Mlipuko wa drone watikisa uwanja wa ndege Dubai

Dar es Salaam. Hali ya taharuki imetanda katika jiji la Dubai huko Falme za Kiarabu baada ya tukio la mlipuko mdogo kuripotiwa karibu na barabara ya kurukia na kutua ndege katika Uwanja wa Kimataifa wa Dubai.

Tukio hilo limesababisha kusimamishwa kwa muda kwa baadhi ya safari za ndege.

Taarifa za awali zinaeleza mlipuko huo umehusishwa na kitu kinachodhaniwa kuwa ndege isiyo na rubani (drone), kilichoanguka karibu na eneo la uwanja huo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Habari ya Dubai, operesheni za uwanja huo zilisitishwa kwa muda ili kutoa nafasi kwa mamlaka za usalama kufanya tathmini ya hali ilivyokuwa na kuhakikisha usalama wa abiria, wafanyakazi wa mashirika ya ndege pamoja na wahudumu wa uwanja huo.

Baadaye, mamlaka zilithibitisha kuwa tukio hilo lilikuwa dogo na lilitokana na mabaki ya kitu kilichoanguka baada ya kuingiliwa na mifumo ya ulinzi wa anga.

Taarifa hiyo imebainisha kuwa hakuna mtu aliyeripotiwa kujeruhiwa katika tukio hilo, huku uchunguzi zaidi ukiendelea ili kubaini chanzo halisi cha tukio hilo.

Mapema leo, Jumamosi Machi 7, 2026, katika mitandao ya kijamii, video mbalimbali zilisambaa zikionesha mlipuko mdogo ukifuatiwa na moshi mweusi uliokuwa ukitanda kwenda juu karibu na majengo ya abiria katika uwanja huo.

Video hizo zimeonesha tukio hilo likitokea karibu na eneo linalojulikana kama Concourse A, sehemu maalumu ya uwanja huo inayotumika kupokea na kuhudumia abiria pamoja na ndege zinazopakia au kushusha abiria.

Baadhi ya mashuhuda waliokuwapo karibu na eneo hilo wamesema walihisi hali isiyo ya kawaida kabla ya mlipuko huo kutokea.

“Nilisikia sauti kama ya injini ndogo inayofanana na ya drone ikikaribia, kisha ghafla kukatokea mlipuko mdogo na moshi kuanza kupaa,” amesema mmoja wa mashuhuda aliyekuwa karibu na eneo hilo wakati tukio linatokea.

Taarifa za mwanzo zimeeleza kuwa safari zote za ndege zilisimamishwa kwa muda, hatua iliyochukuliwa ili kuruhusu uchunguzi wa haraka kufanyika katika eneo hilo.

Hata hivyo, baadaye shirika la ndege la Emirates lilitangaza kuwa huduma za usafiri wa anga zilianza kurejea taratibu, ingawa baadhi ya safari zilicheleweshwa kutokana na usumbufu uliotokea.

Miongoni mwa safari zilizoathiriwa ni ndege ya EK001 iliyokuwa ikielekea Uwanja wa Ndege wa Heathrow nchini Uingereza, ambayo iliondoka baada ya kuchelewa kwa saa kadhaa.

Mchambuzi wa masuala ya usalama kutoka BBC News amesema picha zilizorekodiwa wakati wa tukio hilo zinaonesha kitu kikishuka kwa kasi kabla ya mlipuko mdogo kutokea.

Hata hivyo, amesema bado haijathibitishwa iwapo drone hiyo ilidunguliwa na mifumo ya ulinzi wa anga au kama ilikuwa ni jaribio la shambulio lililolengwa katika eneo hilo.

Tukio hilo limetokea katika kipindi ambacho hali ya kisiasa katika Mashariki ya Kati imeendelea kuwa tete.

Mvutano huo umehusishwa na mfululizo wa mashambulizi ya kujibu kati ya vikosi vinavyohusishwa na Iran na miundombinu ya kijeshi ya mataifa mengine katika eneo la Ghuba ya Uajemi.

Ripoti za kimataifa zinaeleza kuwa mvutano huo umeongezeka katika siku za karibuni kufuatia mashambulizi ya anga yaliyofanyika wiki moja iliyopita katika muktadha wa mgogoro unaohusisha mpango wa nyuklia wa Iran.

Kutokana na hali hiyo, tukio la mlipuko karibu na uwanja wa ndege wa Dubai limesababisha kuchukuliwa kwa tahadhari kubwa katika sekta ya usafiri wa anga, hasa kutokana na umuhimu wa uwanja huo ambao ni miongoni mwa viwanja vya ndege vyenye shughuli nyingi zaidi duniani.

Serikali ya Falme za Kiarabu imeendelea kusisitiza kuwa usalama wa anga ni kipaumbele kikubwa na kwamba mifumo ya ulinzi inaendelea kuimarishwa, ili kukabiliana na vitisho vinavyoweza kujitokeza.

Wataalamu wa usalama wamesema matumizi ya ndege zisizo na rubani katika migogoro ya kisasa yameongeza changamoto mpya kwa mifumo ya ulinzi wa anga.

Kwa mujibu wao, teknolojia hiyo inaweza kurahisisha mashambulizi kwa sababu vifaa hivyo vinaweza kupenya mifumo ya kawaida ya ulinzi wa anga na kufika katika maeneo nyeti bila kutambuliwa mapema.

Tukio hilo, kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya usalama, linaonesha jinsi teknolojia ya kisasa ya kivita inavyoendelea kubadilisha sura ya migogoro ya kimataifa na kuongeza wasiwasi katika sekta ya usafiri wa anga duniani.

Mashirika ya habari ya kimataifa yanaendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya tukio hilo lililovuta hisia za wengi kutokana na umuhimu wa jiji la Dubai katika usafiri na biashara ya kimataifa.