada ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa mwaka 2020.
Katika uamuzi wake, mahakama imebaini kuwa kifungu cha 41(7) cha Katiba ya Tanzania kinakiuka kifungu cha 7(1) cha Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu, ambacho kinahakikisha haki ya mtu kusikilizwa kwa haki mbele ya chombo cha sheria.
Aidha, mahakama imesema kifungu hicho kinakiuka pia wajibu wa nchi wanachama uliowekwa katika kifungu cha kwanza cha mkataba huo, kinachozitaka nchi kuhakikisha haki zilizobainishwa katika mkataba huo zinalindwa na kuheshimiwa.
Kwa mujibu wa mahakama hiyo, kwa kuwa kifungu hicho kinazuia mahakama kuchunguza au kupokea mashauri yanayopinga ushindi wa mgombea wa urais, kinawanyima wananchi haki ya kisheria ya kufungua na kusikilizwa mashauri yao.
Kutokana na hilo, Mahakama imeitaka Tanzania ndani ya kipindi cha mwaka mmoja kurekebisha kifungu cha 41(7) cha Katiba yake na kuhakikisha kinazingatia viwango vya haki za binadamu vilivyowekwa katika Mkataba wa Afrika.
Mahakama hiyo pia imeamua kuwa kila upande utagharamia gharama zake katika shauri hilo.
Katika kesi hiyo, waombaji waliwakilishwa na mawakili wa haki za binadamu akiwamo Mohamed Salim Ally Muyenga na Donald Deya.
Kwa upande wa Serikali ya Tanzania, uwakilishi ulifanywa na Mwanasheria wa Serikali, Ally Possi, akisaidiwa na Sarah Duncan Mwaipopo, pamoja na Nkasori Sarakikya, ambaye ni Mkurugenzi wa Haki za Binadamu katika Wizara ya Katiba na Sheria.
Awali, katika hoja zao za utetezi, mawakili wa Serikali waliiomba mahakama kutupilia mbali kesi hiyo wakidai haikufuata taratibu za ndani za kisheria na kwamba mahakama hiyo haina mamlaka ya kuisikiliza.
Hata hivyo, mahakama ilitupilia mbali hoja hiyo na kueleza kuwa ina mamlaka ya kusikiliza maombi yanayohusu madai ya ukiukaji wa haki za binadamu zilizoainishwa katika mkataba wa Afrika, pamoja na mikataba mingine ya haki za binadamu ambayo Tanzania imeiridhia.
Aidha, mahakama imebaini kuwa ina mamlaka ya kisheria, muda, na kieneo kusikiliza shauri hilo, licha ya Tanzania mwaka 2019 kuondoa tamko chini ya Ibara ya 34(6) lililokuwa linawaruhusu watu binafsi na taasisi kufungua mashauri moja kwa moja katika mahakama hiyo dhidi ya Serikali.
Hata hivyo, kuhusu sharti la kukamilisha taratibu za ndani za kisheria kabla ya kuwasilisha shauri katika mahakama hiyo, mahakama ilikubaliana kwa sehemu na Serikali ya Tanzania kwamba baadhi ya madai ya waombaji hayakuwa yamekidhi kikamilifu sharti hilo.
Awali, waombaji hao waliwasilisha jumla ya madai 12 mbele ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, yakihusu madai mbalimbali ya ukiukwaji wa haki za kisiasa na kiraia wakati wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Miongoni mwa madai hayo ni kukamatwa kwa baadhi ya wagombea wa vyama vya upinzani, kusimamishwa kwa kampeni zao, pamoja na kuenguliwa kwa baadhi ya wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani.
Pia, walipinga uteuzi wa kada wa chama tawala kushika wadhifa wa Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, wakidai kuwa hatua hiyo ilidhoofisha uhuru na uaminifu wa taasisi hiyo muhimu katika kusimamia uchaguzi.
Madai mengine yalihusu kuwepo kwa vikwazo vya kisheria vinavyodaiwa kuzuia upingaji wa matokeo ya uchaguzi wa urais baada ya kutangazwa, pamoja na vitendo vya vurugu dhidi ya wagombea wa upinzani na wafuasi wao.
Waombaji pia walitoa madai ya kuwepo kwa vitendo vya rushwa ya kura, kujazwa kwa kura bandia kwenye masanduku ya kura, pamoja na uhesabuji wa kura uliodaiwa kufanyika kwa njia isiyo ya kawaida.
Aidha, waliibua madai ya kufungiwa kwa baadhi ya vyombo vya habari huru na kudhibitiwa kwa huduma za mawasiliano pamoja na mitandao ya kijamii katika kipindi cha uchaguzi.
Kwa mujibu wa waombaji, matukio hayo kwa pamoja yalidhoofisha uadilifu, uwazi, na uaminifu wa mchakato mzima wa uchaguzi nchini.
Kutokana na madai hayo, waliiomba mahakama itamke kuwa Tanzania ilikiuka wajibu wake chini ya mikataba mbalimbali ya haki za binadamu ya kikanda na kimataifa, ikiwamo Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu, Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa, pamoja na Itifaki ya Mkataba wa Afrika kuhusu Haki za Wanawake Barani Afrika, maarufu kama Itifaki ya Maputo.
Aidha, waliomba mahakama ithibitishe kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa haki za kushiriki katika uchaguzi, haki ya usawa, haki ya utu, pamoja na haki ya ushiriki wa kiraia.
Pia, waliiomba mahakama kuiamuru Serikali ya Tanzania kuwachukulia hatua wote waliohusika na vitendo hivyo, sambamba na kuchukua hatua za kikatiba, kisheria, na kiutawala kurekebisha kasoro zilizobainishwa.
Zaidi ya hayo, waombaji waliomba Serikali iwalipe fidia pamoja na kugharamia gharama za kesi hiyo.
Katika kesi hiyo, waombaji walikuwa wanawakilishwa na mawakili wa haki za binadamu akiwamo Chidi Anselm Odinkalu, Ibrahim Kane, na Donald Deya.
Akizungumza baada ya hukumu kutoka, wakili wa waombaji, Mohamed Salim, amesema wameridhishwa na uamuzi wa mahakama, licha ya hukumu hiyo kuchelewa kutolewa.
Amesema walitarajia hukumu hiyo ingetolewa kabla ya uchaguzi mkuu wa Tanzania Oktoba 29, 2025, lakini wamepokea uamuzi huo kwa matumaini mapya ya kuendelea kutafuta haki.
“Kwa kweli tulitarajia hukumu itoke kabla ya uchaguzi uliopita, lakini kwa sasa hatutarudi nyuma. Tutashughulikia madai mengine yaliyobaki kwa kufuata taratibu za ndani za kisheria,” amesema.
Ameongeza kuwa watajadiliana na wanasheria wenzao ili kubaini hatua zinazofuata katika mahakama za ndani kwa lengo la kuhakikisha haki inapatikana kwa manufaa ya vizazi vijavyo.