Tetesi zimeibuka zikidai kuwa kiongozi wa juu wa kijeshi nchini Iran, Esmail Qaani, huenda aliuawa na utawala wa nchi hiyo baada ya kutuhumiwa kuwa jasusi aliyesaliti kiongozi wa kidini aliyekuwa madarakani, Ali Khamenei.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo bado hazijathibitishwa rasmi, Brigedia Jenerali Qaani ambaye ni kamanda wa kikosi maalum cha Quds Force kinachohusishwa na Islamic Revolutionary Guard Corps (IRGC) alinusurika katika shambulio la ghafla lililoripotiwa kumuua Khamenei wiki iliyopita.
Hata hivyo, uvumi ulianza kusambaa usiku wa jana ukidai kuwa Qaani alitambuliwa kama mtu aliyetoa taarifa za siri kwa maadui wa Iran. Taarifa hizo ambazo hazijathibitishwa zinasema huenda alihukumiwa kifo baada ya kutoweka hadharani tangu kuzuka kwa mashambulizi ya kijeshi katika eneo hilo.

Kwa miaka kadhaa, Qaani amekuwa akizungumziwa katika duru za kisiasa na kijeshi kutokana na kunusurika katika mashambulizi kadhaa ya kulenga viongozi wa Iran na washirika wake. Hali hiyo ilimfanya apewe jina la utani la “The Man With Nine Lives” kutokana na uwezo wake wa kupona katika hatari kubwa.
Baadhi ya ripoti zisizothibitishwa zilizosambaa katika vyombo vya habari vya mtandaoni vya Kiarabu zimedai kuwa Qaani aliondoka katika eneo la tukio dakika chache kabla ya mlipuko uliodaiwa kumuua Khamenei katika makazi yake ya rais Jumamosi iliyopita.
Hii si mara ya kwanza kwa Qaani kuepuka kifo katika mashambulizi yanayodaiwa kufanywa na Israel dhidi ya viongozi wa Iran na washirika wake katika eneo la Mashariki ya Kati.

Awali iliripotiwa kuwa huenda alifariki pamoja na mrithi wa uongozi wa Hezbollah, Hashem Safieddine, kufuatia mlipuko wa bunker uliotokea wiki iliyopita. Hata hivyo, vyanzo kutoka Lebanon, Iraq na Iran vilidai baadaye kuwa hakuwepo katika mkutano huo.
Kadhalika, taarifa nyingine zinasema Qaani pia alinusurika shambulio jingine wiki iliyotangulia ambalo lilidaiwa kumuua kiongozi wa Hezbollah, Hassan Nasrallah.
Hadi sasa, mamlaka za Iran hazijatoa taarifa rasmi kuthibitisha au kukanusha madai hayo yanayoendelea kusambaa katika mitandao na vyombo vya habari vya kimataifa.